Mbeya na utalii wa ndani usiotangazwa

                                             Moja ya minara inayolipendezesha Jiji la Mbeya
                        Matema Beach Hotel iliyopo ufukwe wa wa Ziwa Nyasa waialayani Kyela, Mbeya.
                                Ziwa Ngozi ililopo, Uporoto, wilayani Rungwe, mkoani Mbeya.

MKOA wa Mbeya ni miongoni mwa mikoa ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini inayozalisha mazao ya chakula kwa wingi nchini.

Mbeya ambayo kwa sasa kiutawala ipo chini ya Mkuu wa Mkoa, Abbas Kandoro, ina wilaya tisa na majimbo ya uchaguzi 12.
Wilaya hizo ni Mbeya, Chunya, Mbeya Vijijini, Mbarali, Momba, Mbozi, Ileje, Rungwe na Kyela.

Majimbo ya uchaguzi ni Rupa, Songwe, Momba, Mbozi Magharibi, Mbozi Mashariki, Ileje, Mbeya Vijijini, Mbeya Mjini, Mbarali, Rungwe Magharibi, Rungwe Mashariki na Jimbo la Kyela.

Mbali na uzalishaji wa mazao ya chakula, mkoa una kivutio cha utalii kinachojulikana kuwa labda pekee ndicho kilichopo mkoani hapa ambacho ni Kimondo kilichopo Wilaya ya Mbozi.

Mbali na kivutio hicho ambacho walau kimetangazwa na serikali kwa asilimia fulani, vivutio vingine vilivyojaribu kutangazwa ni Mbuga ya wanyama Lukwati iliyopo wilayani Chunya na Hifadhi ya Taifa ya Kitulo huku vivutio lukuki vya utalii wa ndani vikiwa vimeachwa kama vile havina umuhimu.

Kati ya vivutio vya ndani vilivyopo Mbeya ambavyo havijatangazwa ni alama ya unyayo wa mguu wa mtu wa kale iliyopo Nkangamo wilayani Momba, michoro ya kale iliyopo eneo hilohilo inayosadikika kuchorwa miaka 3,000 iliyopita.

Pia kuna makundi makubwa ya mamba yaliyopo katika Ziwa Rukwa upande wa Mbeya wilayani Mbozi na maji ya moto yaliyopo katika chemichemi ya Songwe, maporomoko ya maji ya Nsala na Mfuto wilayani Mbozi.

Si hivyo tu, bali kuna vivutio vingine vya utalii wa ndani ambavyo havijatangazwa kama mashamba makubwa ya kahawa yaliyopo Mbeya ambapo inasadikika kuwa ni sehemu ya kwanza katika uwekezaji uliofanywa na Wazungu hapa nchini kufungua mashamba hayo yaliyopo wilayani Mbozi.

Hivyo ni vivutio muhimu katika kizazi hiki ambacho kinahitaji kipate historia yake maana utamaduni na mambo kama haya ya historia ndiyo urithi na kielelezo cha nchi yoyote duniani.

Urithi mwingine wa historia hapa nchini ambao ni kivutio tosha ni daraja linalojulikana kwa jina la Daraja la Mungu lililopo Kiwira wilayani Rungwe ambapo wenyeji wa eneo hilo wanasema kuwa daraja hilo halijawahi kutengenezwa na mtu yeyote bali vizazi na vizazi vililikuta daraja hilo na ndiyo kisa cha kuliita daraja la Mungu.
Kuna Ziwa Ngozi lililopo Namba One ambalo liko urefu wa mita 150 kutoka kilele cha milima inayozunguka ziwa, ambapo kina cha maji lina urefu wa mita 73 na ukubwa wa kilometa za mraba ni 3.75.

Ziwa hilo limezungukwa na misitu mizuri ya asili ya kitropiki hali nzuri ya hewa na tulivu.

Ili kulifikia ziwa hilo ni lazima kutembea kwa mwendo wa kati ya dakika 45 na saa moja kutoka Kijiji cha Mbeya One ambacho kipo barabara kuu ya Mbeya-Kyela.

Kutoka katika kilele cha milima inayozunguka ziwa hilo unalazimika kushuka kwa zaidi ya dakika 45 kwa kutumia mizizi migumu ya miti ya asili iliyopo katika msitu mnene kwa sababu ya mteremko mkali kuelekea katika ziwa hilo.

Ziwa hilo linasadikika kugunduliwa mwaka 1925 likitokea kijiji cha Mwakaleli wilayani Kyela baada ya kudaiwa kuchomwa na jiwe la moto na wakazi wa kijiji hicho ambao ni kabila la Wanyakyusa.
Pia linasadikika kuwa na maajabu ikiwa ni pamoja na kusikia sauti za vikohozi vya watu wasioonekana pamoja na miujiza ya watu wanaotwanga mahindi lakini hawaonekani.

Hata hivyo kwa sasa unapofika eneo hilo misitu inayozunguka ziwa hilo ina hali nzuri pamoja na baadhi ya wanyama wakiwemo nyani huku maji ya ziwa hilo yakiwa yanatumiwa kama mradi wa vijana ambao wamekuwa wakiuza kati ya sh 300 na 500 kwa lita.

Wakazi wa kijiji hicho, wanaamini kuwa maji ya ziwa hilo ni dawa kwa ajili ya kutibu watoto ambao wamekuwa wakishtuka nyakati za usiku na kwamba pindi wanaponywesha maji hayo hali hiyo hukoma mara moja.

Ziwa Ngozi ni moja ya maziwa 10 yaliyopo wilayani Rungwe ambapo maziwa mengine yanayofaa kwa utalii wa ndani ni Ndwati, Kisiba, Chungululu, Ikapu, Itamba, Asoko, Ilamba, Kingili, Katubwi na Itende.

Ziwa Kisiba lililopo eneo la Masoko ambalo hakuna mto unaoingia humo lakini maji yake hayapungui kwa msimu wa kila mwaka linasadikika kuwa kuna masanduku ya fedha chini yake lakini hakuna anayefanikiwa kuyachukua kutokana na mazindiko ya kiasili.

Pia kuna kivutio kingine kijulikanacho kwa jina la Kijungu kinachosemekana kiliua watu zamani hasa kabila la Kindali linalosadikiwa ni la watu wabishi.

Hivyo watu wa kabila hilo walikuwa wakiruka na kupotelea ndani ya kijungu hicho ambapo wenzao walikuwa wakiwadhihaki na kusema (utanyelite bhukomu) maana yake haujui kuruka vema ndiyo maana walikuwa wakitumbukia na kupotea.

Kijungu hicho kinasadikika kuwa mahala kilipo kulikuwa ni sehemu ya matambiko ya kimila hivyo ukipita eneo hilo na kuruka kilikuwa kinatanuka kisha mrukaji kutumbukia na kupotea.

Kijungu hicho kipo chini ya mto wa Kiwira karibu na Daraja la Mungu na maporomoko ya maji wilayani Rungwe.

Kwa upande wa Ziwa Nyasa lenye samaki zaidi ya aina 1000 wakiwamo samaki wa mapambo ambao ni sehemu nzuri ya utalii wa ndani na uchumi wa taifa letu kwa ujumla ukiwemo ufukwe wa Matema Beach.

Mbali na vivutio nilivyoviainisha hapo juu, pia kuna kivutio cha utalii wa ndani ambacho ni mbunga ya kutengenezwa (kufugwa) na makumbusho yaliyopo eneo la Ifisi-Mbalizi Wilaya ya Mbeya Vijijini karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Songwe.

Nikirudi kuhusu Kimondo ambacho ni kama jiwe gumu, kinaelezwa kuwa kilidondoka kutoka mawinguni hadi ardhini.

Kimondo hicho kipo eneo la Kijiji cha Ndolezi wilayani Mbozi, mkoani Mbeya na ni kimondo chenya utofauti mkubwa na vimondo vilivyowahi kuanguka duniani.

Eneo hilo ambalo kimondo hicho kinapatikana takribani kilomita 70 kutoka jijini Mbeya na ili kukifikia unapita barabara ya lami ambayo ni barabara kuu ya Tanzania-Zambia, ambapo ukifika eneo la Mahenje kuelekea njia ya Masangula na Masoko unaelekea Kijiji cha Ndolezi mahala ambapo kipo kimondo hicho.

Kupitia makala hii natoa wito kwa wanaharakati, waandishi wa habari na serikali kwa ujumla kujitokeza kuhamasisha utalii wa ndani na kuvitangaza vivutio kama hivi ninavyoamini vipo kila kona ya nchi yetu na huo ndio urithi wa vizazi vyetu.

Kama tutafanya hivyo kwa pamoja, kuvitangaza na kuvielezea vivutio vyetu ikiwa ni pamoja na kuwaelimisha wananchi wanaoishi karibu na vivutio hivi kuvitunza hakuna ambaye atapinga kuhifadhi na kuvitunza vivutio hivi.

Naishauri serikali kuchukua hatua za makusudi kutangaza vivutio vilivyopo Mbeya na mikoa mingine badala ya kuishia kuangalia zaidi vivutio vilivyopo mikoa michache hapa nchini, hasa mikoa ya Kanda ya Kaskazini.Chanzo; Tanzania Daima
0

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

HIVI NDIVYO BIASHARA YA NGONO NAMNA INAVYOTIKISA MOROGORO: SEHEMU YA PILI.

DC MJEMA AONJA ADHA YA MAFURIKO AKIKAGUA ATHARI ZA MAFURIKO ILALA

DC MKURANGA AZINDUA MRADI WA MASHAMBA MJI YA NAMAINGO MSOLWA

TGGA WAMUAGA BOSS WA GIRL GUIDES AFRIKA KWA HAFLA KABAMBE

WAPENZI WANASANA WAKIFANYA MAPENZI GESTI

IJUE HISTORIA YA UHASIMU WA KOREA KASKAZINI NA MAREKANI

ANGALIA PICHA NDEGE KUBWA YA ABIRIA DUNIANI ILIYOANZA SAFARI NDEFU ZAIDI!

Wasafi TV kuanza kurusha matangazo yake leo (+video)

WAGGGS AFRIKA WAIPONGEZA TGGA KWA KUONGOZA AFRIKA KUSAJILI GIRL GUIDES WENGI