NI FAINALI AMBAYO HAPEWI MTOTO MAJUKUMU LEO YANGA NA AZAM


Kikosi kilichoipeleka Yanga fainali mwaka huu; Kutoka kulia waliosimama Nadir Cannavaro, Kevin Yondan, Said Bahanuzi, Ally Barthez, Athumani Chuji na Oscar Joshua. Waliopiga magoti kutoka kulia ni Juma Abdul, David Luhende, Haruna Niyonzima, Godfrey Taita na Hamisi Kiiza.
Na Mahmoud Zubeiry
NYASI za Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam leo zinatarajiwa kuhimili patashika tena ile ya nguo kuchanika, wakati washindi wa pili wa Ligi Kuu ya Bara msimu uliopita, Azam FC watakapomenyana na washindi wa tatu, Yanga SC katika fainali ya Klabu Bingwa ya soka Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame.
 
Hii inakuwa mara ya pili mfululizo, kwa fainali ya michuano hiyo kukutanisha timu za Dar es Salaam pekee, mwaka jana mabingwa watetezi, Yanga wakitwaa taji hilo kwa kuwafunga watani wao wa jadi, Simba SC 1-0 bao pekee la mshambuliaji ambaye amekwishatupiwa virago, Kenneth Asamoah dakika ya 118 katika mechi iliyodumu kwa saa mbili.
 
Yanga, leo wanatetea taji dhidi ya timu ambayo inakuja juu kwa kasi ya kuridhisha katika soka ya Tanzania, tayari kuingia kwenye orodha ya timu mpya tishio barani Afrika kama Berekum Chelsea ya Ghana, Azam FC inayomilikiwa na mfanyabiashara Said Salim Bakhresa.
 
Yanga wataingia uwanjani, wakiwa na kumbukumbu ya kufungwa mechi tatu mfululizo za mashindano na Azam msimu uliopita, mbili za Ligi Kuu na moja ya Kombe la Mapinduzi na zaidi mbele ya mdomo wa lango lao, atakuwapo John Bocco ‘Adebayor’, ambaye amekuwa na bahati ya kutikisa nyavu zao.
 
Lakini kwa ujumla, tangu Azam ipande Ligi Kuu mwaka 2008, imekutana na Yanga mara 14, imeshinda mara saba, sare tatu na kufungwa nne.
 
Ukuta wa Yanga, utakaoongozwa na Kelvin Patrick Yondan, utakuwa na shughuli nzito ya kukabiliana na viungo washambuliaji wa Azam wenye kasi kama Kipre Herman Tchetche, ambaye kwenye mashindano ya mwaka huu amecheza kwa kiwango cha juu.
 
Lakini ukuta wa Azam utakaongozwa na Mwanasoka Bora wa Tanzania, Aggrey Morris utakuwa na kibarua kizito cha kukabiliana na washambuliaji wawili wenye uchu, Said Bahanuzi ‘Spider Man’ na Hamisi Kiiza ‘Diego’, ambao kwa pamoja wameifungia Yanga mabao 10, matano kila mmoja hadi sasa sawa na Bocco.
 
Kocha wa Yanga, Tom Saintfiet amesema kwamba fainali ya Kombe la Kagame itakuwa ngumu kwa sababu wapinzani wao, Azam FC ni timu yenye kucheza kandanda ya kuvutia na amesikitikia kuwa na majeruhi wengi kikosini.
 
Amesema katika mchezo wa leo, atawakosa nyota wake wanne kati ya 20 aliowasajili kwa ajili ya mashindano haya, ambao ni kipa Yaw Berko, mabeki Juma Abdul ambao ni majeruhi, Godfrey Taita anayetumikia adhabu ya kadi nyekundu na Nizar Khalfan ambaye ni majeruhi pia.
 
Hata hivyo, Mtakatifu Tom amesema kwamba pamoja na ukweli huo wanahitaji kutetea Kombe na watapigana hivyo hivyo pamoja na changamoto zinazowakabili kuhakikisha taji linabaki nyumbani.
 
Ikumbukwe Yanga ilifuzu kuingia Fainali, baada ya kuifunga APR 1-0, bao pekee la mwanasoka bora wa Uganda, Hamisi Kiiza ‘Diego’ dakika ya 110, akiunganisha krosi ya karibu ya Haruna Niyonzima ambaye alitumia mwanya wa mabeki wa APR kuzubaa wakisikilizia maamuzi ya refa, baada ya Said Bahanuzi kuangushwa.
 
