KIVUMBI YANGA, APR LEO

MABINGWA watetezi wa Kombe la Kagame, Yanga na Azam FC, leo zinaweza kuandika tena historia ya timu za Tanzania kukutana kwenye fainali ya michuano hiyo kama ilivyokuwa mwaka jana, lakini hilo likiwezekana tu endapo zitashinda mechi zao ngumu za hatua ya nusu fainali leo kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Mwaka jana Yanga ilitwaa ubingwa wa michuano hiyo inayoandaliwa na Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) baada ya kuwafunga bao 1-0 wapinzani wao wakubwa katika soka la Tanzania, Simba.

Hali hiyo inaweza kujirudia tena mwaka huu, endapo Yanga wataifunga timu ngumu ya APR ya Rwanda katika nusu fainali ya pili, baada ya ile ya kwanza itakayoikutanisha Azam na Vita Club ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Kufikia hatua hiyo, mabingwa watetezi Yanga, waliwatoa wenzao wa Zanzibar timu ya Mafunzo kwa mikwaju ya penalti 5-3 katika robo fainali iliyomalizika kwa sare ya bao 1-1 baada ya dakika 90.

Azam, ikicheza kwa mara ya kwanza Kombe la Kagame, ilisonga mbele baada kuitia aibu ya kipigo cha mabao 3-1, mabingwa wa mara sita michuano hiyo, Simba katika mchezo uliochezwa Jumanne wiki hii.

Mechi zote zinatarajia kuwa ngumu kutokana na hatua iliyofikiwa, lakini bila shaka taswira ya ushindani itakayoliteka jiji la Dar es Salaam, itakuwa mchezo wa Yanga na APR.

Ushindani huo unategemewa katika dhana mbili, kwanza ubora wa timu hizo zinazoundwa na wachezaji wenye viwango vinavyolingana, na pili ni kisasi cha mchezo wa kwanza hatua ya makundi, ambapo Jangwani walitikisha kamba za APR mara mbili bila majibu.

Kiufundi, Yanga italazimika kubadili mbinu ilizozitumia katika mechi yao ya kwanza dhidi ya APR ambayo haitakuwa tayari kuruhusu kipigo cha pili mfululizo ndani ya siku tatu.

Mabingwa Yanga, itawategemea washambuliaji wake Saidi Bahanuzi na Hamis Kiiza katika kuzivuruga kamba za APR, ambao nao watakuwa na Leonel Preus na Seleman Ndikumana kuiandama ngome ya Yanga.

Pia ushindani mkubwa unatarajiwa kuwepo katika idara ya kiungo, ambako Haruna Niyonzima na Athuman Iddi wanakuwa wakionyesha manjonjo yao kama ilivyo kwa Jean Claude Iranzi na Jean Claude Mugiraneza wanaosubiriwa kung'aa kwa upande wa Wanyarwanda .

Hakuna shaka, beki kisiki Mbuyu Twite ataongoza jopo la ulinzi wa APR akisaidiwa na Jonson Bagoole kama itakavyokuwa kwa Nabir Haroub atatengeneza ngtome ya Yanga akisaidiana na Kelvin Yondan.

Kwa upande wa Azam ambayo haijapoteza mchezo kwenye michuano hii, itashuka dimbani ikiwa maazimio ya kutaka kuweka rekodi ya kushiriki mara kwanza na kutwaa taji.

Aina ya soka lao lenye pasi nyingi linaloshabihiana na wapinzani wao AS Vital, pamoja na kujivunia wachezaji waliokaa pamoja kwa muda mrefu kunaufanya mchezo wa leo kuwa mgumu.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

KOCHA BENCHIKHA AMESEPA

MASHUSHUSHU WA MAMELODI WALIKUJA KUTUPELELEZA: HERSI