AJIRA LUKUKI ZAMWAGWA JESHI LA POLISI

Waandishi Wetu
JESHI la Polisi litaajiri askari wapya 3,000 wengi wao wakiwa wasomi kutoka taasisi za elimu ya juu.

Akiwasilisha makadirio ya Bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2012/13 katika kikao cha Bunge, Dodoma jana, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi alisema:

“Sehemu ya waajiriwa itapatikana kutoka katika shule na vyuo vya elimu ya juu na idadi nyingine kutoka vijana wa JKT (Jeshi la Kujenga Taifa). Utaratibu huu unalenga kuwa na askari wenye sifa stahiki na waaminifu kwa kazi ya Polisi.”

Alisema polisi wataendelea kuongeza ufanisi katika upelelezi wa makosa ya jinai na kwamba mwaka 2012/2013 litatumia vyuo vyake vya Dar es Salaam na Kidatu kutoa mafunzo kwa askari wa kufanya kazi hiyo.

Dk Nchimbi alisema mafunzo hayo ya ukusanyaji na uchambuzi wa taarifa za kiintelijensia na mbinu za kisasa za upelelezi, zitatolewa kwa maofisa, wakaguzi na askari wapatao 1,000.

Wakimbizi kurejeshwa makwao
Waziri huyo alisema Serikali inakamilisha taratibu za kuwarejesha makwao wakimbizi wapatao 40,000, wengi wao kutoka Burundi, ifikapo mwishoni mwa mwaka huu.

Hadi kufikia Aprili 30, mwaka huu, Tanzania ilikuwa na wakimbizi 112,645 wakiwamo Warundi 48,195, Wakongo 62,632, Wasomali 1,548 na wakimbizi wa mataifa mengine 270.

Hatua ya kuwarejesha makwao wakimbizi itawezesha kufungwa kwa Kambi ya Mtabila, Kigoma yenye wakimbizi 38,800, ambayo inapaswa kuwa imefungwa ifikapo Desemba 31, mwaka huu.
“Katika mwaka 2011/12, idadi ya wakimbizi wa Burundi kutoka kambi hiyo waliorejea kwao ni 155 tu, hali iliyosababisha kambi hiyo kutofungwa,” alisema Dk Nchimbi na kuongeza:

“Mkakati mpya wa kufunga kambi hiyo ni kwamba limefanyika zoezi la mahojiano ya kina na wakimbizi hao kwa lengo la kubaini kama wapo wakimbizi wenye sababu za msingi za kuendelea kuwepo nchini.”
Alisema mahojiano hayo yalifanyika kati ya Septemba na Desemba mwaka jana na kwamba matokeo yanaonyesha kwamba 33,705 hawana sababu za msingi za kuendelea kuwa wakimbizi na wengine 2,045 walionekana kuwa na sababu za msingi.

Malumbano yaendelea
Malumbano yameendelea kulitikisa Bunge baada ya jana Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Utaratibu na Bunge), William Lukuvi kukatisha hotuba ya Waziri Kivuli wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Vicent Nyerere akidai inazungumzia mambo ambayo yako Mahakamani.

Nyerere alisoma bajeti yake baada ya ile iliyosomwa na Waziri Nchimbi lakini, wakati akiendelea, Lukuvi aliomba mwongozo wa Spika, Anne Makinda na kisha kuomba hotuba hiyo isitishwe.
Kitendo hicho kilisababisha mabishano ya kikanuni huku wabunge wakitunishiana misuli na kushindana kwa utaalamu wa kujua vifungu vya sheria na kanuni za Bunge.

Hii ni mara ya pili kwa Serikali kuzuia hotuba za wizara hiyo kutoka Kambi ya Upinzani. Mara ya kwanza ilikuwa katika hotuba ya Makadirio ya Mwaka jana (2011/12) ambapo aliyekuwa Waziri Kivuli wa Wizara hiyo, Godbless Lema alizuiwa kusoma hotuba yote.

Jana, baada ya Waziri Lukuvi kuwasilisha ombi lake, alisimama Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu ambaye alisema haikuwa haki kwa Serikali kukatisha hotuba hiyo kivuli na kwamba kitendo hicho kinakwenda kinyume cha utamaduni wa Bunge.

“Kama ambavyo Serikali imeachwa ikasoma hotuba yake yote, msemaji wa kambi ya upinzani Bungeni naye aachwe asome na aeleze kile ambacho ni maoni ya kambi, tangu kuanza kwa Bunge hili na mabunge yaliyopita, si utamaduni kukatisha hotuba ya upinzani,” alisema Lissu.

Lissu alisema wapinzani wamekuwa wakinyanyaswa na kwamba kuzuiwa kwa hotuba yao mara kadhaa, ni mbinu za kuwafanya wasieleze kwa Watanzania uovu unaofanywa na Serikali.

Baada ya hapo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema alisimama na kueleza kuwa anaunga mkono hoja ya Lukuvi kwa kuwa maelezo yaliyoko katika ukurasa wa nne wa hotuba ya upinzani yalitakiwa yakasemwe polisi.