Wakati Azam wanawania taji la kwanza kabisa la michuano hii, wanayoshiriki kwa mara ya kwanza, Yanga watakuwa wakisaka taji la tano, baada ya awali kutwaa Kombe hilo 1975, 1993, 1999 na 2011.
 
Kocha Muingereza, Stewart Hall wa Azam FC iliyoitoa AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ili kuingia fainali, kwa kuifunga mabao 2-1, mabao yake yakifungwa na John Bocco ‘Adebayor’ na Mrisho Ngassa, amesema kwamba Yanga ni timu nzuri na fainali hiyo itakuwa ‘classic’, yaani baab kubwa.
 
Stewart ambaye mapema mwaka huu aliiwezesha Azam kutwaa taji la kwanza, Kombe la Mapinduzi, alisema kwamba Yanga imekuwa ikiimarika siku hadi siku na sasa imefikia kuwa timu bora na anatarajia upinzani mkali leo.
 
Muingereza huyo alisema kwamba pamoja na ukweli huo nia yao Azam ni kutwaa Kombe hilo. “Vijana wangu hadi sasa wamenifurahisha kwa kucheza kwa kufuata maelekezo yangu. Mechi na AS Vita ilikuwa ngumu, hadi mapumziko tulikuwa nyuma kwa 1-0. Lakini niliwaambia tukiwa vyumbani, watulie tuendelee kucheza mpira wetu, tusihamaki, walinielewa na wakacheza nilivyotaka.
 
Hiyo ndio siri ya ushindi, kwa kiwango kile na uchezaji ule, naona kabisa tunaweza kuwafunga Yanga na kuchukua Kombe, timu yetu ni nzuri na wachezaji wanatulia uwanjani kama ulivyoona,”alisema.
 
Stewart sasa baada ya kuiwezesha Azam kuwa timu ya pili nje ya Simba na Yanga kuingia fainali ya Kombe la Kagame, baada ya Moro United mwaka 2006, ambayo ilifungwa na Polisi Uganda mabao 2-1, anafukuzia rekodi ya kuifanya Azam kuwa timu pekee nchini nje ya vigogo hao, kutwaa taji hilo.
 
Katika mchezo wa leo, vikosi vinatarajiwa kuwa;
Yanga SC; Ally Mustafa ‘Barthez’, Stefano Mwasyika, Oscar Joshua, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Athumani Iddi ‘Chuji’, Rashid Gumbo, Haruna Niyonzoma, Said Bahanuzi, Hamisi Kiiza na David Luhende. Benchi; Shamte Ally, Juma Seif, Ladislaus Mbogo, Idrisa Assenga na Jerry Tegete.
 
Azam FC; Deo Munishi ‘Dida’, Ibrahim Shikanda, Erasto Nyoni, Said Mourad, Aggrey Morris, Jabir Aziz, Kipre Tcheche, Salum Abubakar, John Bocco ‘Adebayor’, Ibrahim Mwaipopo na Ramadhan Chombo ‘Redondo’. Benchi; Mwadini Ally, Samir Haji Nuhu, Joseph Owino, George Odhiambo, Mrisho Ngassa, Khamis Mcha ‘Vialli’ na Gaudence Mwaikimba. Kwa hisani ya Bin Zubeiry Blog
Kikosi kilichoipeleka Azam fainali, kutoka kulia waliosimama ni Said Mourad, Ibrahim Mwaipopo, Aggrey Morris, Erasto Nyoni, John Bocco na Ramadhan Chombo. Walioinama kutoka kulia ni Jabir Aziz, Salum Abubakar, Ibrahim Shikanda, Kipre Tcheche na Deo Dida.
JE, WAJUA?
1.                      Yanga ilizaliwa rasmi mwaka 1935 na tangu wakati huo imekuwa ikicheza mashindano makubwa ya kitaifa, hadi ujio wa Klabu Bingwa ya Taifa, mwaka 1966, ambayo baadaye iligeuzwa kuwa Ligi Daraja la Kwanza, 1982 na mwaka 1996 ikawa Ligi Kuu, wakati Azam FC ilizaliwa mwaka 2004 na ikaanza kucheza Ligi Kuu mwaka 2008.
2.                      Hii ni fainali ya pili mfululizo kuzikutanisha timu za Tanzania tupu, baada ya ile ya mwaka jana na pia ni fainali ya nne kwa ujumla, baada ya zile za mwaka 1975, 1992 na 2011 kuzikutanisha timu za Tanzania tupu, nyingine zote zikizikutanisha Simba na Yanga.
3.                      Azam inakuwa timu ya pili nje ya Simba na Yanga, kihistoria kuingia fainali ya michuano hii, baada ya Moro United kufanya hivyo mwaka 2006 na kufungwa na Polisi Uganda mabao 2-1 Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, mgeni rasmi akiwa rais Jakaya Mrisho Kikwete.
4.                      Tangu Azam FC ipande Ligi Kuu ya Tanzania Bara, inayodhaminiwa na kampuni ya Vodacom Tanzania, mwaka 2008, imekwishakutana na Yanga mara 14 na imefanikiwa kushinda mechi saba zikiwemo tatu mfululizo zilizopita, sare tatu na kufungwa nne,
5.                      Kocha Msaidizi wa Azam FC, Kali Ongala, mtoto wa mwanamuziki nyota wa zamani Tanzania, Dk Remmy Ongala (sasa marehemu), alikuwemo kwenye kikosi cha Yanga kilichotwaa Kombe la Kagame mwaka 1999 mjini Kampala, Uganda, wakiifunga SC Villa kwa penalti 5-3 kufuatia sare ya 1-1 ndani ya dakika 120.
6.                      Kiungo wa Azam FC, Salum Abubakar, baba yake, Abubakar Salum ‘Sure Boy’alikuwemo kwenye kikosi cha Yanga kilichotwaa Kombe la michuano hiyo, mwaka 1993 mjini Kampala, Uganda wakiifunga SC Villa 2-1.
7.                      Hadi inaingia kwenye mechi ya leo, Azam FC haijafungwa mechi hata moja, kuanzia kwenye mechi za Kundi lake, B, ikianza kwa kutoa sare ya 1-1 na Mafunzo, 0-0 na Tusker, kabla ya kuifunga Simba SC mabao 3-1 katika Robo Fainali na AS Vita mabao 2-1 katika Nusu Fainali.
8.                      Yanga ilikaribishwa kwenye michuano ya mwaka huu na kipigo cha 2-0 kutoka kwa Atletico ya Burundi katika Kundi C, kabla ya kushinda 7-1 dhidi ya Waw Salaam ya Sudan Kusini, na 2-0 dhidi ya APR ya Rwanda, ilishinda kwa penalti 5-3 dhidi ya Mafunzo katika Robo Fainali, kufuatia sare ya 1-1 na ikashinda 1-0 dhidi ya APR katika Nusu Fainali ndani ya dakika 120.
9.                      Katika mabao 11 iliyofunga Yanga hadi sasa, mabao 10 yamefungwa na watu wawili, Hamisi Kiiza ‘Diego’ na Said Bahanuzi ‘Spider Man’ na lingine Nizar Khalfan, wakati katika mabao sita ya Azam FC hadi sasa, matano yamefungwa na mtu mmoja, John Bocco ‘Adebayor’, lingine Mrisho Ngassa.
