TAKWIMU YAWAMWAGIA WABUNGE MABILIONI YA FEDHA KUHAMASISHA SENSA

WAKATI Serikali ikidai kuwapo kwa nakisi katika bajeti ya kuendesha sensa nchini, imebainika kuwa Ofisi ya Taifa ya Sensa, imewamwagia wabunge mamilioni ya shilingi kwa ajili ya kufanya uhamasishaji kwenye majimbo hayo.

Aliyekuwa Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo akizungumza mwezi jana mjini Dodoma alisema gharama za sensa zimeongezeka kwa Sh27.1 bilioni hivyo kufanya bajeti hiyo kuwa Sh141.5 bilioni 141.5 kutoka Sh114.4 bilioni za awali.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili na kuthibitishwa na Ofisi ya Sensa kwa upande mmoja na Ofisi ya Bunge kwa upande mwingine, umebaini kuwa kila mbunge katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amepewa kiasi cha Sh1 milioni kwa ajili ya kazi hiyo.

Idadi ya wabunge hivi sasa ni 350, kwa maana hiyo fedha zilizotolewa na ofisi ya sensa kwenda kwa ofisi ya Bunge kisha kugawanya kwa wabunge hao ni Sh350 milioni.

Kamishna wa Sensa, Hajat Amina Said Mrisho alikiri kufanyika kwa malipo hayo kwa kile alichodai kuwa ni kuwawezesha wabunge kushiriki kazi ya kuhamasisha watu ili kufanikisha kazi hiyo.
“……Ndiyo ni kweli kwamba tulitoa fedha kwa wabunge ijapokuwa siwezi kujua ni kiasi gani lakini kila mbunge alipewa shilingi milioni moja kwa ajili hiyo, tunafanya hivyo kwa lengo la kuwawezesha kuwahamasisha wananchi,” alisema Hajat Mrisho.

Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah alisema fedha hizo zilipitia katika ofisi yake tu kwa ajili ya kuwafikia wabunge kama Ofisi ya Sensa ilivyoomba.

“Kama watu wa sensa wamekwambia kwamba walizileta kwetu basi ndiyo hivyo, si kwamba nakataa hapana, kwa hiyo na sisi tulivyozipokea tukawafikishia walengwa,” alisema Dk Kashililah na kuongeza:

“Kama fedha hizo zingekuwa ni za Bunge ningekuwa na maelezo zaidi, lakini kusema kweli zimepitia tu kwa hiyo siwezi kuzisemea zaidi.”

Hata hivyo baadhi ya wabunge waliohojiwa walionyesha kushangazwa na taarifa hizo huku wengi wakisema kuwa hawafahamu kama kuna fedha hizo na hawajapewa taarifa yoyote kuhusu suala hilo.

Malipo ya fedha hizo pia yanatia shaka kwani katika bajeti ya uhamasishaji wa sensa hakuna kipengele kinachoonyesha kwamba wabunge wanapaswa kupewa malipo hayo.
Fedha hizo zililipwa kupitia Ofisi ya Bunge baada ya kumalizika Kikao cha Bunge kilichopita, ambacho pamoja na mambo mengine, kilijadili Ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), mjadala ambao ulizaa mabadiliko makubwa ya Baraza la Mawaziri.

Bajeti ya sensa
Mkulo alisema Serikali ilipanga kukabiliana na nakisi hiyo ya Sh27.1 bilioni kwa kupunguza baadhi ya matumizi katika eneo la posho za vikao vya kamati za sensa kuanzia ngazi ya taifa na wilaya.

Hatua nyingine alizotaja ni kupunguza baadhi ya vifaa vya uhamasishaji kama vile khanga na vitenge na kutumia malori ya Serikali badala ya kukodi kwa ajili ya kusafirishia vifaa.

Alisema hatua hizo zingewezesha kukoa kiasi cha Sh3.7 bilioni hivyo kubaki nakisi ya Sh23.3bilioni ambazo zingetafutwa kwa njia mbalimbali.

Hajat Mrisho alipoulizwa kama kutoa fedha kwa wabunge ni kuongeza mzigo kwenye bajeti alijibu: “Uhamasishaji ni moja ya mambo muhimu katika sensa.”

