Skip to main content

“FURSA YENYE TIJA: TAFAKURI YA UTUMISHI WANGU KAMA NAIBU KATIBU MKUU WA UMOJA WA MATAIFA”- DR. ASHA-ROSE MIGIRO.


Hakika kila chenye mwanzo hakikosi mwisho, na kila mwisho wa jambo moja huwa mwanzo wa jingine. Ingawa huenda ni mapemasanakwangu kutoa tafakuri kamili ya muhula wangu katika nafasi ya Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, hapana shaka kabisa kuwa nafasi hiyo imenipa uzoefu maridhawa. Namshukuru Katibu Mkuu BAN Ki-moon kwa  kunipa fursa hii, kuniamini na kwa ushirikiano mkubwa wakati wote wa utumishi wangu.
Kukitumikia chombo hiki cha kimataifa kwa muda wa miaka mitano na nusu mfululizo ni heshima ya pekee ambayo daima nitaienzi  kama kilele kimojawapo  cha maisha yangu ya utumishi  wa umma.  Kila siku niliyoitumia katika Umoja huo ilikuwa ni darasa la kusukuma mbele mipaka ya ujuzi na elimu.  Nimepata kufahamu mengi zaidi kuhusu Shirika lenyewe; kuhusu dunia na watu wake, lakini pia kufahamu ukomo wa uwezo wa Umoja wa Mataifa katika kushughulikia changamoto mbali mbali zinazoikabili dunia yetu.
Utumishi wangu katika Umoja wa mataifa ulikuwa fursa adhimu iliyonipa uzoefu wa pekee. Kazi hii imeujaza moyo wangu na unyenyekevu wa dhati kwani niliingia Umoja wa Mataifa wakati ambapo  dunia inachagizwa  na  madhila  makubwa makubwa yakiwemo maradhi, umaskini wa kupindukia,  kutokuwapo kwa usawa wa kijinsia,  kuongezeka kwa vitendo vya ukatili na udhalilishaji kwa wanawake na watoto;  na changamoto nyingine nyingi. Kwa muktadha huu ilikuwa fursa ya pekee kuchangia juhudi za pamoja za kuimarisha Umoja wa Mataifa katika kutekeleza majukumu yake katika kipindi cha mazingira magumu  ya kimataifa yaliyojaa changamoto za kipekee kabisa. 
Daima nitaendelea kushukuru na kuthamini kwa dhati jinsi Mhe. Rais Jakaya Mrisho Kikwete, Serikali na Watanzania wenzangu walivyonitia moyo na kunienzi katika kipindi chote nilichokuwa Umoja wa Mataifa. Familia yangu, ndugu na marafiki walikuwa karibu nami kwa dua na kunitia nguvu wakati wote wa utumishi wangu.  Nawashukuru sana.
Hapana shaka  kazi yangu katika Umoja wa Mataifa imeniwezesha  kufahamiana kwa karibu na viongozi wengi wa kimataifa na pia  watu mbali mbali  waliopata mafanikio makubwa duniani.  Nimeweza kufahamu kwa undani thamani ya michango yao katika kujenga amani na ustawi wa dunia.
Zaidi ya yote, sitasahau hisia nilizopata kila nilipokutana na watu wanyonge waliokuwa wanahitaji msaada wa Umoja wa Mataifa.  Nitakumbuka daima tabasamu ya mwanamke mmoja niliyekutana naye katika moja ya ziara zangu barani Afrika nilipotembelea zahanati mojawapo kati ya kadhaa zinazofadhiliwa na Umoja wa Mataifa.  Mama huyo mwenye watoto sita, alikuwa amekikumbatia kitoto chake kimoja kilichokuwa nyonde nyonde; lakini alikuwa na tabasamu iliyojaa faraja na matumaini kwa kuwa alikuwa amefanikiwa kupata bure dawa za kunusuru maisha ya mwanawe.
Maendeleo
Nafasi ya Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa iliasisiwa na  Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa  mwaka 1997 kwa madhumuni ya kuongeza ufanisi wa utendaji wa Sekretariati na kuimarisha  uongozi wa Umoja Mataifa katika medani za uchumi na maendeleo ya jamii.  Majukumu ya Naibu Katibu Mkuu yaliongezeka kadri Shirika lilivyokuwa linapanua shughuli zake. Hatimaye Naibu Katibu Mkuu akakabidhiwa jukumu la kuoanisha na kuratibu idara zote zilizo chini ya mwavuli wa Umoja wa Mataifa. Jukumu hili lilikuwa na manufaa makubwa, hususan tulipoingia katika utekelezaji wa dhana ya “Huduma ya Pamoja ” (Delivering as One – DaO) ili kuleta ufanisi zaidi  katika kazi zetu hususan za maendeleo.
