WAKE WA VIONGOZI WAIPIGA TAFU TAIFA QUEENS

MKE wa Waziri Mkuu, Mama Tunu Pinda amewashukuru Watanzania kwa michango yao kwa ajili ya kuiandaa timu ya Taifa ya Netiboli (Taifa Queens) iweze kushiriki mashindano ya Afrika yanayotarajiwa kuanza Mei 8-12, mwaka huu jijini Dar es Salaam.
 
Ametoa shukrani hizo leo mchana (Jumanne, Mei Mosi, 2012) wakati alipokuwa akizungumza na wachezaji wa timu hiyo katika kambi yao iliyoko Shule ya Filbert Bayi, Kibaha, mkoani Pwani. Mama Pinda ni Mwenyekiti wa Kamati ya Iwezeshe Taifa Queens Ishinde.
 
Mama Pinda ambaye amewaongoza wake wa viongozi mbalimbali zaidi ya 20 ambao ni wanachama wa New Millenium Group, alikabidhi katoni 40 za maji ya kunywa kwa Mwenyekiti wa Chama cha Netiboli (CHANETA), Bibi Anna Bayi na mbele ya wanamichezo hao.
 
Mama Pinda alisema wamebakiza kiasi cha sh. milioni 27 tu ambazo ni ahadi na kwamba kama zote zitatimizwa wiki hii, hakutakuwa na taabu ya kufanikisha mashindano hayo.
 
“Gharama za kuwatayarisha wachezaji na kuendesha mashindano haya hapa nchini zilikuwa jumla ya sh. 158,430,000/-. Kati ya hizo, gharama za kuwaweka wachezaji kambini kwa matayarisho ni sh. 82,650,000/- na gharama ya kuendesha mashindano kwa siku tano ni sh. 75,780,000/-,” alisema.
 
Aliwashukuru  baadhi ya wafadhili ambao walijitolea kulipia moja kwa moja gharama zilizokuwa kwenye bajeti kama vile kulipia gharama za usafiri, uwanja wa michezo, viatu vya michezo, mipira, jezi, track-suits na vifaa vingine.
 
Akitoa mchanganuo wa fedha ambazo zimekwishapokelewa, Mama Pinda alisema: “Kwa waliojitolea vifaa mbalimbali, hadi sasa tunakiri kupokea vitu vyenye thamani ya sh. 53,080,000/- na wale waliojitolea kwa fedha taslimu tumeshapokea jumla ya sh. 77,800,000/-. Vilevile, tunazo ahadi zenye thamani ya sh. 27,550,000/-. Kwa kifupi hali ya kifedha kwa sasa si mbaya kwani tunaamini walioahidi watatimiza ahadi zao ndani ya wiki hii kabla mashindano hayajaanza”.
 
Mapema, katika risala yao, wachezaji hao walisema wanakabiliwa na uhaba wa vifaa vya mbalimbalim kama vile raba, kamba za kuruka, mipira na chupa maalum za maji. Timu ya Taifa Queens ambayo ina wachezaji 16 na maafisa sita, inatarajiwa kuhitimisha kambi Mei 6, 2012 na Mei 7, 2012 itahamia jijini Dar es Salaam ili kushiriki mashindano hayo.
 
Baadhi ya wake wa viongozi walioambatana na Mama Tunu Pinda ni Wake wa Makamu wa Rais, Bi Zakia na Bi Asha Bilal, Mama Anna Mkapa, Mama Husana Kawawa, Mama Regina Lowassa, Mama Sophia Mukama, Mama Janet Magufuli, Mama Josephine Makamba, na baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Iwezeshe Taifa Queens Ishinde.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA

DKT NCHIMBI ASHIRIKI MAZISHI YA ASKOFU.GACHUMA WA KANISA LA NLGCC

π™‚π˜Όπ™ˆπ™Šπ™‰π˜Ώπ™„ π™†π˜Όπ˜Ύπ™ƒπ™€π™•π˜Ό π™†π™„π˜½π™„π™‰π™‚π™’π˜Ό.