Kamati ya Zitto yaingilia kati kusimamishwa bosi wa Tanesco

Mwenyekiti wa POAC, Zitto Kabwe
 SIKU moja baada ya Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), kumsimamisha  kazi  Mkurugenzi Mkuu Mtendaji wa Shirika  hilo, Mhandisi William Mhando, Kamati  ya Bunge ya Mashirika ya Umma (POAC), imeitisha kikao cha dharura kujadili uamuzi huo.
Juzi, Bodi hiyo chini ya Uenyekiti wa Mkuu wa Majeshi Mstaafu Jenerali Robert Mboma, iliwasimamisha kazi, Mhando na viongozi wengine wa Tanesco ambao ni Naibu Mkurugenzi Mtendaji Huduma za Shirika, Robert Shemhilu, Ofisa Mkuu wa Fedha, Lusekelo Kassanga na Meneja Mwandamizi, Ununuzi Harun Mattambo.
Akizungumza na gazeti hili jana, Mwenyekiti wa Kamati Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), Zitto Kabwe alisema kufuatia uamuzi huo wa Bodi ya Tanesco, ameomba ruhusa kwa Spika wa Bunge, Anne Mkinda kuitisha kikao cha dharura na bodi hiyo ijieleze.  Zitto alisema kuwa, mbali na bodi hiyo wamemwita Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA).
“Siku ya Jumatano (kesho kutwa) kamati imemwomba Spika ruhusa ya kuitisha kikao ili bodi nzima ya Tenesco kuja kutupa maelezo ya nini kimetokea, maana taarifa ya CAG na PPRA haina hizo tuhuma wanazosema watu wa Serikali,” alisema Zitto na kuongeza:
“POAC tunahusika na usimamizi wa fedha za shirika, tunataka kujua ubadhirifu na masuala ya kisheria na  itahakikisha uwajibikaji na tutasimamia hilo kwa nguvu zote kwani  hatutaki uonevu na tutalinda wanaoonewa.  Hata hivyo, kauli hiyo ya Zitto inakuja wakati baadhi ya wabunge akiwamo yeye mwenyewe hivi karibuni walishinikiza mawaziri ambao wizara zao zilitajwa kuhusika na tuhuma za ufisadi katika ripoti ya CAG wajiuzulu.

Mhandisi William Mhando
Zitto pia ndiye aliyeongoza zoezi la kukusanya saini za wabunge kwa ajili ya kupiga kura za kutokuwa na imani na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda baada ya ripoti ya CAG kuonyesha ufisadi mkubwa serikalini.  Akisoma ripoti ya POAC baada ya kutolewa ripoti na CAG, Zitto alisema kuwa, Tanesco kulikuwa na ongezeko la gharama za ununuzi kutoka Sh300 bilioni za mwaka juzi hadi Sh600 bilioni katika ripoti ya mwaka huu na kuhoji, chanzo cha ongezeko la gharama hizo kwa asilimia 100.
Hata hivyo, taarifa za ndani kutoka Wizara ya Nishati na Madini zinaeleza kuwa uamuzi wa bodi hiyo kumng'oa Mhando na wenzake unatokana na kushindwa kuwajibika kwa Mkurugenzi huyo kumaliza mgawo wa umeme na kuendelea kuwapo kwa vitendo vya hujuma katika uzalishaji wa umeme.
Kauli ya Utouh
Hata hivyo, akizungumzia suala hilo Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh alisema hana taarifa zozote za kuitwa na Kamati ya POAC kuhusiana na sakata la kusimamishwa viongozi wa Tanesco.
“Sijapata taarifa za kuitwa na Kamati ya Bunge ya Mashirika ya Umma, wewe ndiyo unanijulisha kuhusu hilo.”
Utouh alisema kwa sasa hawezi kuzungumza kuhusu ripoti ya hesabu za Tanesco kama walipata hati safi au hati chafu hadi aipitie upya ripoti hiyo.
“Kwa harakaharaka siwezi kufahamu kama Tanesco walipata ripoti ya aina gani inayohusu matumizi ya fedha hadi niisome upya ndipo ninaweza kulizungumzia,” alisema Utouh.
CAG alisema taarifa za kusimamishwa viongozi wa Tanesco ameziona na kuzisoma katika vyombo vya habari.
Mwambalaswa Mmoja wa Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi, Victor Mwambalaswa alitaja baadhi ya tuhuma zilizosababisha bodi hiyo kumsimamisha Mhando pamoja na maofisa wenzake kuwa ni kuhusika katika matumizi mabaya ya fedha za umma.
Mwambalaswa ambaye pia ni Mbunge wa Lupa (CCM), alizitaja tuhuma nyingine  kuwa, ni matumizi mabaya ya madaraka likiwamo la kuongoza kwa upendeleo.
Alidai upandishwaji vyeo unafanywa kwa misingi ya ukabila.
“Msingi wa tuhumu hizo ni ziara aliyofanya Waziri wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa Sospter Muhungo  hivi karibu ambapo aliwataka wafanyakazi wenye kero kuwasilisha malalamiko yake wizarani ili yafanyiwa kazi,” alibainisha Mwambalaswa.
Pia, uamuzi wa kutaka watendaji nao wawajibike ulitangazwa na Rais Jakaya Kikwete Ikulu Mei 4, wakati akitangaza baraza jipya la mawaziri ambapo alisema kuwa, mbali ya uwajibikaji kisiasa, bodi za wakurugenzi na watendaji ambao taasisi zao zimetajwa katika ripoti ya CAG kuhusika na matumizi mabaya ya fedha za umma, watapaswa kuwajibishwa.   
Ilivyokuwa  Hatua hiyo ilitangazwa juzi jijini Dar es Salaam kufuatia  kikao cha dharura cha Bodi ya Wakurugenzi ya Tanesco kilichofanyika  Julai 13 mwaka huu, ambacho kilijadili tuhuma mbalimbali dhidi ya menejimenti ya Tanesco.  Kikao hicho kiliongozwa na Mwenyekiti wake, Jenerali Mstaafu Robert Mboma  na kuchukua uamuzi wa kumsimamisha kazi Mhando ili kupisha uchunguzi wa tuhuma za ubadhirifu na matumizi mabaya ya madaraka. 
“Hivyo, bodi iliazimia pamoja na mambo mengine kama ifuatavyo: Uchunguzi wa tuhuma hizo uanze mara moja kwa kutumia uchunguzi huru na kumsimamisha kazi Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Mhandisi William Mhando ili kupisha uchunguzi huo na kwa kuzingatia matakwa ya sheria za kazi nchini,” ilieleza sehemu ya taarifa aliyoitoa  Mboma kwa vyombo vya habari.  Mhando aliteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Tanesco kuanzia Juni Mosi Mwaka 2010. 
Baada ya uteuzi huo, Mhando alisema atahakikisha wateja wote wa Tanesco wanakuwa na mita za Luku.  Kabla ya uteuzi huo, Mhando alikuwa ni Meneja Mkuu Usambazaji Umeme na Masoko katika shirika hilo.  Mhando alichukua nafasi ya aliyekuwa Mkurugenzi wa shirika hilo, Dk Idris Rashid ambaye alimaliza muda wake wa uongozi.
Chanzo: Mwananchi Julai 16. 2012

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

HATUTOPAKI BASI DHIDI YA YANGA-MOKWENA

“PEMBA SALUTI KWENU” DK. NCHIMBI*

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA