Ni gharika Yanga, Azam

TIMU ya Yanga leo inakabiliwa na kibarua kigumu cha kutetea ubingwa wake wa Kombe la Kagame mbele ya Azam katika mechi ya fainali itakayochezwa uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

Wakati Yanga chini ya Kocha wake Tom Seintfiet ikitaka kushinda kuweka rekodi ya kulitwaa mara ya tano tangu kuanzishwa rasmi michuano hiyo 1974, Azam wanataka kubeba mara ya kwanza.
Mbali ya Yanga kutaka kutwaa taji hilo mara ya tano baada ya kufanya hivyo mwaka 1975, 1993, 1999 na 2011, Kocha Saintfiet, pia atakuwa akitaka kuanza vizuri kibarua chake.

Aidha, kama Yanga itafungwa itakuwa imetema taji la michuano hiyo ililolitwaa Julai 10, 2011 chini ya Kocha Mganda, Sam Timbe.
Pia, kufungwa kwake itakuwa pigo kubwa kwa uongozi mpya wa klabu hiyo ulioingia madarakani Julai 15 kupitia uchaguzi mdogo chini ya Mwenyekiti wake Yusuf Manji.

Mazingira hayo, yanaifanya Yanga kucheza kufa na kupona kuhakikisha wanashinda sio tu kutetea taji, pia kuanza vizuri kwa kocha na uongozi mpya.

Azam wao chini ya Kocha wao Stewart Hall, ni kama hawana cha kupoteza leo kwani kwa kufika hatua ya fainali, ni fahari kwao kutokana na kushiriki michuano hiyo kwa mara ya kwanza.

Wakati Yanga ikishiriki michuanio hiyo tangu kuasisiwa kwake, Azam iliyoanzishwa Juni 24, 2007, imeshiriki mara ya kwanza, hivyo hata ikifungwa, bado itastahili pongezi kubwa.

Mbali ya kufika fainali, Azam ni timu iliyoonyesha kiwango bora kiuchezaji tangu hatua ya makundi, robo fainali na nusu fainali ikiing’oa timu ngumu ya AS Vita ya DR Congo.

Sababu hizo zinaifanya mechi ya leo kuwa yenye ushindani mkali zaidi dimbani huku Azam ikitarajia kupata sapoti kubwa ya hamasa kutoka kwa mashabiki wa Simba.

Ingawa Yanga leo inacheza na Azam, kwa upinzani wa jadi wa wapenzi wa soka nchini, mechi ya fainali itachukua sura ya Uyanga na Usimba.

Saintifiet kwa upande wake amedokeza kuwa, amefuatilia uchezaji wa Azam katika mechi zake na kubaini kuwa, ni timu inayocheza soka ya kiwango cha juu, lakini hana shaka na vijana wake.

“Azam si timu ya kubeza, ni timu ambayo binafsi naihofia kutokana na kiwango chake, nitawakabili nikijua ugumu wa mechi hiyo, kocha wao anajua nini anafanya, lolote linaweza kutokea kesho (leo),” alisema Saintfiet anayeweza kumpanga beki wake Juma Abdul kutokana na kupona maumivu.

Nae Kocha Msaidizi wa Azam, Kali Ongala, alisema wamejipanga vizuri kushinda mechi ya leo kwani Yanga si timu ngeni kwao, watahakikisha wanaendeleza rekodi ya kuwafunga.

“Tuko fiti, naamini vijana watapambana kufa na kupona kuwafunga Yanga kuweka rekodi ya kutwaa ubingwa wa michuano hiyo kwa mara ya kwanza,” alisema Ongala aliyekuwemo kwenye kikosi cha Yanga kilichobeba taji hilo mwaka 1999 mjini Kampala, Uganda.
Hali ya mambo ikiwa hivyo, rekodi baina ya timu hizi, zinaibeba Azam ambayo imeshinda mara zote nne walizokutana kati ya Septemba, 2011 hadi Machi 10, 2012.

Yanga ambayo jana ilihamisha kambi kutoka Jangwani hadi hoteli ya Double Tree, Masaki, imefungwa mara zote mbili katika Ligi Kuu ya bara msimu uliopita; Septemba 18, 2011 (1-0) kabla ya kulimwa 3-1, Machi 10, 2012.

Desemba 20, 2011, Yanga ilifungwa 2-0 katika mechi ya Hisani kuchangia fedha za kugomboa vifaa vya walemavu zilizokuwa zimekwama bandarini.

Aidha, ushindi wa Azam wa 3-0 wa Januari 7, 2012 katika mechi ya robo fainali ya Kombe la Mapinduzi, inaifanya Yanga kuwa na rekodi mbaya, ingawa si kigezo pekee cha kufungwa tena leo.
Fainali hiyo itatanguliwa na mechi ya mshindi wa tatu kati ya APR ya Rwanda waliofungwa na Yanga 1-0 katika nusu fainali dhidi ya AS Vita iliyofungwa na Azam 2-1.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA

DKT NCHIMBI ASHIRIKI MAZISHI YA ASKOFU.GACHUMA WA KANISA LA NLGCC

π™‚π˜Όπ™ˆπ™Šπ™‰π˜Ώπ™„ π™†π˜Όπ˜Ύπ™ƒπ™€π™•π˜Ό π™†π™„π˜½π™„π™‰π™‚π™’π˜Ό.