Chenge kumtetea Mramba kesi ya ufisadi

Tausi Ally
WAZIRI wa zamani wa Fedha, Basil Mramba ameanza kujitetea katika kesi ya matumizi mabaya ya ofisi za umma na kuisababishia Serikali hasara ya Sh11.7 bilioni huku akiwataja mashahidi sita akiwamo aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Andrew Chenge kuwa mashahidi wake.

Mashahidi wengine watakaomtetea Mramba katika kesi hiyo, ni Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Mwakilishi wa Kampuni ya M/S Alex Stewart Government Business Assayers, Erwine Florence, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali, John Cheyo na Mtaalamu wa Ushauri wa Masuala ya Kodi, Florian Msigala.

Baada ya kutaja idadi hiyo ya mashahidi, Mramba aliliambia jopo linaloongozwa na Jaji John Utamwa akisaidiwa na Jaji Sam Rumanyika, Msajili Sauli Kinemela kuwa shahidi wa sita ambaye wanatarajia kumwita, bado hajathibitisha kama atakwenda kutoa ushahidi au la.

Mramba alieleza kuwa kati ya mashahidi hao anaotarajia kuwaita kumtetea, watatu watawasilisha nyaraka na wengine watafika mahakamani.

Licha ya kuwataja mashahidi hao, Mramba aliiambia Mahakama kuwa atatoa utetezi wake kwa njia ya kiapo.

Mbali na Mramba, Waziri wa zamani wa Nishati na Madini, Daniel Yona na Katibu Mkuu wa zamani wa Wizara ya Fedha, Gray Mgonja nao wameiambia Mahakama kuwa na wenyewe watajitetea kwa njia ya kiapo na pia watatetewa na mashahidi hao.

Lakini Mgonja aliongeza shahidi mwingine aliyemtaja kwa jina moja la Karisti.
Baada ya kutoa taarifa hiyo, Mramba alianza kujitetea na Wakili wake Hurbert Nyange alimtaka aieleze Mahakama chimbuko la kesi inayomkabili.

Mramba alisema ana umri wa miaka 71. Alidai kuwa chimbuko la kesi hiyo ni malalamiko yaliyokuwapo bungeni kwa wananchi na kwenye vyombo vya habari kuwa ingawa Tanzania ina migodi kadhaa ya dhahabu, haijafaidika kwa sababu migodi hiyo ilikuwa inaiibia Serikali na kuidanganya juu ya uzalishaji na uuzaji wa madini hayo nje ya nchi.

Alidai kuwa kutokana na malalamiko hayo, Serikali ilibidi kuchukua hatua ya kujibu hoja hizo zilizojitokeza katika jamii. Hivyo iliileta kampuni ya Alex Stewart Government Business Assayers kukagua migodi hiyo ili Serikali ipate maelezo juu ya malalamiko ya wananchi.
Mramba aliendelea kueleza kuwa Serikali iliiteua BoT ifanye kazi ya kutafuta kampuni inayoweza kufanya kazi hiyo kwa niaba yake na ikafanya hivyo kwa kuingia mkataba na kampuni iliyochaguliwa ya Alex Stewart Government Business Assayers.

“Kampuni ya Alex Stewart Government Business Assayers ni kampuni ambayo ipo katika kundi la kampuni za Alex Group ambazo makao makuu yake yapo nchini Uingereza, lakini kampuni hiyo ya Alex Stewart Government Business Assayers makao makuu yake yapo nchini Marekani,” alisema Mramba.

Alidai kuwa aliyeagiza BoT kufanya kazi hiyo ya kumtafuta mkaguzi wa dhahabu ni Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa na kwamba wakati huo yeye akiwa Waziri wa Fedha alipewa jukumu la kuhakikisha gharama za kumlipa mkaguzi huyo zinapatikana ndani ya Serikali, BoT au popote.

Alidai kuwa kati yake na Gavana, hakuna aliyekuwa na mamlaka juu ya mwingine na kwamba Gavana alikuwa na wajibu wa kufanya mchakato wa kumtafuta mkaguzi wa dhahabu.
Mramba alisisitiza kuwa yeye hakuhusika kwenye mchakato huo kwa kumtafuta wala kumleta hapa nchini wala kumtuma mwakilishi yeyote kumwakilisha kwenye kamati iliyoteuliwa kufanya mchakato huo, bali alipewa agizo la kumlipa.

“Mimi kama waziri sikuwa na mtu wangu kwenye ile kamati lakini Wizara ilituma mwakilishi, ambaye alikuwa Mwanasheria Bethar Soka wakati wa kuhoji kampuni mbili ili wachague na kwenye kujadili vipengele vya mkataba,” alisema Mramba wakati akitoa utetezi wake.

Mramba alidai kuwa katika mchakato huo, Bethar aliwahi kuandika barua TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania) akiomba ushauri juu ya kipengele kilichopo kwenye mkataba huo kinachotoa msamaha wa kodi.
Baada ya Mramba kueleza hayo, Nyange aliiomba Mahakama imruhusu kuzungumza na mteja wake, Jaji Utamwa alimruhusu. Hata hivyo, mazungumzo yao yalikuwa ya kunong’ona kitendo ambacho kilimfanya Wakili Mkuu wa Serikali, Fredrick Manyanda kupinga akiomba wazungumze kwa sauti ili na wao wasikie.

Manyanda baada ya kutoa pingamizi hilo, Nyange alisema kwa sauti kuwa alikuwa akimwambia mteja wake aache kuzungumza juu ya mambo aliyoyasikia na yale asiyoyajua, bali azungumze kile ambacho anakifahamu.

Kutokana na hoja hiyo, Mramba alidai kuwa wakati Bethar akiwa kwenye kamati (timu) hiyo, yeye hakuwapo wala hakujua alichoagizwa na kwamba hakuwahi kumpa mfanyakazi wake maagizo yoyote kwenye kamati hiyo na hajui Wizara ya Fedha ilikuwa na mamlaka gani kwenye makubaliano.

Mramba aliongeza kudai kuwa BoT katika kusimamia uchumi, ndiyo yenye wajibu wa kumshauri Waziri wa Fedha, lakini Waziri wa Fedha hawezi kuishauri BoT au Gavana.

Alibainisha kuwa mkataba kati ya Kampuni ya Alex Stewart Government Business Assayers na Serikali, ulisainiwa na aliyekuwa Gavana wa BoT, hayati Daud Balali na Makamu wa Rais wa kampuni hiyo, Erwine Frorence.

Alidai kuwa Gavana alisaini kutokana na mamlaka aliyokuwa nayo pamoja na agizo la Rais.
Akimhoji Mramba Wakili Nyange alisema: “Inasemekana kama isingekuwa wewe Gavana asingesaini huo mkataba.”

Mramba alijibu: “Mimi sikumwambia Gavana asaini, nilimwambia afungue mkataba na siyo asaini mkataba.”

Mramba alidai kuwa tangu mwanzo, Gavana mwenyewe aliomba asaini, lakini yeye na Waziri wa Nishati na Madini baada ya kujadili na kukubaliana, walimtaka afungue mkataba ili baadhi ya vitu fulani vianze kushughulikiwa ili hatimaye asaini na utekelezwe... “Nilimwambia don’t sign (usisaini) nikampa na sababu.”

Jaji Utamwa ameiahirisha kesi hiyo hadi leo saa 7:00 mchana Mramba atakapoendelea kutoa utetezi wake.

Mramba, Yona na Mgonja walifikishwa mahakamani mwaka 2008. Inadaiwa kuwa, kati ya Agosti, 2002 na Juni 14, 2004, Dar es Salaam, washtakiwa wakiwa watumishi wa umma, walitumia vibaya madaraka yao na kuisababishia Serikali hasara ya Sh11.7 bilioni.
Ilidaiwa kuwa washtakiwa hao waliipatia msamaha wa kodi isivyo halali, Kampuni ya M/S Alex Stewart ya Uingereza. Chanzo;Mwananchi

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

KOCHA BENCHIKHA AMESEPA

MASHUSHUSHU WA MAMELODI WALIKUJA KUTUPELELEZA: HERSI