Mkulima auawa na mfugaji, yazuka mapigano

Waandishi Wetu
MAPIGANO makali kati ya wakulima na wafugaji yamezuka katika eneo la Ikwiriri wilayani Rufiji, Mkoa wa Pwani na kusababisha vifo, majeruhi, nyumba kuchomwa moto, maduka kuvunjwa na barabara kufungwa kwa zaidi ya saa sita.

Chanzo cha mapigano hayo, kinaelezwa kuwa ni kutokana na kuuawa mkulima wa Ikwiriri, Shamte Seif (60) na wafugaji katika ugomvi uliotokana na ng’ombe kuingia kwenye shamba lake.

Hadi jana jioni, watu kumi na moja walikuwa wameripotiwa kujeruhiwa, tisa kati ya hao wamelazwa katika Kituo cha Afya Ikwiriri na wawili walihamishiwa katika Hospitali ya Misheni Mkuchu, Ikwiriri baada ya hali zao kuwa mbaya.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Ernest Mangu alithibitisha kuuawa kwa Seif na kusema wafugaji wawili wanashikiliwa na polisi.

Habari zilizopatikana kutoka Ikwiriri zinasema, baada wananchi kupata taarifa za kifo cha mkulima kisha kushiriki katika mazishi yake, ndipo walipoanza kuwasaka wafugaji popote walipo.

Bila kujali kama walihusika au la katika mauaji hayo, wakulima hao wakiwa na silaha za jadi ikiwemo mishale, walivamia nyumba kadhaa zinazodaiwa kuwa za wafugaji na kuzichoma moto.

Taarifa zinasema wakulima hao waliungana na wananchi wengine kuwawinda wafugaji popote walipo kwa lengo la kulipiza kisasi cha mauaji hayo.

Aidha, walikwenda kwenye Kituo cha Polisi Ikwiriri wakitaka wakabidhiwe watuhumiwa wa mauaji ya mkulima huyo ili wawashughulikie.

Katika vurugu hizo, kundi hilo la wapiganaji lilivunja duka la dawa lililopo Ikwiriri na kupora dawa zote zilizokuwemo.

Pia kundi hilo liliweka mawe na magogo kwenye Barabara Kuu itokayo Dar es Salaam kwenda Mtwara na kusababisha magari kusimama kwa zaidi ya saa sita.

Wakati magari hayo yakiwa yamesimama, wapiganaji hao walikuwa wakiyarushia mawe na kusababisha mengine kugeuza na kurudi yalikotoka.

Habari zinasema magari mengi yaliharibiwa vibaya likiwemo moja la aina ya Toyota Noah hali iliyomlazimu  mmiliki wake, kupiga risasi takriban 10 hewani kwa lengo la kuwatawanya wapiganaji hao, hali iliyosababisha eneo hilo kuwa kama uwanja wa vita.

Baadhi ya wafugaji katika eneo hilo na maeneo ya jirani ilibidi watelekeze mifugo yao na kujificha kunusuru maisha yao.

“Ninakupigia simu nikiwa nimejificha porini, hali huku ni mbaya tunaomba msaada wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) waje kuzima ghasia hizi,” alisema mkazi mmoja wa Ikwiriri ambaye aliomba jina lake lisitajwe gazetini.

Vurugu hizo zilililazimu Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani kuomba nguvu ya ziada kutoka Makao Makuu ya Jeshi hilo, Dar es Salaam.

Helikopta moja na magari yaliyokuwa na Askari wa FFU zaidi ya 80 yalitolewa kwenda kuongeza nguvu.
Taarifa zaidi kutoka Ikwiriri zinasema, vurugu hizo ni kubwa ambazo hazijawahi kutokea katika eneo hilo.

Inadaiwa kwamba katika siku za hivi karibuni kumekuwa na migogoro ya mara kwa mara kati ya jamii hizo na kwamba wakulima wamekuwa wakikasirishwa na vitendo vya wafugaji kupitisha mifugo kwenye mashamba yao.
Migogoro hiyo imekuwa ikizidi pale mifugo hiyo ilipobainika kula mazao yao.

Hata hivyo, wafugaji hao wanadaiwa kuwa wamekuwa wakiendelea kupitisha mifugo yao kwenye mashamba ya wananchi.

Mkuu wa Mkoa afika
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mwantumu Mahiza alifika kwenye eneo la tukio na kuwasihi wakulima hao kuacha kujichukulia sheria mkononi.

Akiwa hapo, Mahiza alielezwa kuwa viongozi wa wilaya hiyo wamekuwa wakipewa malalamiko kuhusu migogoro kati ya wakulima na wafugaji, lakini wamekuwa hawaitatui.

Walisema mbaya zaidi wafugaji wamekuwa wakipendelewa zaidi kwa sababu wana uwezo kifedha, ambazo wamekuwa wakizitumia kutoa rushwa.

Wakataka viongozi waandamizi karibu wote wa wilaya hiyo waondolewe kwa sababu wameshindwa kazi.
Habari hii imeandaliwa na Raymond Kaminyoge, Julieth Ngarabali na Amini Yasin, Pwani.

 

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA

DKT NCHIMBI ASHIRIKI MAZISHI YA ASKOFU.GACHUMA WA KANISA LA NLGCC

π™‚π˜Όπ™ˆπ™Šπ™‰π˜Ώπ™„ π™†π˜Όπ˜Ύπ™ƒπ™€π™•π˜Ό π™†π™„π˜½π™„π™‰π™‚π™’π˜Ό.