MKAPA KUTINGA KORTINI

RAIS mstaafu, Benjamin Mkapa, Mei 8, anatarajiwa kufika katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, kutoa ushahidi wake katika kesi ya uhujumu uchumi na kuisababishia serikali hasara ya zaidi ya sh bilioni tatu inayomkabili aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia, Profesa Costa Mahalu.

Hayo yalisemwa jana saa tisa alasiri na mawakili wa Mahalu, Mabere Marando na Alex Mgongolwa, nje ya viwanja vya mahakama hiyo ikiwa ni dakika tano tu tangu Hakimu Mkuu Mfawidhi wa mahakama hiyo Elvin Mugeta kuahirisha usikilizwaji wa kesi hiyo ambayo ulianza jana.

Hakimu Mugeta ambaye anataka kesi hiyo imalizike haraka kwani ni ya muda mrefu, Mei 7 mawakili wa upande wa jamhuri kutoka ofisi ya Mkurugenzi wa Mshtaka nchini, Vicent Haule na Ponsian Lukosi, kwa kushirikiana na wa Taasisi ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa, Ben Lincoln, watamaliza kuwahoji washtakiwa, Mahalu na aliyekuwa Mkurugenzi wa Fedha wa Ubalozi huo, Grace Martin.

Marando akiambatana na Mahalu aliwaambia waandishi wa habari mara tu baada ya Hakimu Mugeta kuahirisha kesi kuwa shahidi anayekusudiwa kuletwa ni Rais mstaafu, Benjamin Mkapa, ambaye alidai tayari amekubali kuwa shahidi wa Mahalu.

Mapema asubuhi jana Wakili wa Serikali, Vicent Haule, Lukosi na Lincoln, walimhoji Mahalu ni kwa nini akiwa Balozi nchini Italia, alikubali kununua jengo la ubalozi kwa kutumia mikataba miwili na kama serikali ilikuwa ikiitambua?

Akijibu maswali hayo Mahalu alidai kuwa ni kweli jengo la ubalozi wa Italia lilinunuliwa kwa mikataba miwili na serikali ya Tanzania akiwemo aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Jakaya Kikwete, na Rais wa wakati huo Mkapa ndiyo waliompa baraka zote.

Mahalu alisema alikuwa akiwaarifu kwa maandishi, kwa njia ya simu, mazungumz
o ya ana kwa ana kuhusu manunuzi yale na kwamba wao ndiyo waliokuwa wakimpa maelekezo yote.
“Nasisitiza tena kama alivyosema Kikwete Juni mwaka 2004 bungeni kuwa taratibu na sheria ya manunizi ya umma zilifuatwa katika ununuzi wa jengo hilo ….na kule Italia suala la mikataba miwili siyo kosa na ndiyo maana hata serikali ya Italia haikunishtaki kwa kununua jengo lile kwa mikataba miwili,” alidai Profesa Mahalu.

Akipangua hoja ya wakili Haule kuwa ni kwa nini barua ya serikali inaonyesha ubalozi wake ulitenguliwa Machi mwaka 2006 lakini hadi Aprili mwaka 2006 aliendelea kuwa balozi na kupewa tuzo mbalimbali na serikali ya Italia, Balozi Mahalu alisema kwanza serikali ilikosea kutumia sheria za kutengua ubalozi wake kwani ilimuandikia barua ya kutengua ubalozi wake Machi lakini ikashindwa kupeleka barua hiyo Wizara ya Mambo ya Nje ya serikali ya Italia kuifahamisha uamuzi huo.

Alisema kwani kwa mujibu wa kanuni na masuala ya kidiplomasi serikali husika inapotengua ubalozi wa balozi wake inapaswa ipeleke taarifa hiyo kwenye wizara ya mambo ya nje ya nchi anayofanyia kazi na kisha wizara hiyo itatakiwa ipeleke taarifa yake kwa Mkuu wa Itifaki na kisha mkuu huyo wa Itifaki kwa niaba ya nchi husika itengue ubalozi wa balozi huyo anayefanya kazi nchini kwako, lakini serikali ya Tanzania hilo haikulifanya na ndiyo maana hadi April 2006 serikali ya Italia ilikuwa ikimtambua kama balozi wa Tanzania.Chanzo; Tanzania Daima

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

KOCHA BENCHIKHA AMESEPA

MASHUSHUSHU WA MAMELODI WALIKUJA KUTUPELELEZA: HERSI