MAJAMBAZI YATIKISA DAR


MTAA wa Shingofeni uliopo Ilala Sharrif Shamba, Dar es Salaam jana uligeuka uwanja wa mapambano ya risasi za moto baina ya polisi na watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi wanadaiwa kuwa waikusudia kupora katika nyumbani ya mfanyabiashara mmoja anayeishi katika eneo hilo.

Wakati tukio hilo likitikisa jiji la Dares Salaam ambalo ni kitovu kikuu cha Ulinzi na Usalama, tukio jingine limetokea Wilayani Misungwi, Mkoani Mwanza ambako majambazi walivamia vijiji viwili na kuviteka kwa saa sita na kupora Sh9.8milioni, kumuua mtu mmoja na kujeruhi wengine.

Katika tukio la Dar es Salaam, ambalo lilikuwa kama sinema lilidumu kwa zaidi ya saa mbili lakini watuhumiwa hao walijikuta wakiangukia katika mikono ya polisi kutokana na mtego ambao ulikuwa umetegwa dhidi yao.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi wa Ilala, Marietha Minagili alithibitisha kutokea kwa tukio hilo lililoanza saa saba za mchana baada ya watuhumiwa hao wakiwa katika gari aina ya Toyota Corola kuingia katika mtaani hapo na kuelekea katika nyumba waliyokusudia kufanya uhalifu.

Baadhi ya watu walioshuhudia tukio alisema majambazi hao wakati walipokuwa wakielekea katika nyumba hiyo, polisi walikuwa wakiwafuatilia kwa karibu.

Walisema; “Walipoikaribia nyumba hiyo walibaini kuwa polisi walikuwa wakifuatilia ndipo mapambano ya kurushiana risasi yalipoanza na kusababisha taharuki katika eneo hilo na kuwafanya watu waliokuwapo kukimbia ovyo.

Majambazi hao ndiyo waliaza kuwarushia risasi polisi na kuingia katika nyumba waliyokuwa wakienda kuivamia.

Polisi walijibu mapigo hayo kwa kupiga risasi hewani huku wakitoa amri kwa watuhumiwa hao wa ujambazi kujisalimisha, lakini hawakutii na polisi wakawazingira katika nyumba hiyo.

Wakati hali ikiendelea kuwa tete katika mtaa huo, polisi walilazimika kuongeza nguvu kwani magari mengine zaidi ya matatu yakiwa yamesheheni askari polisi wenye silaha yaliwasili.

Magari hayo yalikuwa na askari wa doria na wale wa kikosi maalum cha kupambana na majambazi, wakiungana wenzao waliotangulia kuzingira nyumba hiyo na kuufunga mtaa huo.

Baadhi ya Polisi waliingia katika nyumba hiyo kuwafuata watuhumiwa hao ambao kwa mujibu wa taarifa za polisi, walikuwa wamepanda darini ambako waliamriwa kushuka na kujisalimisha.

Kamanda Marietha alisema kuwa, polisi waliwatia mbaroni watuhumiwa wanne pamoja na bastola moja na risasi sita.

Alisema walifanikiwa kuwakamata baada ya polisi kuweka mtego eneo hilo, kwani mapema walipata taarifa za kuwapo kwa mpango kuwapo kwa uhalifu.

“Tulipata taarifa kutoka kwa raia wema kuwa kuna watu wamekusudia kufanya ujambazi katika nyumba hiyo, hivyo tukajipanga na kufanikiwa kuwatia mbaroni baada ya kukimbilia katika nyumba ambayo walikusudia kufanya uhalifu wao,” alisema Kamanda huyo.

Wengine wateka
kijiji Mwanza

Katika hatua nyingine, watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi ambao idadi yao bado haijafahamika, walivamia Kijiji cha Misasi na Seke wilayani Misungwi, wakiwa na silaha za moto na kufanikiwa kukiteka kwa saa sita na kupora jumla Sh.9.8 milioni, kuua mtu mmoja na kuwajeruhi watatu.

Tukio hilo lilitoke Jumapili iliyopita mnamo saa 2: 47 usiku.

Kamanda wa polisi Mkoa wa Mwanza, Liberatus Barlow alithibitisha kutokea kwa matukio hayo na kubainisha kuwa, jeshi lake linawashikilia
watu wawili kwa tuhuma za kuhusika tukio hilo.

Akielezea uvamizi huo, kamanda Barlow alisema katika tukio la kwanza saa 2:45 kwenye Kijiji cha Misasi, Kata ya Misasi ya Inonelwa wilayani
humo, walivamia nyumbani kwa Mariam Jackson (43) ambaye ni wakala wa kuuza soda anayeishi mita chache na kituo hicho cha polisi.

Kamanda alisema wakiwa nyumbani kwa mfanyabiashara huyo, majambazi hao walifanikiwa kumjeruhi kwa mapanga yeye na mumewe Wiliam Kayichile (60) na mtoto wao aliyefahamika kwa jina la Juliana Peter(19) na Sh400,000.

Wote wamelazwa katika Hospitali ya rufaa ya Bugando kwa matibabu kufuatia kujeruhiwa kichwani kwa mapanga.

Kamanda Barlow alisema baada ya majambazi hao kupora kwa mfanyabiashara huyo na kumjeruhi walikwenda katika Kijiji jirani cha Seke Kata ya Buhingo na kupora kiasi Sh100,000 nyumbani kwa Ramadhani Rashidi (39).

“Baada ya uporaji huo walivamia nyumbani kwa Mwandu Charles wakamjeruhi kwa risasi na kupora Sh4.8 milioni. Majeruhi huyu alifariki wakati akipelekwa hospitali kwa matibabu,” alifahamisha
Kamanda.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

HATUTOPAKI BASI DHIDI YA YANGA-MOKWENA

“PEMBA SALUTI KWENU” DK. NCHIMBI*