Kwa bahati nzuri, ninamaliza kipindi changu kukiwa na maendeleo mazuri yanayotokana na jitihada za kimataifa za kupambana na umaskini. Takwimu za kuaminika za hivi karibuni zinatuambia kuwa juhudi zetu za kupunguza idadi ya watu maskini duniani kufikia angalau nusu ya viwango vya sasa zimeanza kuzaa matunda. Taarifa hii ni ya kutia moyo licha ya ukweli kwamba dunia inapitia dhahama kubwa ya kiuchumi kuliko wakati mwingine wowote katika miaka ya hivi karibuni. Pamoja na majukumu mengine,nguvu zetu tulizielekeza zaidi kwenye kufanikisha malengo ya maendeleo ya milenia na malengo mengine ya maendeleo yaliyokubaliwa kimataifa. Nilihamasika sana na dhamira waliyoionesha wadau na washirika wetu wa maendeleo: serikali, mashirika ya kiraia na mashirika ya biashara. Kwani wote kwa pamoja waliyatumia malengo hayokamakilingo cha msingi katika kutokomeza umaskini.
Katika kufanikisha utekelezaji madhubuti wa malengo ya maendeleo ya milenia nilipewa jukumu la kukamilisha ahadi ya Katibu Mkuu aliyoitoa kwa nchi wanachama ya kuunda Mfumo Kamilifu wa Utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDGs Integrated Implementation Framework ). Ninaona fahari kwamba naondoka Umoja wa Mataifa mfumo huu ukiwa umekamilika ambapo Katibu Mkuu aliuzindua mwezi Juni mwaka huu. Kwa mara ya kwanza mfumo huu umeweka utaratibu ambao utauwezesha Umoja wa Mataifa na wadau wote kufuatilia mwenendo wa utekelezaji wa ahadi za kisera na kifedha.  Hapana shaka utaratibu huu utaongeza uwajibikaji wa wadau na upimaji sahihi wa hatua za maendeleo.
Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDGs) Barani Afrika
Kwa mwelekeo huo huo,  Katibu Mkuu alizindua Jopo la Viongozi la Kuhimiza Utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya Milenia Barani Afrika (MDG Africa Steering Group) mwezi September 2007. Kikundi hiki kinajumuisha taasisi zote kuu duniani zilizo mstari wa mbele katika kuchochea kasi ya maendeleo ya Afrika.  Nilipata bahati ya kukiongoza kikosi-kazi (MDG Africa Working Group) kilichokuwa mhimili wa Jopo hilo la viongozi. Baada ya  miaka mitano ya majadiliano ya kina, Jopo hilo likiongozwa na Katibu Mkuu limetoa mapendekezo kamambe  ya utekelezaji. Endapo mapendekezo haya yatazingatiwa  basi yatakuwa nyenzo muhimu ya kuweka sera na mikakati madhubuti itakayosaidia maendeleo katika nchi husika na duniani kwa ujumla. Napenda kutoa mwito kwa wadau wote kuyapa umuhimu mapendekezo haya.
Ninafahamu kwamba tathmini kamili ya mafanikio ya utekelezaji  wa Malengo ya Maendeleo ya Milenia imepangwa kufanyika Septemba  mwaka 2013.  Hata hivyo tayari tunaweza kusema kuwa Malengo haya yameleta mabadiliko chanya katika maisha ya watu wa kawaida  sehemu nyingi duniani, hususan barani Afrika. Ni dhahiri kuwa jamii  nyingi zimenufaika na utekelezaji wa malengo ya maendeleo ya milenia sio kwa kufanyiwa hisani bali kwa wao wenyewe kuwa na mikakati maalum ya kupiga hatua madhubuti za kujiletea maendeleo stahimilivu na yaliyolenga kuleta usawa baina ya watu.
Mkutano wa Rio + 20
Ni jambo la kutia moyo kwamba maendeleo shirikishi na yenye kuleta usawa ni baadhi ya masuala muhimu yaliyojadiliwa katika mkutano wa Rio +20 uliomalizika hivi karibuni. Suala hili litachukua nafasi kubwa pia katika kuandaa mfumo wa maendeleo unaotarajiwa  baada ya mwaka 2015,  mwaka uliokusudiwa kufikia malengo ya maendeleo ya milenia.  Nilipokabidhiwa jukumu la kuratibu maandilizi ya ushiriki wetu kwenye mkutano wa Rio+20 nilitiwa moyo na nia ya dhati ya mashirika ya Umoja wa Mataifa ya kubuni mkakati wa pamoja wa kutekeleza maazimio ya Rio+20. Napenda kuzishukuru nchi wanachama kwa kufikia makubaliano katika masuala mengi yaliyojadiliwa Rio licha ya changamoto nyingi zinazotokana na mtikisiko wa uchumi duniani. Ninafurahi kwamba maazimio ya mkutano huu yatachangia upatikanaji wa maendeleo stahimilivu, shirikishi na yenye kuleta usawa na hususan kuhakikisha kunakuwa na mustakabali mzuri kwa wanawake na wasichana.
