UVIMA yaazimia kujiunga na NHIF

Na Mwandishi Wetu
VIONGOZI na wawakilishi wa Vikundi vilivyounganishwa na Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) wamekubaliana kwa kauli moja kujiunga na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) mara baada ya kumailika kwa taratibu zinazotakiwa.
 
Hatua hiyo waliifikia Dar es Salaam juzi wakati wa mafunzo yaliyotolewa na Mfuko huo kuhusiana na huduma za matibabu za uchangiaji kupitia Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF).
 
Washiriki hao zaidi ya 40 kwa pamoja walisema wako tayari kujiunga na NHIF kwa kuwa ina manufaa makubwa na itawawezesha kuwa na uhakika wa kupata matibabu kote nchini lakini pia kunufaika zaidi na fao la wastaafu ambalo NHIF inalitoa kwa wanachama wake.
 
"NHIF ina manufaa makubwa kwa kuwa ina wigo mpana wa huduma zake ambazo unaweza kuzipata popote na inatibia hata magonjwa makubwa hivyo tuko tayari kujiunga na kuhamasisha zaidi wenzetu kwa kuwa mtaji mkubwa wa kila mwananchi ni afya yake hasa kwa kuwa na uhakika wa kupata matibabu," alisema Tatu Ngao ambaye ni Mwenyekiti wa Umoja wa Vikundi vya WAMA.
 
Akiwasilisha mada kwa wanavikundi hao, Kaimu Mkurugenzi anayeshughulikia Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) Rehani Athuman, aliwaeleza kuwa endapo wakijiunga na Mfuko huo wataweza kunufaika wao wakiwa kama wachangiaji, wenza wao na wategemezi wanaotambulika kisheria.
 
Aliwaomba washiriki hao kuona umuhimu wa kujiunga na mifuko hiyo na kuelimisha wanachama wengine katika vikundi kuhusu umuhimu wa kuchangia gharama za matibabu kabla ya kuugua lakini pia kuendeleza kushiriki katika shughuli za usimamizi wa huduma za matibabu kupitia kamati za Afya za vituo vya maeneo wanayoishi.
 
(WAMA mkijiunga mtakuwa kichocheo kikubwa hata cha wengine kujiunga na kunufaika na huduma zetu lakini pia itawasaidia sana kufanya shughuli zenu za ujasiliamali mkiwa na uhakika wa matibabu," alisema Rehani.
 
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Uhai wa Mfuko ambaye pia alimwakilisha Mkurugenzi Mkuu, Michael Mhando, aliwahakikishia washiriki hao kuwa watakapojiunga watapata huduma zote zinazotolewa na Mfuko huo.
 
"Azimio lenu la kukubaliana kwa pamoja kujiunga na NHIF limetupa faraja kwani nia yetu ni kuona Watanzania wakiwa na uhakika zaidi wa kupata matibabu wanapougua hivyo sisi kama Mfuko tunakwenda kulifanyia kazi haraka ili muweze kufikia azimio lenu," alisema Mhando.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA

DKT NCHIMBI ASHIRIKI MAZISHI YA ASKOFU.GACHUMA WA KANISA LA NLGCC

π™‚π˜Όπ™ˆπ™Šπ™‰π˜Ώπ™„ π™†π˜Όπ˜Ύπ™ƒπ™€π™•π˜Ό π™†π™„π˜½π™„π™‰π™‚π™’π˜Ό.