Dk Slaa amvimbia Waziri Nchimbi

KATIBU Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa amesema hawezi kujipeleka polisi kuhojiwa kutokana na kauli yake kwamba yeye na viongozi wengine wawili wa chama hicho wanatishiwa kuuawa na kigogo mmoja wa Idara ya Usalama wa Taifa, huku akieleza sababu mbili za kugomea wito huo wa Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Emmanuel Nchimbi.Juzi, Dk Nchimbi aliliagiza Jeshi la Polisi kuwahoji viongozi wote wa Chadema waliotoa tuhuma za kutaka kuuawa hata kama wao hawana imani na jeshi hilo.

Akizungumzia na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Dk Slaa alisema yeye na wenzake, Mbunge wa Ubunge, John Mnyika na Mjumbe wa Kamati Kuu, Godbless Lema hawatakwenda polisi kuhojiwa na jeshi hilo likitaka liwakamate.

Alilishauri jeshi hilo kutumia njia zake za kiitelijensia kujua ukweli wa mambo badala ya kufikiri kwamba wanaweza kupata maelezo kuhusu suala hilo kutoka kwake au viongozi wengine wa chama hicho.
“Leo (jana) asubuhi Ofisa wa Makao Makuu ya Polisi amenipigia simu kuomba appointment (miadi) lakini nasema sina muda. Sisi hatuendi (polisi) kwa sababu walishatudanganya mara nyingi tu.

Kama wanataka watukamate. Wao wana wapelelezi na usalama wachunguze,” alisema Dk Slaa na kuongeza:
“Kwani wao wanavyotukataza kufanya mikutano wakisema wana taarifa za kiitelijensia, huwa tunawauliza ni nani kawaambia? Na wao wachunguze kwa vyombo vyao kwa sababu ni jukumu lao kulinda usalama wa wananchi .”

Sababu za kutoamini polisi

Dk Slaa alisema sababu ya kutokuwa na imani na polisi ni pamoja na kutomweleza mpaka leo, vilipo vinasa sauti walivyovichukua katika hoteli aliyokuwa akiishi mjini Dodoma... “Walivichukua vile vinasa sauti na hawakutuambia ni nini kilichokuwa ndani, wangetupa tupeleke kwa wataalamu tukavichunguze.”

Alisema sababu nyingine ni tukio la kupigwa kwa wabunge wa chama chake mkoani Mwanza, akidai kwamba licha ya polisi kupewa taarifa mapema, hawakuchukua hatua yoyote.

Kutokana na hayo, alisema haoni sababu ya kuhojiwa na polisi kwani viongozi wa chama hicho kwa muda mrefu wamekuwa wakieleza mambo mbalimbali yanayotishia usalama wa wananchi na nchi, lakini jeshi hilo limeshindwa kuyafanyia kazi.

“Sasa kama wameshindwa hayo sasa wanataka kutuhoji kwa lipi? Hatuendi sisi tumeshawaeleza kinachoendelea kazi ni kwao,” alisema Dk Slaa.
Alisema taarifa walizozipata juzi ni kwamba maofisa wa jeshi hilo walikaa kikao muda mfupi baada ya kusikia tuhuma zilizotolewa na chama hicho na kuongeza kwamba wanachokisubiri hivi sasa ni kukamatwa.

Alidai kuwa jeshi hilo linaendelea kufanya makosa huku likitambua wazi kuwa maisha ya Watanzania yapo hatarini.

“Ndiyo maana, madaktari wameomba Umoja wa Mataifa (UN), kumwekea ulinzi Dk Steven Ulimboka katika hospitali aliyolazwa, hii yote ni ishara kwamba hali si shwari,” alisema Dk Slaa.
Alisema kazi ya polisi ni kutekeleza wajibu wao mara baada ya wananchi kutoa taarifa zinazohitaji kufanyiwa uchunguzi.

“Chadema ni chama makini, tunajua kuwa polisi walifanya kikao, wanatakiwa kujua kuwa nyumba yao inavuja… sasa kama nyumba yao inavuja sisi hatuoni haja ya kwenda kuhojiwa. Tunamuomba Mungu na tunajua atatulinda na wao acha waendelee kufanya vikao vyao.”

Operesheni Sangara kuendelea

Katika hatua nyingine, Chama hicho kimeanza sehemu ya pili ya Operesheni Sangara baada ya kufanya hivyo katika Mikoa ya Morogoro, Iringa, Singida, Dodoma na Manyara.

Dk Slaa alisema jana kwamba katika operesheni hiyo inayotarajiwa kuanza wiki ijayo, watapita katika majimbo 44, kata 406 na vijiji 4,000.
Alisema katika operesheni hiyo, watawatumia wabunge wao, viongozi wa halmashauri kuu na makada wake wengine.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

HATUTOPAKI BASI DHIDI YA YANGA-MOKWENA

“PEMBA SALUTI KWENU” DK. NCHIMBI*

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA