BONGE LA GAME YANGA NA APR TAIFA LEO


Kikosi cha Yanga; Kutoka kulia waliosimama Nadir Haroub 'Cannavaro', Kelvin Yondan, Yaw Berko ambaye leo anaweza kumpisha Barthez, Said bahanuzi, Athumani Iddi 'Chuji' na Oescar Joshua, wakati waliopiga magoti mbele kutoka kulia ni Hamisi Kiiza, Haruna Niyonzima, ambaye anaweza kumpisha Juma Seif 'Kijiko', Godfrey Taita, Stefano Mwasyika ambaye anaweza kumpisha Juma Abdul na Nizar Khalfan.
Na Prince Akbar
MABINGWA watetezi wa Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, Yanga SC leo wanashuka Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kumenyana na timu ya Jeshi la Rwanda, APR katika mchezo wa mwisho wa Kundi C kutafuta mpangilio wa nafasi ya kwanza, ya pili na ya tatu kwenye kundi hilo.
Yanga yenye pointi tatu, katika nafasi ya tatu, inaweza kumaliza mechi za kundi hilo katika nafasi ya pili, iwapo itashinda mechi ya leo, lakini sare au kufungwa itabaki katika nafasi hiyo hiyo.
APR yenye pointi nne, inaweza kupanda hadi nafasi ya kwanza kwenye kundi hilo na kuongoza kwa wastani wa mabao, iwapo itaifunga Yanga, kwani hadi sasa timu hiyo ya jeshi la Kagame, inalingana kwa wastani wa mabao (GD) na vinara wa kundi hilo, Atletico ya Burundi, saba kila timu.
Katika mchezo wa leo, Yanga iko hatarini kuwakosa nyota wake wawili, kipa wake namba moja, Mghana Yaw Berko, ambaye ni majeruhi sawa na kiungo wa zamani wa APR, Haruna Niyonzima, wakati kipa Ally Mustafa ‘Barthez’ yuko fiti kwa asilimia 100 sawa na beki Juma Abdul aliyeumia kwenye mechi ya kwanza dhidi ya Atletico, timu yake ikilambwa 2-0.   
Safu ya ushambuliaji ya APR inaweza kuongozwa na wakali wawili, Mrundi Suleiman Ndikumana na Olivier Karekezi ambao wote wana miili mikubwa ni hatari kweli sambamba na kiungo mshambuliaji, Mganda Danny Wagaluka, wakati Yanga bila shaka Said Bahanuzi na Hamisi Kiiza wataendelea kumpumzisha kwenye benchi Jerry Tegete na Nizar Khalfan ataongoza safu ya kiungo.
Kihistoria mechi kati ya Yanga na APR huwa ni kali na za kusisimua tangu zianze kukutana mwaka 1995 katika Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati na mara nyingi watoto wa Jangwani hunyanyaswa na timu hiyo ya jeshi la Rwanda. 
Mechi hiyo itatanguliwa na mchezo wa Kundi A, kati ya Ports ya Djibouti na URA ya Uganda.
JE WAJUA?
1.                      Klabu ya Armee Patriotique Rwandaise, maarufu kama A.P.R., ilianzishwa mwaka 1993 na inamilikiwa na Jeshi la Rwanda na katika kipindi cha uhai wake, mafanikio yake makubwa ni kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Rwanda mara 12 (1995, 1996, 1999, 2000, 2001, 2003, 2005, 2006, 2007, 2009, 2010 na 2011), Kombe la Kagame mara mbili (2004 na 2007) na kufika Nusu Fainali ya Kombe la Washindi mwaka 2003.
2.                      Young Africans SC maarufu kama Yanga iliyoanzishwa rasmi mwaka 1935, hadi sasa mafanikio yake makubwa ni kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Bara mara 23, (1968, 1969, 1970, 1971, 1972, 1974, 1981, 1983, 1985, 1987, 1989, 1991, 1992, 1993, 1996, 1997, 1998, 2002, 2005, 2006, 2008, 2009 na 2011), Kombe la Kagame mara nne (1975, 1993, 1999 na 2011), kufika Robo Fainali ya Klabu Bingwa Afrika mara tatu (1969, 1970 na 1998) na Kombe la Washindi 1996.
3.                      Wakati Yanga, kocha wake ni Mbelgiji Tom Saintfiet, APR inafundishwa na kocha Mholanzi, Ernie Brandts- na wakati Yanga Mwenyekiti wake ni mfanyabiashara milionea, Yussuf Manji, APR Mwenyekiti wake ni mdogo wa rais wa Rwanda, Paul Kagame aitwaye Alex Kagame.
4.                      Nembo ya Yanga ina alama ya Mwenge, ramani ya Afrika na mpira- ikimaanisha kushiriki harakati za Uhuru wa Tanganyika, ambayo baadaye iliungana na Zanzibar na kuwa Tanzania (Mwenge), timu halisi ya Afrika (ramani) na timu ya mpira (mpira), wakati nembo ya APR ina alama ya mnyama Simba na mpira- vikimaanisha, ni wafalme kama mnyama Simba porini (Simba) na timu ya mpira (mpira).  
5.                      Wakati Yanga huvalia jezi za rangi ya kijani na njano, APR wao huvalia jezi za rangi nyeupe na nyeusi siku zote, mara nyingi zikiwa za mistari ya punda milia.
6.                      Wakati wapinzani wa jadi wa Yanga, nchini Tanzania ni Simba SC kwa APR wapinzani wao wa jadi Rwanda ni Rayon Sport.. Kwa hisani ya Bin Zubeiry Blog

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

KOCHA BENCHIKHA AMESEPA

MASHUSHUSHU WA MAMELODI WALIKUJA KUTUPELELEZA: HERSI