Aliongeza: “Fedha hazitolewi kwa wabunge tu, hata kwenye mikoa. Kwa mfano, tulipokuwa Tabora tuliupa mkoa Sh20 milioni kwa ajili ya kuuwezesha kufanikisha shughuli husika, tutaendelea kutoa fedha kwa ajili ya shughuli hizi zitakavyokuwa zikiendelea.”

Hata hivyo, katika bajeti ya uhamasishaji wa shughuli za sensa ambayo ni Sh4.42 bilioni, hakuna kipengele cha malipo kwa wabunge kwa ajili ya kufanya uhamasishaji.

Badala yake, bajeti hiyo ya uhamasishaji imetenga fedha kwa ajili ya vifaa vya uhamasishaji (Sh3.95 bilioni), uimarishaji wa kitengo cha habari na mawasiliano kwa umma (Sh1.97 milioni) na matangazo kwenye vyombo vya habari (Sh74.8 milioni).

Gharama nyingine za uhamasishaji ni mikutano ya kuwaelimisha viongozi wa dini (Sh20.76 milioni), vipindi vya radio na televisheni (Sh57 milioni), kukodi magari na vifaa vya matangazo (Sh90 milioni) na gharama za mikutano ya uhamasishaji wilayani na mikoani (Sh117.3 milioni).

Fedha za sensa zinatolewa na Serikali ambayo imechangia asilimia 77 ya fedha zote na wadau wa maendeleo ambao ni Shirika la Umoja wa Mataifa linalojishughulisha na Idadi ya Watu (UNFPA), Serikali ya Uingereza kupitia Shirika la Maendeleo la Kimataifa (DFID) na Serikali ya Japan wametoa asilimia 23 ya bajeti nzima.

Wasemavyo wabunge
Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe alikiri Ofisi ya Sensa kuwaingizia kwenye akaunti za wabunge kiasi hicho cha fedha lakini akasema kuwa yeye amezirejesha kwa Katibu wa Bunge.

“Hii ni hongo, ni rushwa ya wazi kwa nini wabunge wapewe fedha hizi sasa? Mimi kweli niliwekewa lakini kwa kufahamu kwamba si sahihi nimezirejesha kwa Katibu wa Bunge, akitaka awarudishie wahusika,” alisema Zitto.

Naye Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Stella Manyanya, alisema wabunge walipewa semina na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) na kisha kuwataka wakirudi kwenye majimbo yao watoe elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa sensa na kuwahamasisha kushiriki kwa hali na mali.

“Nakumbuka baada ya semina hiyo wabunge waliwataka NBS kuwawezesha ili wawafikie wananchi kutoka na maeneo yao kuwa makubwa na wao NBS walisema wataangalia angalau namna ya kuchangia mafuta, lakini kwa kweli sijui kama kuna fedha ambazo zimeshatolewa,” alisema Manyanya na kuongeza:

“Kama wameshatoa nitawashukuru kwa kuwa watakuwa wamefanya vyema kwani kweli elimu kwa wananchi ni muhimu na maeneo ya wabunge ni makubwa.”

Kwa upande wake Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR Mageuzi), David Kafulila alisema hana taarifa zozote juu ya jambo hilo zaidi ya kujua kuwa, mbunge ni mjumbe wa kamati ya sensa ya wilaya.

Mbunge Wawi (CUF), Hamad Rashid Mohamed alisema hana taarifa zozote juu ya suala hilo, zaidi ya kujua kuwa NBS walifanya semina ambayo hata hivyo haikuwa na posho.

“Walifanya semina bungeni na siku hizi hata posho huwa hawatoi na hizo fedha unazosema mimi sijaziona kabisa,” anasema Mohamed.

Katika hotuba yake ya kufunga mwaka 2011, Rais Jakaya Kikwete alitangaza rasmi dhamira ya Serikali kufanya Sensa ya Watu na Makazi nchini kote Agosti 26 Agosti mwaka huu.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

KOCHA BENCHIKHA AMESEPA

MASHUSHUSHU WA MAMELODI WALIKUJA KUTUPELELEZA: HERSI