“Mheshimiwa Spika, nasikitika kusema kwamba humu ndani ukurasa wa tatu kuna jambo ambalo jana (juzi) jioni ulitolea uamuzi kwa kutumia Kanuni ya 48 na nina imani kuwa waheshimiwa wabunge ambao wanajua hizi kanuni za kwenye vitabu watakubali kuwa hili jambo si la kujadili kwenye hotuba,” alisema Werema.

Alisema suala jingine ni la Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Peter Msigwa na kwamba liko mahakamani na hata suala la Dk Steven Ulimboka nalo liko mahakamani.
“Naunga mkono hoja ya Waziri wa Nchi kwamba maneno haya yasiingie naomba kutoa hoja,” alisema Werema, huku akisema kuwa Lissu ni mtovu wa nidhamu.

“Yaliyoko mahakamani nasema hapana na ninasisitiza yote yaliyoko mahakamani kweli hapana. Yaliyoko mahakamani hapana. Waheshimiwa wabunge naomba tuwe na heshima lakini yaliyoko mahakamani nasema hapana.” alisisitiza Jaji Werema.

Baadaye alisimama Spika Makinda na kusema yale yote ambayo yako mahakamani hatayaruhusu yajadiliwe hivyo yatolewe. Alitaka yatajwe ili yasijadiliwe... “Sijui ni yapi yako mahakamani kwa hiyo naomba mniambie ili niyajue.”

Lukuvi alisimama na kuyataja kuwa ni suala la Msigwa, Dk Ulimboka na lile lililojitokeza hivi karibuni huko Iramba Magharibi ambako mtu mmoja aliuawa katika vurugu zilizotokea kwenye mkutano wa hadhara wa Chadema.

Baadaye Mbunge wa Nyamagana (Chadema), Ezekiah Wenje alisimama na kusema pamoja na kuwa yeye si mwanasheria, kanuni zinasema hairuhusiwi kuzungumzia mwenendo wa mahakama hivyo, kinachozungumziwa ni maelezo ya kesi zilizopo mahakamani.

“Spika naomba uelewe na unisikilize kwa makini ili uelewe, sehemu ambazo Werema na Lukuvi wamezisoma wamezitafsiri kwa mitizamo yao, naweza kusema wako guided by narrow interpretation (wanaongozwa na tafsiri finyu),”alisema Wenje.

Malumbano hayo yalimsimamisha pia Mbunge wa Bariadi Mashariki (UDP), John Cheyo akitumia Kanuni ya 76(1) na (2) akitaka hoja hiyo isitishwe ili jambo hilo liangaliwe na kujua mambo yapi yako mahakamani.

“Spika mimi nadhani watu wanataka haki itendeke, ubishi uliopo hivi sasa unaweza ukaahirishwa na kwamba tukaahirisha hoja hii ili kuangalia ni mambo gani yaliyopo mahakamani,” alisema.
Hata hivyo, Makinda alisema mvutano haukuwa umefikia hatua ya kuahirisha Bunge na badala yake, aliitaka Kamati ya Maadili na Madaraka ya Bunge kukutana na kulitolea uamuzi jambo hilo kama maneno yaliyoandikwa na upinzani yako mahakamani basi hayatasomwa lakini, kama hayako mahakamani watarudia kuyasoma.

Ataka Waziri, Naibu waonje rumande

Katika hatua nyingine, Mbunge wa Ludewa (CCM), Deo Filikunjombe alipendekeza Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi na Naibu Wake, Pereira Ame Silima wawekwe rumande walau kwa miezi sita ili waonje adha ya hali mbaya katika mahabusu nchini.

“Bunge hili lipitishe uamuzi, waziri na naibu wake wakae jela hata miezi sita tu pengine wataweza kufahamu hali ilivyo mbaya katika mahabusu zetu. Hali ni mbaya kwelikweli na tunaposema tunamaanisha wala hatutanii,” alisema Filikunjombe.

Aliitaka Serikali kuongeza fedha zaidi ili kuliwezesha Jeshi la Polisi kununua silaha za kisasa: “Polisi hawana silaha zozote kuwawezesha kupambana na uhalifu na badala yake limeachiwa virungu ambavyo huvitumia kupigia wanafunzi, wakati wa migomo na maandamano ya Chadema,” alisema Filikunjombe.

Mbunge huyo alipendekeza kuwa ni bora jeshi hilo likasukwa upya na kupunguza ukubwa wake, ili kuliwezesha kuwa dogo lakini lenye silaha za kisasa zaidi kuliko kuwa na jeshi kubwa lenye silaha za kizamani.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA

DKT NCHIMBI ASHIRIKI MAZISHI YA ASKOFU.GACHUMA WA KANISA LA NLGCC

π™‚π˜Όπ™ˆπ™Šπ™‰π˜Ώπ™„ π™†π˜Όπ˜Ύπ™ƒπ™€π™•π˜Ό π™†π™„π˜½π™„π™‰π™‚π™’π˜Ό.