SEHEMU YA HOTUBA YA MSEMAJI WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI WIZARA YA NISHATI NA MADINI JOHN JOHN MNYIKA (MB)

UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika, awali ya yote niungane na wote wenye mapenzi mapema katika kuomba ulinzi wa Mwenyezi Mungu wakati tukitimiza wajibu wa kibunge kwa mujibu wa ibara ya 63 ya Katiba ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania na Kanuni Kudumu za Bunge (Toleo la mwaka 2007) kifungu cha 99 (7) wa kuishauri na kuisimamia serikali; kwa kuwasilisha maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani kuhusu mapitio ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2011/2012 na makadirio ya matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2012/2013.
Mheshimiwa Spika, nitumie pia nafasi hii kuwashukuru Watanzania wenzangu wa kada, hadhi na ngazi mbalimbali katika taasisi na maeneo mengi ndani na nje ya nchi waliouniunga mkono kwa hali na mali katika kipindi chote cha misukosuko ya kusimamia ukweli na uwajibikaji: katika kuifuatilia serikali na kuunganisha wadau wengine kuwezesha maendeleo katika jimbo la Ubungo; wakati wa kesi ya kupinga matokeo ya ushindi wetu; wakati wa operesheni za kuhamasisha mabadiliko katika maeneo mengine nchini na katika uwakilishi wa wananchi bungeni. Utaratibu wa kupokea maoni na kutoa taarifa za mara kwa mara za maendeleo kupitia mikutano na wananchi pamoja na katika mtandao wa http://mnyika.blogspot.com tutaendelea nao. Kaulimbiu yetu ni ile ile: AMUA; Maslahi ya Umma Kwanza.
Mheshimiwa Spika; Sekta za Nishati na Madini zina umuhimu maalum katika uchumi wa nchi na maisha ya wananchi katika kipindi cha sasa na muda mrefu ujao. Wakati nishati ikiwa nyenzo ya kuendesha maisha ya kiuchumi, kisiasa na kijamii ya wananchi na nchi kwa ujumla; madini ni mtaji na ni kati ya mitaji mikubwa ya kuwezesha maendeleo ya haraka ya taifa. Hata hivyo, pamoja na Tanzania kujaliwa rasilimali hizi nyingi ikiwemo watu, ardhi yenye rutuba, maji (bahari, mito na maziwa), kuwa katika eneo la kimkakati la kijiografia kwa biashara na maliasili, bado takwimu za hali ya uchumi kwa mwaka 2011 zinaonyesha sehemu kubwa ya Watanzania wako kwenye lindi la umaskini.
Mheshimiwa Spika, tunajadili sekta za nishati na madini wakati taifa likiwa kwa mara nyingine tena kwenye tishio la mgawo wa umeme pamoja na serikali kukanusha kwamba hakutakuwa na mgawo wa umeme. Tunajadili mapitio ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2011/2012 wakati kwa mara nyingine tena kukiwa na mvutano

baina ya watendaji waandamizi wa Wizara ya Nishati na Madini na Taasisi zake wakiwa katika mvutano ambao umeambatana na kutuhumiana hadharani kupitia vyombo vya habari juu ya tuhuma za ubadhirifu na matumizi mabaya ya madaraka. Tunajadili makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka 2012/2013 wakati kukiwa na tuhuma za vigogo wa serikali kuingiziwa fedha kifisadi katika akaunti zao za nchini Uswisi na makampuni ya nje ya utafutaji na uchimbaji wa madini, mafuta na gesi asili huku viongozi wa dini wakiwa wamezindua ripoti juu ya ukwepaji kodi na upotevu wa mapato kwa serikali unaogusa pia makampuni kwenye sekta za nishati na madini (The One Billion Dollar Question).
Mheshimiwa Spika, namuomba kila mmoja wetu atafakari kwa ukweli wa nafsi na nafasi yake tumefikaje hapa kama taifa na kwa pamoja tukubaliane kuwa wabunge tuwajibike kuisimamia serikali kuhakikisha maazimio yote ya bunge kuhusu sekta za nishati na madini ya miaka mbalimbali yanatekelezwa kwa haraka na kwa ukamilifu. Naamini iwapo maazimio ya Bunge juu ya Mkataba baina ya TANESCO na Kampuni ya Richmond Development Company LLC yangetekelezwa yote na kwa wakati toka mwaka 2008, maazimio ya bunge juu ya uendeshaji wa sekta ndogo ya gesi asili ya mwaka 2011 yangezingatiwa yote na kwa haraka, maazimio kuhusu uhalali wa utaratibu wa Wizara ya Nishati na Madini kuchangisha fedha kwa ajili ya kupitisha bajeti bungeni ya mwaka 2011 yangechukuliwa