10.             Makipa wote watakaonza leo, Ally Mustafa kwa Yanga, na Deo Munishi kwa Azam wana sifa mbili kubwa. Kwanza ni majina yao ya utani, Ally ‘Fabian Barthez’ alikuwa kipa wa Ufaransa iliyotwaa Kombe la Dunia mwaka 1998, ikiifunga 3-0 Brazil katika fainali, ambayo kipa wake alikuwa Dida, (jina la utani la Deo Munishi wa Azam) ambaye siku ya fainali alikaa benchi wakati Taffarel anatunguliwa na Zidane mawili na lingine Petit. Pili, wote hawa walikuwa makipa wa akiba wa Simba, mbele ya Juma Kaseja.
11.             Mwenyekiti wa Yanga, Yussuf Mehboob Manji ni mfanyabiashara maarufu mwenye asili ya Kiasia, ambaye utajiri wake ni wa kurithi kutoka kwa marehemu baba yake, Mehboob Manji, amesoma pamoja na Mkurugenzi wa Azam, Yussuf Said Bakhresa, Howard University, Washington, D.C. Marekani- ambaye naye pia anaendeleza utajiri wa baba yake, Said Salim Bakhresa kwa pamoja na ndugu zake, chini ya kaka yao, Abubakar.
ORISHA YA MABINGWA, WENYEJI NA WASHINDI WA PILI KOMBE LA KAGAME
MWAKANCHIBINGWAMATOKEOMSHINDI WA PILINCHIMWENYEJI
1967 KenyaAbaluhya5–0dagger[A]Sunderland Tanzania
1968-73
Halteddagger[B]
1974 TanzaniaSimbaAbaluhya Kenya Tanzania
1975 TanzaniaYoung Africans2–0Simba Tanzania Zanzibar
1976 KenyaLuo Union2–1Young Africans Tanzania Uganda
1977 KenyaLuo Union2–1Horsed Somalia Tanzania
1978 UgandaKampala City Council0–0*[C]Simba Tanzania Uganda
1979 KenyaAbaluhya1–0Kampala City Council Uganda Somalia
1980 KenyaGor Mahia3–2Abaluhya Kenya Malawi
1981 KenyaGor Mahia1–0Simba Tanzania Kenya
1982 KenyaA.F.C. Leopards1–0Rio Tinto Zimbabwe Kenya
1983 KenyaA.F.C. Leopards2–1ADMARC Tigers Malawi Zanzibar
1984 KenyaA.F.C. Leopards2–1Gor Mahia Kenya Kenya
1985 KenyaGor Mahia2–0A.F.C. Leopards Kenya Sudan
1986 SudanAl-Merrikh2–2*[D]Young Africans Tanzania Tanzania
1987 UgandaVilla1–0Al-Merrikh Sudan Uganda
1988 KenyaKenya Breweries2–0Al-Merrikh Sudan Sudan
1989 KenyaKenya Breweries3–0Coastal Union Tanzania Kenya
1990
HAYAKUFANYIKAdagger[E]
1991 TanzaniaSimba3–0Villa Uganda Tanzania
1992 TanzaniaSimba1–1*[F]Young Africans Tanzania Zanzibar
1993 TanzaniaYoung Africans2–1Villa Uganda Uganda
1994 SudanAl-Merrikh2–1Express Uganda Sudan
1995 TanzaniaSimba1–1*[G]Express Uganda Tanzania
1996 TanzaniaSimba1–0ArmΓ©e Patriotique Rwandaise Rwanda Tanzania
1997 KenyaA.F.C. Leopards1–0Kenya Breweries Kenya Kenya
1998 RwandaRayon Sports2–1Mlandege Zanzibar Zanzibar
1999 TanzaniaYoung Africans1–1*[H]Villa Uganda Uganda
2000 KenyaTusker3–1ArmΓ©e Patriotique Rwandaise Rwanda Rwanda
2001 KenyaTusker0–0*[I]Oserian Kenya Kenya
2002 TanzaniaSimba1–0Prince Louis Burundi Zanzibar
2003 UgandaVilla1–0Simba Tanzania Uganda
2004 RwandaArmΓ©e Patriotique Rwandaise3–1Ulinzi Stars Kenya Rwanda
2005 UgandaVilla3–0ArmΓ©e Patriotique Rwandaise Rwanda Tanzania
2006 UgandaPolice2–1Moro United Tanzania Tanzania
2007 RwandaArmΓ©e Patriotique Rwandaise2–1Uganda Revenue Authority Uganda Rwanda
2008 KenyaTusker2–1Uganda Revenue Authority Uganda Tanzania
2009 RwandaATRACO1–0Al-Merrikh Sudan Sudan
2010
Not helddagger[J]
2011 TanzaniaYoung Africans1–0Simba Tanzania Tanzania
2012
TanzaniaYoung AfricansVsAzam Tanzania Tanzania
LEO

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA

DKT NCHIMBI ASHIRIKI MAZISHI YA ASKOFU.GACHUMA WA KANISA LA NLGCC

π™‚π˜Όπ™ˆπ™Šπ™‰π˜Ώπ™„ π™†π˜Όπ˜Ύπ™ƒπ™€π™•π˜Ό π™†π™„π˜½π™„π™‰π™‚π™’π˜Ό.