TAARIFA YA SMZ KUHUSU AJALI YA MELI YA MV. SKAGIT ILIYOTOLEWA JANA USIKU JULAI 19,2012



Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imetoa taarifa usiku huu ikieleza idadi ya watu waliopatikana wakiwa hai ni 146 na kupata maiti 62.
Akitoa taarifa hiyo kwa vyombo vya habari usiku leo,Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Ali Juma Shamuhuna alisema taarifa hiyo ndio sahihi na kuwataka wananchi kutoamini taarifa zinazotolewa na watu wengine zaidi ya Serikali.
Waziri Shamuhuna alisema kwamba maiti 62 walipatikana ambao kati ya maiti hizo watoto ni 9 na kuna raia mmoja wa kike wa kigeni ambaye hakuweza kutambulika  Uraia wake,lakini umeonekana picha yake moja ndogo ya hati ya kusafiria.
Waziri Shamuhuna alisema meli hiyo ilibeba jumla ya abiria 290 kati ya hao watu wazima 250, watoto wadogo 31 na mabaharia 9.
Waziri huyo aliwataka wananchi katika sehemu mbalimbali hasa katika vijiji vilivyo kandokando ya bahari watakapoona maiti au mtu akiwa hai ambaye wanadhani ni wa ajali ya Meli ya Skagit.
Aidha, Waziri Shamuhuna alisema kwamba kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam ambao watakuwa na wasiwasi wa kutowaona ndugu na jamaa zao amewataka kufika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa ajili ya kupata taarifa zaidi au kuripoti  habari za kupotelewa kwa ndugu au jamaa zao.
Kwa upande wa Zanzibar, Waziri huyo aliwataka wananchi kufika kwa Masheha wao kutoa taarifa kama hizo.
Serikali imewashukuru makampuni binafsi za usafiri baharini kwa msaada wao na wasisite kutoa msaada katika kazi inayoendelea ya kutafuta watu au maiti wengine katika eneo la tukio.
Meli ya Mv. Skagit ilizama Julai 18,2012 karibu na Kisiwa cha Chumbe umbali wa maili sita kuelekea Kusini mwa Kisiwa kidogo cha Yasin Zanzibar ikitokea Bandari ya Dar es Salaam ilikoanza safari saa 5:30 asubuhi.
Meli hiyo inamilikiwa na Kampuni ya Sea Guall Sea Transport Ltd, Kampuni ambayo Meli yake nyengine ya Mv. Fatih ilizama ikiwa Bandarini Malindi Zanzibar na kufariki watu sita mwaka 2009.
Mwisho.
IMETOLEWA NA:
IDARA YA HABARI(MAELEZO) ZANZIBAR
ZANZIBAR, TANZANIA 
JULAI 19,2012

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

HATUTOPAKI BASI DHIDI YA YANGA-MOKWENA

“PEMBA SALUTI KWENU” DK. NCHIMBI*