SSRA imeanza vibaya, ibadilike

WAFANYAKAZI wengi hivi sasa wamekuwa na kilio kikubwa juu ya marekebisho ya sheria za Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya mwaka 2012 yaliyopitishwa na Bunge Aprili 13, mwaka huu na kusainiwa na Rais Jakaya Kikwete.

Sheria hiyo inaweka bayana kuwa mwanachama wa mfuko wowote wa hifadhi ya jamii hataruhusiwa kuchukua mafao yake kwa sababu yoyote mpaka hapo atakapofikisha miaka 55 au 60, tofauti na ilivyokuwa awali ambapo mwanachama alikuwa na uwezo wa kuchukua fedha zake miezi sita baada ya kuanza kazi.

Mabadiliko hayo yanapingwa na wadau kila kukicha huku wengine wakitishia kuiburuza mahakamani Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA), ambayo ina dhamana ya kusimamia mifuko hiyo inayodaiwa kuwekeza kwenye miradi isiyo na faida kiasi cha kuhatarisha fedha za wanachama wake.

Kimsingi tunatambua umuhimu wa uwepo wa SSRA kwa sababu kulikuwa na tofauti kubwa ya mafao baina ya mfuko mmoja kwenda mwingine lakini tungependa kuiomba Mamlaka hiyo kuangalia upya sheria hiyo kwa lengo la kusikiliza na kutii mahitaji ya wanachama wake.

Tunaamini kuwa sheria ili iwe na manufaa ni lazima isikilize mahitaji ya walengwa lakini kama matakwa ya walengwa yatapuuzwa, kuna kila dalili ya kukwama kwa sheria husika na iwapo mamlaka husika zikiilazimisha, tija na ufanisi katika sehemu za kazi vitapungua.

Hatuoni sababu kwa watendaji wa SSRA kutoangalia upya sheria hiyo kwa sababu katika mazingira ya sasa ajira nyingi zimekuwa si za uhakika pamoja na matarajio ya watu kuishi kuzidi kupungua siku hadi siku kulingana na mabadiliko ya hali ya hewa.

Inawezekana lengo la Mamlaka hiyo likawa zuri lakini mguu walioanza nao ukawa mbaya, tuna imani wadau husika wangeshirikishwa kwa mapana zaidi kelele za kuipinga sheria hiyo tunazozisikia hivi sasa zisingekuwapo au kama zingekuwepo basi kwa kiwango kidogo sana.

SSRA wangezunguka kwenye maeneo mbalimbali kuwahamasisha wadau juu ya jambo hilo kabla ya kushiriki katika kuandaa mabadiliko hayo ambayo mpaka sasa ni idadi ndogo ya wafanyakazi waliokuwa wakijua kuna mchakato wa kurekebisha sheria hiyo.

Tumeshaona namna mchakato wa kuandika Katiba mpya unavyofanyika ambapo Tume ya Katiba imekuwa ikipita kwenye maeneo mbalimbali kukusanya maoni ya wananchi juu ya uundwaji wa Katiba wanayoitaka, hivyo ni vema SSRA watumie nafasi hiyo.
Tumesikitishwa na kauli ya Mkurugenzi Mkuu wa SSRA, Irene Isaka, kuwa mamlaka hiyo itakwenda kwenye maeneo ya kazi kutoa umuhimu na ubora wa sheria hiyo, hili tunaamini lingefanywa kabla ya mabadiliko ya sheria hiyo.

Tunaamini kuwa mchakato huu uligubikwa na usiri kutoka kwa viongozi wa serikali na wa mamlaka hiyo, hivyo ni vema wahusika wakatafakari upya juu ya sheria hii na ikiwezekana ifanyiwe marekebisho yenye kuzingatia mahitaji ya wafanyakazi.

Tunaiomba serikali ambayo mara kwa mara imekuwa ikijinasibu kuwa ni sikivu kuonesha usikivu wake kwa kuzingatia mahitaji ya wafanyakazi badala ya kufanya mambo yanayowaumiza wanachama wake.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA

DKT NCHIMBI ASHIRIKI MAZISHI YA ASKOFU.GACHUMA WA KANISA LA NLGCC

π™‚π˜Όπ™ˆπ™Šπ™‰π˜Ώπ™„ π™†π˜Όπ˜Ύπ™ƒπ™€π™•π˜Ό π™†π™„π˜½π™„π™‰π™‚π™’π˜Ό.