Uwezeshaji wa wanawake na usawa wa kijinsia
Tukirejea kwenye suala hili, hata baada ya Mkutano wa Rio + 20 tutawajibika kuendelea na juhudi za uwezeshaji wa wanawake na kuleta usawa wa kijinsia.  Wakati wa utumishi wangu Umoja wa Mataifa tumefanya bidii kubwa na kutumia muda mwingi kushughulikia suala hii. Tumetumia hadhi na ushawishi wa ofisi yetu kupaza sauti za wanawake na wasichana na kukuza ushiriki wao katika jamii. Tumeendesha kampeni za kupiga vita ukatili kwa wanawake na wasichana.  Tumezihimiza mamlaka katika ngazi za kitaifa na kimataifa kutunga sera na sheria zinazozingatia haki za wanawake na usawa wa kijinsia, na tumetaka wapewe fursa kushika nafasi za uongozi katika jamii.  Ndiyo maana kwa upande wetu hatukuweka koleo chini hadi pale tulipokamilisha uanzishwaji wa idara inayojulikana kwa kifupi kama “UN Women” mnamo Julai 2010. Hii ni idara ya Umoja wa Mataifa  iliyoundwa kwa madhumuni ya kuongoza masuala ya wanawake na usawa wa kijinsia kwa umakini na ufanisi zaidi kuliko hapo awali. Tumefanya jitihada hizi kwa kuamini kuwa hakuna uamuzi wowote ule, uwe mdogo au mkubwa, unaofanywa na Umoja wa Mataifa bila ya kuzingatia maendeleo na ustawi wa wanawake na wasichana.
Huduma ya Pamoja
Kwa upande mwingine ninapenda kuwapongeza kwa dhati wenzangu wote waliomo katika utumishi wa Umoja wa Mataifa,wake kwa waume,walioutumia ujuzi na weledi wao wote kuchangia maendeleo ya nchi na jamii tunazozihudumia. Natoa shukrani za pekee kwa wale wote waliopo kwenye ofisi na vituo vya Umoja wa Mataifa nje ya Makao Makuu na ambao wanafanya kazi katika mazingira magumu na yenye changamo nyingi. Hao wote wanadhihirisha umuhimu wa kuwapo kwa Shirika hili kama chombo cha kuhimiza maendeleo katika ngazi zote za kitaifa, kikanda  na kimataifa. Katika kutekeleza dhana ya “Huduma ya Pamoja” (Delivering as One) Waratibu Wakaazi wa Umoja wa Mataifa wamekuwa na mchango muhimu sana.Uratibu wao umeongeza ubora na wepesi wa utoaji huduma kwa nchi wanamowakilisha Shirika. Hatuna budi kuwashukuru kwa mchango wao mkubwa katika kufanikisha dhana ya “Huduma ya Pamoja”.  Ni dhahiri kwamba  uwezo wa nchi mwanachama kumiliki mchakato wa maendeleo yake unakuwa  imara zaidi  pale ambapo kuna mtiririko mzuri wa huduma za Umoja wa Mataifa na fursa za kukuza ushirikiano endelevu na wadau wengine wa maendeleo.  Wakati uamuzi rasmi kuhusu maendeleo ya dhana hii ukisubiri kukamilika kwa majadiliano ya nchi wanachama, ninaamini kwa dhati kuwa utaratibu wa kutoa  “Huduma ya Pamoja” kupitia mpango mmoja uliokubaliwa na wote ni mwelekeo sahihi na wenye tija.
Nchini mwetu Tanzania, mashirika ya Umoja wa Mataifa yamekuwa yakifanya kazi kwa ushirikiano wa karibu sana toka mwaka 2011 kupitia mpango mmoja uitwao “Mpango wa Umoja wa Mataifa wa Kusaidia Maendeleo” (United Nations Development Plan – UNDAP). Mpango huu unakwenda sambamba na mwaka wa fedha wa Serikali yaani Julai 1 hadi Juni 30 na kwa mantiki hiyo kuuwezesha kuzingatia vipaumbele vya Serikali. Kupitia mpango huu Umoja wa Mataifa umejiwekea utaratibu wa kujipima na kujitathmini ambao unatoa fursa kwa hatua za haraka kuchukuliwa inapobidi. Utaratibu huu unapatikana kwenye tovuti. Kwa upande wa uendeshaji, mfumo huu wa utendaji kazi kwa pamoja umetuwezesha kutekeleza majukumu mengi kwa kutumia raslimali chache ambapo“ziada” iliyopatikana imeelekezwa kwenye shughuli nyingine za maendeleo.
Afya ya Jamii

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

KOCHA BENCHIKHA AMESEPA

MASHUSHUSHU WA MAMELODI WALIKUJA KUTUPELELEZA: HERSI