Zitto ataja wizi kampuni za simu

MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto (CHADEMA), amesema Kampuni ya mtandao ya Onmobile inashirikiana na makamupni ya simu za mikononi kuwanyonya wasanii kwa kuwalipa asilimia ndogo ya mapato yanayotokana na matumizi ya nyimbo zao.

Akichangia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia iliyosomwa bungeni mjini Dodoma jana, Zitto alisema kinachoshangaza kampuni hiyo iliyohodhi mambo yote ya kampuni za Vodacom na Airtel, inafanya kazi bila leseni.

“Ukimpigia simu Waziri Mkuu… utasikia simu yake ina wimbo wa Rose Mhando, Naibu Waziri Adam Malima yeye upo wimbo wa Dar mpaka Moro wa Wanaume Familly na ukinipigia mimi utasikia Kurani ama wimbo wa CHADEMA.

“Lakini kinachoshangaza wasanii hawa wananyonywa licha ya nyimbo zao kutumika, tunadhani wasanii wanapata… si kweli kwani hata vituo vya redio na televisheni vya serikali vinatumia nyimbo hizi bila kuwalipa chochote.

Makampuni makubwa ya Vodacom na Airtel wameingia mkataba na Onmobile na wanaingiza sh bilioni 43 kutokana na milio,” alisema mbunge huyo aliyeonyesha nia ya kuutaka urais mwaka 2015 kupitia chama chake.

Zitto alifafanua kuwa katika mapato hayo Onmobile anachukua mgawo wa asilimia 80, mawakala wa kati asilimia 13 na wasanii wanaambulia asilimia saba pekee, jambo alilodai kwamba halikubaliki.

Pia alisema kampuni hiyo inayofanya shughuli za mtandao wa kuingiza milio ya nyimbo kwenye simu haina wafanyakazi wa kueleweka wala ofisi maalumu.

Kwa mujibu wa Zitto, ofisi za kampuni hiyo zipo ndani ya Vodacom na Airtel na wanaofanya kazi ni watu wawili.

“Mheshimiwa Mwenyekiti ukiona vijana wetu wanavyohangaika kutayarisha miziki yao halafu bado hawalipwi mrabaha kwamba kampuni inayofanya kazi ya networking ndiyo inapata asilimia 80, si jambo la haki,” alisema.

Mbunge huyo alibainisha kwamba alipata kuzungumza na Naibu Waziri wa wizara hiyo January Makamba na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) akiwaeleza ujanja huo wa makampuni ya simu kutoingia mikataba na wasanii badala yake yanawatumia mawakala.

“Mheshimiwa Makamba tulikaa nikakweleza na leo narudia ili tusaidie vijana wetu maana hata wewe ni kijana. Wabunge tukubaliane hapa kuwa katika hii mikataba wasanii wetu wapate asilimia 50,” alisema.

Mbunge huyo aliitahadharidha serikali kuwa isiogope kuichukulia hatua kampuni hiyo kwa kisingizio kuwa mikataba itawafunga, akifafanua kwamba iwapo Kampuni ya Onmobile iliweza kuja nchini kufanya kazi bila leseni ni wazi kuwa inapaswa kuchukuliwa hatu kwa kuikosesha serikali mapato.

Aliitaka serikali kulitumia Shirika la Posta kuuza kazi za wasanii kwa kuwa liko kila sehemu nchi nzima na linaaminika.

Baadhi ya wabunge waliochangia hotuba hiyo kutoka Viti Maalumu ni Leticia Nyerere (CHADEMA), Riziki Omary Juma na Raya Ibrahim Khamis (CUF), mwingine ni Mbunge wa Mkanyageni, Habib Mnyaa (CUF) walioitaka serikali kutunga sheria ya kudhibiti mitandao ya internet na kijamii ili kuzuia matumizi mabaya yanayofanyika sasa.

Pia walitaka serikali kueleza kiasi kinachopatikana kutoka kwenye makampuni ya simu kwani hupata faida kubwa kuliko mapato wanayolipa serikalini.

Wabunge hao pia waliitaka TCRA kuyachukulia hatua makampuni ya simu yanayowasumbua wateja kwa kuwapigia simu za matangazo kila wakati na kuwatoza malipo kwa huduma wasizozihitaji.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KOCHA BENCHIKHA AMESEPA

MASHUSHUSHU WA MAMELODI WALIKUJA KUTUPELELEZA: HERSI

KOCHA WA AL.AHLY ASEMA YANGA NI TIMU BORA NA NGUMU