Urais 2015 wazidi kuwatesa wanasiasa

MEMBE ASEMA HAJAOTESHWA KUGOMBEA, ATANGAZA ORODHA YA MAADUI 11, CUF
YAONYA MAKUNDI CCM NI HATARI

Waandishi Wetu
MBIO za kuwania urais wa mwaka 2015 zimezidi kuwatesa wanasiasa, baada ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe kueleza kuwa hajaoteshwa kuwania kiti hicho, huku Mwenyekiti wa CUF Profesa Ibrahim Lipumba akionya kuwa makundi tofauti yanayowania nafasi hiyo ndani ya CCM ni hatari.Membe mbali na kusema hajaoteshwa kugombea urais, ameeleza kuwa ana orodha ya watu kumi na moja wanaomhujumu na kuonya kuwa ipo siku atawataja kwa majina hadharani.
Waziri Membe alitoa kauli hiyo juzi usiku katika Kipindi cha Dakika 45, kinachorushwa na Televisheni ya ITV kila Jumatatu.

Membe alihusisha hujuma hizo na mbio za Uchaguzi Mkuu wa 2015, baada ya kuulizwa ikiwa watu hao wanamfuatafuata kutokana na suala la Uchaguzi Mkuu ujao wa urais.

“Wanajua mambo yote haya, wanaogopa nisiwaguse na wangekuwa na uwezo wangeanza kampeni, labda nioteshwe (urais) na ole wao nikioteshwa ndoto hiyo…” alisema. Waziri Membe na kuongeza:
“Mtu aliye mbaya wako anakuwa na macho matatu. Kwa hiyo kutokana na uwezo wa jicho la tatu anaanza kuzuia lile analoliona lisitokee. Mimi nina macho sita. Nitawataja. Hebu wewe fikiria, kila baada ya miezi miwili naletewa mitego, vituko. Lakini nawaambia Watanzania, waache waseme na mimi ipo siku itakuwa zamu yangu nitawaweka wazi ili kila mtu aelewe.”
“Wasije wakadhani wakijificha kwa wahariri, majumbani kwao ambako ndiyo kuna ofisi zao kwenye ma-godown (maghala) yao ndiyo watakwepa, nitawalipua ili wajue. Ukikaa juu ya nyoka, akigeuka atakuuma tu.”
“Ipo siku nitawaanika hao watu na wapo kumi na moja. Kuna waandishi wa habari mle ndani wawili. Nitawatwanga peupe. Ninyi subirini hata ndani ya Bunge, nitazipangua tuhuma hizo moja baada ya nyingine. Nikimaliza bungeni wajiandae, nitawaanika majina yao, picha zao na mambo yote waliyoandika kwenye magazeti kwa kipindi cha miaka miwili ya uongozi wangu kwenye wizara.”

“Nilikwenda Brazil nikazungumza na Waziri wao wa Mambo ya Nje changamoto anazokumbana nazo akasema ni uongo. Nikamwuliza anapambana nazo vipi akanipa dawa ambayo ni kuwaanika. Nawaambia nitawaanika hapatakalika hapa.”

“Unajua nchi hii kisiasa ina watu ambao wana nguvu nje ya mamlaka ambayo wanayatumia kuvuruga. Wanapenda tuwe na watu wanaovurugika, wasingependa kuona watu wametulia. Ikiwa utaamka na kusema leo nitajivua gamba, leo nitafanya hivi utaandamwa.
Wapinzani na wabunge
Akizungumzia siasa za vyama vingi, Membe alivikosoa vyama hivyo akivitaka viwe makini.
“Naona bado hatujakaa sawa kwa siasa za vyama vingi. Ni kweli, tuna vyama vya upinzani lakini inabidi viwe makini. Kitu ambacho wapinzani hawajui ni kwamba nguvu ya wananchi inaweza kubadilika saa 24, nguvu ya wananchi iko kama bahari ina mawimbi ya kupanda na kushuka,” alisema.
Alisema vipo baadhi ya vyama vya upinzani barani Afrika, vilivyoingia madarakani na kuanguka akisema vilishindwa kutambua nguvu ya wananchi.

Aliwataka wabunge wa upinzani kutumia muda wao mwingi kuangalia majimbo yao badala ya kusema tu bungeni. “Wapinzani ‘reference’ yao iko majimboni siyo bungeni. kipimo chako cha kazi ni jimboni, siyo ukasuku wa kuzungumza bungeni na waandishi wa habari. Nendeni jimboni kwake mkaone uchungu alionao. Lakini siyo anatumia asilimia 100 kuisemea dunia na nchi nzima huku amelisahau jimbo lake,” alisema.
Aliwakosoa pia wapinzani kwa kukosoa bajeti halafu baadaye wanawafuata mawaziri kuwaomba fedha zilizotengwa.
“Nakwambia naomba tupitishe hizo pesa, unakataa, halafu kesho unakuja na kusema katika hizo pesa ulizopitishiwa naomba kwa ajili ya miradi ya maji,…”

Uendeshaji Bunge
Kuhusu uendeshaji wa Bunge, Membe alisema hakuna tatizo ingawa aligusia kuwepo kwa ushabiki ulioibuka ambao alisema unalipeleka pabaya.
“Viongozi wa Bunge wanafanya kazi nzuri ila huu ushabiki unaofanywa na ubabe usipodhibitiwa tutaliharibu. Nawaambia Watanzania ukiona mbunge anatumia muda mwingi bungeni kuliko jimboni, jibu ni moja tu, kumwondoa.”

CUF nayo yanena

Wakati Membe akisema hayo, Baraza Kuu la Chama cha Wananchi (CUF), limetoa tamko na kuonya kwamba mpasuko wa kisiasa ndani ya Serikali ya CCM, unaathiri na kuyumbisha nchi kikisema umesababisha makundi ambayo yanapambana kuwania nafasi ya kugombea urais ifikapo 2015.

Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba alisema hayo Dar es Salaam jana alipokuwa akieleza maazimio ya kikao cha Baraza Kuu la Uongozi wa Taifa la chama hicho ambayo yaliitaka Serikali ya CCM kuacha kuyumbisha nchi kwa kuangalia suala la urais 2015.

Profesa Lipumba alisema jukumu la msingi la chama kinachounda Serikali ni kufahamu kwamba nchi inahitaji mabadiliko ambayo yatawaletea maendeleo wananchi na huu si wakati wa kujadili nani anatakiwa kuwa Rais mwaka 2015, kwani hiyo ni njia ambayo inaweza kuwagawa Watanzania.

Bajeti bado tatizo
Kuhusu Bajeti ya Serikali, Profesa Lipumba alisema kikao cha Baraza Kuu kimebaini kuwa malengo ya Bajeti ya 2011/2012 hayakufikiwa kwani mfumuko wa bei umezidi kuongezeka tofauti na Serikali inavyoeleza kwamba umepungua.

“Takwimu zinaonyesha kwamba wakati Waziri wa Fedha anasoma hotuba ya Bajeti Juni, 2011 mfumuko wa bei ulikuwa asilimia 10.9 na uliongezeka hadi kufikia asilimia 20 na kwamba mwishoni mwa mwaka 2011, ulipungua kidogo hadi kufikia asilimia 18.2 lakini bado ni tatizo kwa wananchi kwani wanaendelea kuteseka na hali ngumu ya maisha kutokana na bei za bidhaa kuendelea kuwa juu,” alisema.

Alisema katika kukabiliana na upungufu wa umeme, Serikali iliahidi kukamilisha mradi wa kuzalisha umeme wa megawati 100 Dar es Salaam pamoja na megawati 60 Mwanza lakini mpaka sasa hakuna dalili yoyote ya kukamilika kwa miradi hiyo.

“Serikali ilisaini mkataba wa kupewa mkopo wa Euro 61 milioni na benki ya HSBC. Mkopo huo ulielekezwa kugharimia ujenzi wa mtambo wa kufua umeme wa megawati 60 Nyakato, Mwanza lakini cha kushangaza bajeti tano mfululizo zimekuwa zikitoa ahadi kama hizi bila utekelezaji,” alisema na kuongeza:

“Serikali ya CCM imeshindwa kutatua matatizo ya umeme na kuisababishia nchi kupata hasara na kudhoofisha uchumi.”
Akizungumzia ushiriki wa chama hicho katika uchaguzi wa marudio ya Ubunge katika Jimbo la Bububu, Zanzibar alisema CUF kimeridhia kushiriki kwani hiyo ni ngome yake kubwa na kimejipanga kushinda.

Imeandikwa na Elias Msuya, Aidan Mhando na Vicky Kimaro

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

HATUTOPAKI BASI DHIDI YA YANGA-MOKWENA

“PEMBA SALUTI KWENU” DK. NCHIMBI*

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA