YANGA KWAWAKA LEO, WANACHAMA WATANGAZA KUMTIMUA NCHUNGA

Sunday, May 20, 2012

 Mwenyekiti wa Kamati ya Wazee wa Klabu ya Yanga, Ibrahim Akilimali akitangaza kumfuta Uenyekiti wa timu hiyo, Lyod Nchunga, wakati wa mkutano wa wanachama unaoendelea muda huu kwenye klabu hiyo, Mtaa wa Jangwani/Twiga jijini Dar es Salaam.
Wanachama wa Yanga wakishangilia tamko la kumg'oa Mwenyekiti wa Klabu hiyo Lyod Nchunga
 Mashabiki wa Yanga ambao si wanachama, wakifuatilia mkutano wakiwa mbali
 Tofauti na vikao vingine vya Yanga ambavyo hufanyika katika ukumbi wa  jengo la Klabu hiyo, mkutano huu wa leo unafanyika kwenye Uwanja nje ya jengo.
 Mmoja wa wanachama wa Yanga, anayeitwa Nyachia akionyesha kadi yake wakati wa kujisajili kuingia kwenye mkutano huo. Picha kwa hisani ya Nkoromo Daily Blog


Dar es Salaam, Tanzania
WANACHAMA zaidi ya 600 wa Klabu ya Yanga ya jijini Dar es Salaam leo, wamehudhuria Mkutano wa dharura uliofanyika kwenye uwanja wa Kaunda unaomilikiwa na klabu hiyo walikubaliana kwa kauli moja kumng'oa madarakani aliyekuwa mwenyekiti wa klabu hiyo Lloyd Nchunga.

Kutokana na ukumbi wa mikutano wa klabu hiyo kuwa mdogo wanachama hao walilazimika  kufanyia mkutano wao kwenye uwanja wa Kaunda.
Mkutano huo ulianza majira ya saa sita mchana na kufunguliwa kwa Dua ya Kiislamu iliyosomwa na Ustadh Yasin na kufuatiwa na sala iliyoongozwa na mwanamama Ester Moshi, ambao wote kwa pamoja waliuombea mkutano huo ufanyike kwa amani.

Baada ya kusomwa kwa Dua na sala hiyo, mwenyekiti wa mkutano huo Bakili Makele, aliyepewa dhamana hiyo kutokana na mwenyekiti wa Baraza la wazee Alhaj Jabir Mohammed Kutundu kuwa mgonjwa na baada ya kuufungua alimkaribisha Katibu wa Baraza la wazee wa Yanga, Ibrahim Akilimali.

Akilimali alitumia maneno machache kuelezea udhaifu wa uongozi wa Nchunga na kuwa Baraza la wazee baada ya kuona mambo hayaendi sawa ndani ya uongozi, kukiwa na malalamiko mengi kutoka kwa wachezaji na benchi la ufundi kutolipwa mishshara na posho zao kwa nia nzuri walimshauri waichukue timu katika mkutano waliofanya baina yao na aliyekuwa mwenyeketi wa klabu hiyo Lloyd Nchunga Aprili 26, 2012.

"Ndugu zangu katika mkutano huo Nchunga aliridhia alituambia, wazee wangu kwa sababu ninyi mmesema mnaitaka timu mimi siwezi kuwakatalia lakini mnaonaje nikaenda kuwaeleza na wenzangu yaani wajumbe wa kamati ya utendaji kwa kuwa kesho tunao mkutano," alisema Akilimali.

Alisema kuwa walishangaa siku iliyofuata hakutokea klabuni kama walivyokubaliana ambapo wao walifika klabuni saa nne asubuhi kama makubaliano yao yalivyokuwa lakini hadi saa tano Nchunga hakutokea na baadaye wakaanza kusikia mingong'ono kwamba hawatapewa timu.

"Baadaye tukamsikia akizungumza na vyombo vya habari kwamba hawezi kutukabidhi timu na akatuita majina mabaya, akasema sisi tunakurupuka, sisi hatukutaka kubishana naye tukaamua kumuacha aseme atakavyo kwa kuwa mwisho wa siku kila kitu hujulikana kwa kuwa sisi hatukurupuki," alisema na kuongeza.

"Ninapenda kama mtaridhia kwa sababu yeye alitupa jina basi na sisi leo tunatoa jina tunampa jina kuanzi leo yeye tunamuita fisadi wa mali za Yanga na kwa ridhaa tunatamka kuanzia leo hii Nchunga sio mwenyekiti wa Yanga," alitamka Akilimali.

Alisema kuwa Nchunga alitaka kufanya mali za Yanga ziuzwe kwa sababu amedharau kulipa madeni makubwa anayodaiwa ambayo yametokana na uzembe na dharau zake kwenye mamlaka za soka baada ya kuvunja mikataba ya wachezaji Winsdom Ndlovu raia wa Malawi, Steven Marashi Mtanzania na George Njoroge raia wa Kenya na Shirikisho la soka la kimataifa (FIFA) kuamuru walipwe zaidi ya sh mil 120.

Aliongeza kuwa uongozi mbaya wa Nchunga ulisababisha kujiuzulu kwa wajumbe wanane wa Kamati ya utendaji wa kwanza akiwa makamu mwenyekiti Davis Mosha, akifuatiwa na wajumbe wa kamati ya utendaji, Seif Mohammed maarufu kama Seif Magari, Ally Mayay, Edgar Chibula, Mzee Yusuf, Pascal Kihanga, Mohammed Bhinda ambao pamoja na kifo cha Rutashoborwa kunaifanya kamati ya utendaji kutokidhi tena.

Mwingine aliyejiuzulu na ambaye wanachama walijulishwa kwamba alikuwa na mchango mkubwa ni mjumbe wa kamati ya usajili Abdallah bin Kleb, ambaye ndiye aliyemsajili kipenzi cha wana Yanga, Haruna Niyonzima ‘Fabregas’ wa Rwanda

Kwa mujibu wa Katiba ya Yanga ambayo inafuata ile ya Shirikisho la soka nchini (TFF) na lile la kimataifa (FIFA), iwapo theluthi ya wanachama watajiorodhesha na kutia saini zao, maamuzi yao ya kuomba Mkutano Mkuu yatakubaliwa na ndivyo walivyofanya Yanga, ambapo walisema watapeleka orodha hiyo kwa msajili wa vyama na klabu za michezo Wilaya ya Ilala ili kuomba uchaguzi Mkuu.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

HATUTOPAKI BASI DHIDI YA YANGA-MOKWENA

“PEMBA SALUTI KWENU” DK. NCHIMBI*

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA