WATAKA NYUMBA ZA SERIKALI ZILIZOUZWA ZIREJESHWE

MGOGORO wa uuzwaji wa nyumba za Serikali limeibuka bungeni ambapo baadhi ya wabunge wametaka nyumba hizo zirejeshwe Serikalini.Katika swali la msingi, Mbunge wa Mbulu, Mustapha Akunay (Chadema), alihoji akitaka kujua hatua zilizochukuliwa kwa kuwa nyumba zilizouzwa zilikuwa katika maeneo muhimu yakiambatana na sehemu kubwa ya ardhi.

Mbunge huyo alisema wapo watu ambao waliuziwa nyumba pamoja na maeneo yake bila ya Serikali kujua kuwa maeneo hayo yalikuwa ni makubwa zaidi akitoa mfano kwamba wapo waliouziwa nyumba na eneo lake la kuanzia ekari moja hadi sita na maeneo hayo yapo mjini.


Alihoji ni kwa nini Serikali iliuza nyumba pamoja na maeneo hayo ambayo ni makubwa kiasi cha kuifanya Serikali kushindwa kupanga mipango ya maendeleo mingine tena.


Akunay pia alitaka uamuzi wa kuuza nyumba za Serikali kwa watumishi waliokuwa wakiishi katika nyumba hizo, upitiwe upya ili kurejesha nyumba hizo Serikalini.


Kwa upande wake, Mbunge wa Viti Maalum, Magdalena Sakaya (Chadema), alisema nyumba hizi ziliuzwa kwa bei ya kutupwa hivyo ni lazima zirudishwe Serikalini ili watanzania wote wanufaike.


Akijibu maswali hayo, Naibu Waziri wa Ujenzi Gerson Lwenge alisema Serikali haiwezi na haina mpango wa kuwanyang’anya nyumba wale wote walionunua.


Lwenge alisema kuwa uuzwaji wa nyumba hizo ulikwenda pamoja na uuzwaji wa viwanja vyake na hata maeneo yanayolalamikiwa na wabunge ni mali ya walionunua nyumba.


Kwa mujibu wa Lwenge, uamuzi wa kuuzwa kwa nyumba hizo ulijadiliwa na Bunge na kupitishwa kwa hiyo iwapo wabunge wanataka uamuzi huo ubatilishwe ni vema wakatafuta namna ya kuliingiza jambo hilo tena.


“Aliyejkuwa mbunge wa Vunjo, Aloyce Kimaro alileta hoja binafsi mwaka 2008 na Bunge hili lilijadili kwa kina na kufikia muafaka wa kuziacha nyumba hizo kwa wanunuzi, hivyo nasema bado wanunuzi hao wana haki juu ya nyumba na maeneo yake,’’ alisema Lwenge.


Alisema lengo la Serikali kuuza nyumba ilikuwa ni kupunguza gharama za kuhudumia nyumba zilizokuwa za siku nyingi na kuwawezesha watumishi waliotumikia Serikali kuishi nyumba bora.


“Zoezi la kuuza nyumba hizo lilifanyika baadaya ya uchambuzi wa kina uliojumuisha kuangalia uzoefu wa nchi nyingine, Serikali iliunda tume ambazo zilitoa ushauri wa kitaalamu kuhusu namna bora ya kupunguza tatizo la nyumba Serikalini.


Hata hivyo, Naibu Waziri aliwataka wabunge kutumia kanuni na miongozo kama wanataka kuleta jambo hilo tena ili kulirejesha kwa utaratibu mwingine.


Lwenge alisema Serikali kupitia Wakala wa Majengo (TBA) itaendelea kujenga nyumba nyingine katika mikoa yote na Wilaya zake kwa kutumia fedha inayopatikana kutokana na mauzo ya nyumba na mikopo toka kwenye mabenki mbalimbali.


Alitaja idadi ya majengo yaliyo chini ya TBA ni 2,713 na katika hayo, nyumba 1353 zimepangishwa kibiashara, nyumba 748 zimepangishwa watumishi wa umma, nyumba 416 zinakaa viongozi, nyumba 103 ni za wageni, Ikulu ndogo 37 na majengo ya ofisi 56.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

KOCHA BENCHIKHA AMESEPA

MASHUSHUSHU WA MAMELODI WALIKUJA KUTUPELELEZA: HERSI