NCHUNGA: TUTAFUKUZA WACHEZAJI WENGI, TUMEGUNDUA HUJUMA


Nahodha wa Yanga, Nsajigwa Shadrack akijaribu kumdhibiti Emmanuel Okwi wa Simba katika mechi ya jana.

UONGOZI wa Yanga umesema kwamba umepata taarifa za awali, ya kuwa, mechi yao ya jana dhidi ya mahasimu wao wa jadi, Simba waliyofungwa mabao 5-0, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuna baadhi ya wachezaji walihujumu timu.
 
Mwenyekiti wa Yanga, Wakili Lloyd Baharragu Nchunga ameiambia mchana huu kwamba, kufuatia taarifa hizo, Kamati ya Ufundi inakutana leo jioni na benchi la Ufundi kujadili zaidi na pia kuandaa taarifa nzima ya msimu.
 
Nchunga alisema baada ya Kama ya Ufundi kwa pamoja na benchi la Ufundi kukamilisha taarifa hiyo, wataiwasilisha kwa Kamati ya Utendaji, ambayo nayo itakutana kesho kujadili kwa kina ili kuchukua hatua.
 
“Kuna uwezekano tukawafukuza wachezaji wengi sana, yaani sisi watu wa Yanga ni wa ajabu sana, sijui Uyanga wetu ukoje, nashindwa hata kuelewa,”alisema Nchunga.
 
Nchunga alisema Waandishi wa Habari wenye kutaka ukweli zaidi juu ya hujuma hizo wanaweza kumfuata kipa, Yaw Berko na kumdadisi kwa nini aligoma kuendelea na mechi.
 
Berko hakurejea uwanjani baada ya dakika 45 za kipindi cha kwanza, Yanga ikiwa nyuma kwa bao 1-0 na nafasi yake ikachukuliwa na kipa wa tatu, Said Mohamed aliyetunguliwa mabao manne.
 
“Berko aligoma kuendelea, alisema anaomba atoke na hakuwa ameumia wala nini, alisusua tu, unajua yule ni mlokole safi, ila baada ya kesho kila kitu kitajulikana,”alisema Nchunga.
 
Alipotakiwa kuwataja baadhi ya wachezaji wanaohusishwa na tuhuma hizo, Nchunga alisema; “Siwezi kusema chochote, ila kwa sasa unaweza kuangalia tu uchezaji wa mtu kwenye mechi ya jana na ukapata jibu. 
 
Yanga kama Yanga itatoa taarifa rasmi baada ya taratibu zote kukamilika na wachezaji wahusika kuitwa kuhojiwa sambamba na kuonyeshwa ushahidi ambao hadi sasa tumekwishaukusanya,”alisema.
 
Yanga jana ilifungwa 5-0 na wapinzani wao wa jadi, Simba waliotawazwa rasmi kuwa mabingwa wapya wa Ligi Kuu kwa kumaliza ligi wakiwa na pointi 62.
 
Simba ilipata mabao yake kupitia kwa, Emmanuel Okwi dakika ya kwanza na Patrick na 65, Mafisango dakika ya 58 kwa penalti,
Juma Kaseja kwa penalti pia dakika ya 69 na Felix Sunzu kwa penalti dakika ya 74.
 
Wakati Simba ikimaliza na pointi zake 62, Azam imekuwa ya pili kwa pointi zake 56 baada ya jana kuifunga Kagera Sugar mabao 2-1 Uwanja wa Chamazi na Yanga imeshika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 49.
 
Mwaka 1977, baada ya Yanga kufungwa 6-0 na Simba ilivunja timu na kuunda kikosi kipya, ambacho kilirejesha heshima ya klabu.
 
Mwaka 1994, Yanga ilifungwa 4-1 na Simba na baada ya mchezo huo, ilivunja tena kikosi kutokana na tuhuma za kuhujumiwa na wachezaji wake, safari hiyo ikidaiwa aliyekuwa mfadhili mmoja wa klabu hiyo mwenye asili ya Kiasia, aliwapa fedha wachezaji wafungwe ili kuwakomoa viongozi katika vita iliyokuwa inaendelea baina yao.
 
Baadhi ya wachezaji waliobakishwa kikosini walikuwa ni Kenneth Mkapa, Constantine Kimanda, Sekilojo Chambua, Sanifu Lazaro ‘Tingisha’ na Mohammed Hussein ‘Mmachinga’, wengine wote akiwemo kipa Steven Nemes, Said Mwamba ‘Kizota’ (sasa marehemu) walitimuliwa kwa tuhuma hizo.
 
Baada ya hapo, Yanga iliundwa na wachezaji waliokuwa wakiandaliwa na Tambwe Leya (sasa marehemu) katika kikosi cha pili, ambao ni pamoja na Godwin Mashoto (sasa marehemu), Mzee Abdallah, Anwar Awadh, Maalim Saleh ‘Romario’, Nonda Shaaban na wengineo, waliosajiliwa kutoka timu mbalimbali kuimarisha kikosi kama Bakari Malima, Reuben Mgaza waliotoka Pan African.
 
Kipigo cha sasa cha Yanga kinakuja katika mazingira sawa na kipigo cha 1994, kwani klabu inakabiliwa na mgogoro na baadhi ya viongozi wa zamani wa klabu hiyo na kundi la Wazee la klabu hiyo kuwa kwenye vita ya kumng’oa Nchunga madarakani.
 
Mapema kabla ya mechi hiyo, Wazee wa Yanga walikaririwa wakisema hata kama Yanga ikiifunga Simba jana, lazima Nchunga ataondoka- kauli ambayo inatafsiriwa kama nia yao ilikuwa ni timu ifungwe ili kumchongea kwa wapenzi wa timu hiyo Mwenyekiti huyo aondolewe kwa nguvu.Kwa hisani ya Bin Zubeiry Blog

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

HATUTOPAKI BASI DHIDI YA YANGA-MOKWENA

“PEMBA SALUTI KWENU” DK. NCHIMBI*