CUF yataka Tume Huru kwanza kabla ya Katiba mpya

Mwenyekti wa CUF, Profesa Lipumba akizungumza leo
Na mwandishi wetu,
Dar es Salaam

CHAMA cha Wananchi (CUF), kimeamua kuvunja ukimya baada ya kuamua kuzungumzia mambo muhimu yaliyopo mbele ya Watanzania huku kikitumia nafasi hiyo kudai kwa nguvu zote Tume Huru ya Uchaguzi kabla ya kufikiwa kwa Katiba mpya.
Pia kimesema muda ambao umetolewa na Serikali katika mchakato wa kupata Katiba mpya ni mdogo na wao wanachoona kuna kila dalili ya kutopatikana katiba itakayokidhi mahitaji ya wananchi kutokana na kutokuwa na muda wa kutosha wa kuiandaa.
Akizungumza Dar es Salaam leo, wakati akifungua mkutano wa Baraza Kuu la Uongozi wa Chama hicho, Mwenyekiti Profesa Ibrahim Lipumba, alisema kuwa kuna mambo mengi ambayo Serikali inatakiwa kuwa makini katika kuhakikisha yanafanyika kwa wakati na kubwa ambalo wao wanaona ni bora zaidi ni kupatikana kwa tume huru ya uchaguzi kwanza, ambayo itatenda haki kwa vyama vyote vya siasa.
Prof. Lipumba aliyekuwa akifungua mkutano wa baraza hilo, lililofanyika Makao Makuu ya CUF, Buguruni, alisema kuwa sasa ni wakati wa kutafakari zaidi mambo kwa mapana na umuhimu wake na CUF inaona ni wakati mwafaka wa kuwa na tume huru ya uchaguzi.
"Msimamo wa CUF tunahitaji tume huru ya uchaguzi kabla ya uchaguzi mkuu ujao, hii itasaidia katika kuhakikisha mambo mengi yanayolalamikiwa sasa kuondoka. Itakuwa ni muhimu zaidi kwa tume hiyo kutenda haki hasa katika suala zima la uchaguzi tofauti na sasa tume iliyopo imeshindwa kuwasaidia wanasiasa katika kutafuta haki kwa kila chama," alisema.
Kuhusu Katiba mpya alisema hakuna sababu ya kufanya mchakato wa kuipata kwa haraka kiasi hicho kama ambavyo Serikali imetoa muda kwani ni mdogo na hautoshi kuandaa kitu ambacho kitakuwa mwongozo wa maisha ya Watanzania kwa miaka mingi ijayo.
Alifafanua zaidi kuwa katika mambo ambayo Serikali haipaswi kulipua ni pamoja na upatikanaji wa katiba mpya na ndiyo maana CUF inaona haja ya kuwa na muda wa kutosha kuiandaa tofauti na uamuzi wa Serikali ambao unataka hadi Aprili mwaka 2014 iwe imekamilika.
"Katiba ya nchi inahitaji muda wa kutosha kuiandaa si jambo la kufanya kwa papara kwani mwisho wa siku itakuwa tatizo kubwa ambalo limefanywa aidha kwa kujua ama kutojua. Ushauri wa CUF tunahitaji muda wa kutosha wa kuiandaa Katiba," alisema Prof. Lipumba.
Akizungumzia mgomo wa madaktari, Prof. Lipumba alisema kuwa kwa mujibu wa sheria za nchi kuna taasisi muhimu ambazo hazitakiwi kufanya mgomo na kutolea mfano polisi, zimamoto, na madaktari na kwamba kutokana na umuhimu huo Serikali inatakiwa kuwa makini katika kuhakikisha taasisi hizo hazigomi kwa kuwa karibu nao na kusikiliza mahitaji yao.
"Katika hili la mgomo wa madaktari bado kwa upande wetu tunaona iko haja kwa Serikali kutafuta suluhu ili kuhakikisha malalamiko katika sekta hiyo muhimu yanapungua tofauti na sasa," alisema Prof. Lipumba.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

KOCHA BENCHIKHA AMESEPA

MASHUSHUSHU WA MAMELODI WALIKUJA KUTUPELELEZA: HERSI