kwa uzito unaostahili; taifa lingeepushwa kurudia mijadala ile ile kuhusu Wizara hii hii mara kwa mara. Aidha, kambi rasmi ya upinzani inatoa mwito kwa bunge kupitisha maazimio ya kutaka uwajibikaji wa serikali kwa kushindwa kutekeleza maazimio ya bunge kwa ukamilifu na kwa wakati.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Katiba ya Nchi Ibara ya 52 (1) Waziri Mkuu ndiye mwenye madaraka juu ya udhibiti, usimamiaji, utekelezaji wa siku hata siku wa kazi na shughuli za Serikali ya Jamhuri ya Muungano na ndiye kiongozi wa shughuli za Serikali Bungeni. Ni muhimu basi, badala ya kupokea majibu ya Wizara ya Nishati na Madini pekee ambayo imeendelea kugubikwa na lundo la tuhuma mbalimbali, Waziri Mkuu atoe kauli bungeni kuhusu kujirudia rudia kwa madai ya ufisadi na uzembe katika sekta za nishati na madini.
Aidha, pamoja na mabadiliko ya Mawaziri, Manaibu waziri, Makatibu wakuu na Wakurugenzi wa Wizara ya Nishati na Madini na taasisi zake ya mara kwa mara, Rais ashauriwe kutumia nguvu zake za kikatiba za ibara ya 33, 34, 35 na 36 kuwezesha hatua za kisheria kuchukuliwa kwa wote waliotuhumiwa kwa ufisadi, uhujumu uchumi na matumizi mabaya ya madaraka kwa mujibu wa maazimio ya bunge na taarifa mbalimbali za serikali ili kurejesha misingi ya uadilifu na uwajibikaji katika sekta za nishati na madini.

Mheshimiwa Spika, hivyo kwa ujumla mjadala wa mapitio ya utekelezaji wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2011/2012 na makadirio ya matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2012/2013 ulenge katika kuliepusha taifa letu kuendelea kutumbukia katika ‘laana ya rasilimali’ kama ilivyojitokeza katika mataifa mengine. Tuhakikishe tunalinda uhuru wa taifa letu dhidi ya uporaji wa ardhi na rasilimali zake yakiwemo madini, mafuta na gesi asili ulio katika tishio la ubeberu mamboleo, ufisadi na udhaifu wa kimifumo. Aidha, kupitia mchakato wa katiba mpya wananchi watoe maoni ya kuhakikisha kuwa rasilimali za muhimu ikiwa ni pamoja na madini, mafuta na gesi zinawekewa mfumo wa kunufaisha watanzania wote na pia mikataba kuhusu rasilimali hizo inaridhiwa na Bunge.
Tuchangie mjadala wa sekta hizi nyeti tukikumbuka maneno ya hayati Mwalimu Nyerere katika kitabu chake cha TUJISAHIHISHE cha mwaka 1962, nanukuu: “Lakini woga unaweza kutokana na tamaa ya kila binadamu kupendwa na binadamu wenzake. Sisi wote tunayo tamaa hii, au sivyo tusingekuwa binadamu. Woga huu huweza ukamfanya mtu kuvumilia maovu, hasa kama maovu yale yanatendwa na walio wengi kwa walio wachache, au yanatendwa na wakubwa kwa wadogo. Kwa kuogopa kuwaudhi wengi tunawaacha watende makosa bila kuwasahihisha, wasije wakatuchukia. Huu ni ubinafsi mbaya sana”
6
MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA MWAKA 2011/2012
Mheshimiwa Spika, tarehe 15 Julai 2011 niliwasilisha bungeni maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani kuhusu mapitio ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2010/2011 na makadirio ya matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2011/2012. Kufuatia maoni hayo, yapo masuala machache ambayo Serikali imeyazingatia kwenye utekelezaji na mengine mengi serikali haikuyazingatia pamoja na umuhimu wake kwa maslahi ya nchi na maisha ya wananchi. Hivyo kupitia mapitio haya ya utekelezaji, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali ieleze hatua ilizochukua juu ya maoni hayo ambayo baadhi yalijitokeza pia kwenye maoni ya Kamati za Kudumu za Bunge na michango ya wabunge kwa nyakati mbalimbali. Hakuna sababu ya kutumia muda mrefu kutoa na kujadili maoni mapya ikiwa hakuna mfumo thabiti wa kuhakikisha maoni na maazimio yanatekelezwa kwa wakati na kwa ukamilifu.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA

DKT NCHIMBI ASHIRIKI MAZISHI YA ASKOFU.GACHUMA WA KANISA LA NLGCC

π™‚π˜Όπ™ˆπ™Šπ™‰π˜Ώπ™„ π™†π˜Όπ˜Ύπ™ƒπ™€π™•π˜Ό π™†π™„π˜½π™„π™‰π™‚π™’π˜Ό.