MAANDAMO YA KUMPOKEA DK NUNDU YAPIGWA MARUFUKU

  
JESHI la Polisi mkoani hapa, limezuia maandamano ya kumpokea aliyekuwa Waziri wa Miundombinu na Mbunge wa Tanga Mjini, Omari Nundu (pichani) yaliyokuwa yafanyike jana.

Taarifa iliyotolewa na msemaji wa kamati ya maandalizi ya mapokezi ya mbunge huyo, Ahmed Omari, ilisema Jeshi la Polisi liliwapelekea taarifa ya kusitisha kibali cha maandamano hayo kilichokuwa kimetolewa awali.

Hata hivyo, Omari alidai polisi katika taarifa yao ya zuio hilo, hawakueleza sababu za kuzuiwa kwa maandamano hayo na kwamba kitendo hicho kimewasababishia hasara na usumbufu mkubwa.

“Tumeshangazwa sana na Jeshi la Polisi, kwani wiki iliyopita walitupa kibali na kutuhakikishia ulinzi wa kutosha, lakini jana wametuzuia,” alisema na kudai kuwa hawawezi kukubalina na zuio hilo.

Kutokana na kufutwa kwa mapokezi hayo, kamati hiyo inafanya mpango wa kukutana na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Constantine Massawe ili kujua sababu, kisha watazungumza na vyombo vya habari juu ya hatua watakayoweza kuchukua.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Mussa Marambo aliiambia Tanzania Daima kuwa, wamefuta kibali kilichotolewa awali kuruhusu maandamano hayo, kwa madai ya kuhofia usalama wa mbunge huyo.

“Ni kweli tumezuia kibali cha maandamano hayo, kwa sababu ya kuhofia usalama wa mbunge, kwani walioandaa ni kundi tu la watu wa kawaida ambao hatujui hasa nini lengo lao,” alisema Marambo.

Kaimu Kamanda huyo alisema kama ingekuwa maandamano hayo yametayarishwa na chama chake cha CCM, kusingekuwa na hofu ya kuyazuia, kwa sababu tukio lolote la kuhatarisha usalama wa mbunge huyo lingetokea, chama ndicho kingeweza kuwajibika.

Ijumaa iliyopita, wajumbe wa kamati ya mapokezi iliyoundwa na watu watatu, ikiongozwa na Mbega Hassan, walisema maandamano hayo yaliandaliwa na wapiga kura wa Jimbo la Tanga, kwa lengo la kumfariji mbunge wao kwa kuachwa katika baraza jipya la mawaziri.

Walisema maandamano hayo hayakukihusisha chama chochote cha siasa, kwani wapiga kura bila kujali itikadi zao, waliamua kuyafanya ili kumpa nguvu ya kutekeleza ahadi zake za ubunge alizotoa wakati wa kampeni za kuwania nafasi hiyo.

Akizungumza kwa njia ya simu na Tanzania Daima, Nundu ambaye tangu kuenguliwa kwake hajawasili mkoani hapa, kuelezea kuhusu kadhia hiyo, alijibu kwa kifupi kwamba hana shughuli na mwandishi yeyote wa gazeti, kisha akakata simu.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

HATUTOPAKI BASI DHIDI YA YANGA-MOKWENA

“PEMBA SALUTI KWENU” DK. NCHIMBI*

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA