WANACHOFUATA CHINA NYOTA WA AFRIKA

UMEWAHI kujiuliza, wachezaji mahiri kama Didier Drogba na Nicolas Anelka, wanafuata nini katika Ligi Kuu ya China? Je, ni fedha kukuza viwango vyao au kusaidia soka ya huko nayo ipate umaarufu kama ilivyo kwa nchi nyingine, hasa Ulaya.

Hivi karibuni, nyota wa kimataifa wa Ivory Coast, Drogba ametua klabu ya Shangai Shenhua, akitokea Chelsea ya England aliyoipa ubingwa wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Mbali ya Drogba, nyota wengine wa Afrika wakafuata nyayo akiwemo mshambuliaji wa kimataifa wa Nigeria, Yakubu Aiyegbeni, aliyejiunga na Guangzhou R&F kwa mkataba wa miaka mitatu.

Mwingine ni nyota wa kimataifa wa Mali, Frederic Kanoute, aliyetua Beijing Guoan FC kwa mkataba wa miaka miwili, akitokea Sevilla ya Hispania aliyoichezea kwa mafanikio makubwa.

Aidha, kuna Seydou Keita, nyota wa kimataifa wa Mali, aliyesaini mkataba wa miaka miwili na nusu klabu ya Dalian Aerbin inayocheza Super League ya nchini China.

Keita, ametimkia China akitokea FC Barcelona ya Hispania, aliyopata nayo mafanikio makubwa ya kutwaa jumla ya mataji 14 chini ya Kocha Pep Guardiola.

Kwame Ayew, nyota wa zamani wa kimataifa wa Ghana, aliyewahi kucheza Super League kati ya mwaka 2002 hadi 2006, kwa upande wake, anasema, ni vigumu kusema nyota hao wanafuata fedha tu, bali kucheza soka.

Msingi wa hoja yake umezingatia kuwa kwenye mkataba wa kila mchezaji, kuna kipengele cha kutemwa kama mchezaji husika hatakuwa na mchango uliotarajiwa, hivyo atapaswa kucheza soka ya nguvu.

Aidha, Kwame anasema, mbali ya nyota hao kupata fedha nyingi kupitia mikataba yao na klabu za China, pia wamekuwa msaada mkubwa kwa timu husika kupata umaarufu kwenye Ligi Kuu.

“China imekuwa ikitanuka kwa kiasi kikubwa barani Afrika, kupitia uwekezaji wake katika madini na maliasili,” anasema James Porteous wa Jarida la Morning Post la China ya Kusini na kuongeza: 

“Pengine klabu zimeamua kutumia nafasi ya soka, kupanua wigo wa soko la kibishara, pia kisiasa kati ya China na Afrika, ingawa hakuna ubishi, kinachowapeleka nyota wengi wa Afrika nchini China, ni maslahi.

Kwa mfano, klabu ya Guangzhou Evergrande inayomilikiwa na Evergrande Real Estate Group chini ya mwenyekiti wake, Xu Jiayin, huyu ni tajiri mkubwa nchini humo.

Ni mtu aliyewekeza kiasi cha kiasi cha dola mil. 70 za Marekani miaka kadhaa iliyopita.

Suala la mamilionea wa fedha kuwekeza kwenye klabu kwa lengo la kuwa na kikosi imara, ni utamaduni uliozoeleka katika nchi nyingi duniani, ikiwemo Ulaya.


Pengine kitu ambacho hakijawa wazi, ni dau ambalo hutolewa na klabu kuwanasa wachezaji hao nguli kwa klabu za Ligi Kuu ya China.

Hata hivyo, yaonekana wachezaji hao wamekuwa wakivuna fedha nyingi kupitia mikataba yao.

Kwa upande wake, Kocha Marcello Lippi wa timu ya Guangzhou Evergrande, aliyeipa Italia ubingwa wa Kombe la Dunia mwaka 2006, amekuwa akilipwa mshahara wa dola mil. 16 za Marekani kwa mwaka.

Aidha, kuna habari kuwa, Drogba analipwa mshahara wa dola 350,000 za Marekani kwa wiki, huku Yakubu akitia kibindoni dola 150,000 kwa wiki.

Mshambuliaji wa zamani wa Ghana, Kwame anayecheza soka nchini China kwa miaka minne sasa, haijulikani analipwa kiasi gani haswa, kama Drogba na Kanoute wenye umri wa miaka 34, wakilipwa kiasi hicho.

Porteus anasema, ingawa hawafahamu vizuri nyota hao, lakini kwa fedha wanazolipwa kwa siku, kitakuwa kichocheo kwao cha kujituma zaidi dimbani kuzisaidia timu wanazochezea.

Yakubu anasema, kilichompeleka China si fedha bali soka, hasa baada ya kuifahamu mipango ya klabu hiyo ya Guangzhou R&F.

“Tangu Anelka atue Shanghai Shenhua akitokea Chelsea, nyota wengi mahiri wamefuata nyayo zake China, na ujio wetu unaweza kusaidia kuboresha kiwango cha soka cha China.”

Aidha, uwepo wa nyota kadhaa maarufu katika Super League, utaongeza idadi ya mashabiki katika mechi tofauti na ilivyokuwa hapo awali.

Kwa mfano, timu ya Shanghai Shenshua ilikuwa ikiingiza mashabiki takriban 10,000 katika uwanja wake wa Hongkou.

Nyota wa zamani wa Ghana, Kwame, aliyecheza soka nchini China kati ya 2002 na 2006, anasema ni kitu kizuri kuona nyota mahiri wakijiunga na klabu za Super League.

“Najisikia fahari sana, mimi nilikuwa wa kwanza kucheza soka China. Leo hii kuona wachezaji kama Drogba na Anelka wanakwenda kule (China), ni kitu cha kufurahisha,” anasema Ayew.

“Kwenda China si kufuata fedha tu, ni nchi yenye tofauti kabisa, ikiwa na utamaduni wa aina yake. Si kwamba hawajui soka, wanataka kukuza na kuitangaza soka yao kimataifa.

“Utake usitake, China ni kati ya nchi zenye uchumi mzuri, sasa kwa nini isiwe hivyo kwenye soka? Hiki ndicho kinachowafanya wachezaji wengi mahiri kukubali kujiunga na Super League ya China.”
Hata hivyo, Ayew, mdogo wa aliyewahi kuwa nyota bora wa Afrika, Abeid Pele, anasema tatizo kubwa la nchini China, ni uchache wa wachezaji na makocha kutoka Afrika na Ulaya.

Kwame aliyewahi kuwa mfungaji bora wa Super League mwaka 2004, anasema, kwa mazingira hayo si rahisi mchezaji akaenda China kuvuna fedha tu, isipokuwa pia kusaidia timu kupitia uwezo na uzoefu wake katika mchezo huo.Chanzo;Tanzania Daima

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

HATUTOPAKI BASI DHIDI YA YANGA-MOKWENA

“PEMBA SALUTI KWENU” DK. NCHIMBI*

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA