KOCHA MPYA WA AZAM FC ATAMBULISHWA RASMI LEO

 Makamu Mwenyekiti wa timu ya soka ya Azam, Said Mohammed (kushoto), akimtambulisha kwa waandishi wa habari, Kocha mpya wa timu hiyo, Boris Bunjak aktika mkutano uliofanyika, Dar es Salaam leo. (PICHA NA RICHARD MWAIKENDA)
                                             Kocha Bunjak akifurahi baada ya kutambulishwa
               Mwenyekiti wa timu hiyo akizungumza na waandishi wa habari
                                           Munjak akizungumza na waandishi wa habari


Habari na Mahmoud Zubeiry wa Blog ya BIN ZUBEIRY
AZAM FC, washindi wa Medali tatu za Fedha, Ligi Kuu msimu uliopita, Kombe la Urafiki na Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, leo wamemtambulisha kocha wao mpya kutoka Serbia, Boris Bunjak ambaye atarithi mikoba ya Muingereza Stewart Hall aliyefukuzwa wiki iliyopita.
Mwenyekiti wa Azam FC, amewaambia Waandishi wa Habari leo mchana kwamba, wameingia mkataba wa miaka miwili na Bunjak, ambaye anatua katika klabu hiyo kwa msaada wa kocha wa Simba, Milovan Cirkock ambaye alimuunganisha na wamiliki wa klabu hiyo.
Bunjak mwenye leseni ya Shirikisho la Soka Ulaya (UEFA), anatua Azam, akitokea FC Damac ya Saudia Arabia aliyoanza kuifundisha mwaka jana na kabla ya hapo alifunisha klabu za kibao, zikiwemo FK Sloga Kraljevo, FK Javor Ivanjica, Crvena Zvezda Gnjilane, FK Radnicki Nis, FC Uralan Elista, FK Mladi Radnik, FK Crvena Zvezda Beograd, Al-Shaab, FK Hajduk Kula na Al-Nasr.
Awali, Bunjak aliyezaliwa Novemba 17, mwaka 1954 ( miaka 57), alicheza soka katika klabu za FK Sloga (Kraljevo), FK Vozdovac (Beograd), FK Radnicki (Kragujevac), FK Olimpia (Ljubljana), FK Sumadija (Arandjelovac), FK Sloga (Kraljevo), FK Borac (Cacak) na FK Sloga (Kraljevo).
Kwa kuajiriwa kocha huyo, Vivek Nagul kutoka India, aliyekuwa anakaimu nafasi ya Stewart, ambaye aliletwa na Muingereza huyo anarejea kwenye majukumu ya kufundisha timu za vijana, wakati Kocha Msaidizi ataendelea kuwa Kali Ongala.
Stewart kabla ya kuja Tanzania mwaka juzi, akianza kufundisha timu ya taifa ya Zanzibar, aliwahi kufanya kazi India kwa miaka miwili.
Akiwa India ndipo alikutana na Vivek na wakafanya naye kazi pamoja na akaridhishwa na utendaji wake, hasa katika eneo la vijana na ndio maana alipotua Azam FC akamleta aje kumsaidia katika eneo hilo.
Vivek amekuwa Kocha Mkuu wa Azam Academy tangu mwaka jana, akisaidiwa na Iddi Cheche na Philipo Alando.
Stewart alifukuzwa Jumatano iliyopita kwa kosa la kukaidi maagizo ya Bodi ya Ukurugenzi ya klabu hiyo, kumpanga Mrisho Khalfan Ngassa katika mechi ya fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame dhidi ya Yanga.
Kikao cha Jumatano hiyo pamoja baina ya Bodi ya Ukurugenzi ya Azam FC, Mwanasheria wa kampuni na kocha Stewart kiliafiki kuvunjwa kwa ndoa hiyo na Azam FC ikawa chini ya Nagul, akisaidiwa na Kali Ongala.
Baada ya mechi ya Nusu Fainali ya Kagame, kati ya Azam na AS Vita ya DRC, Stewart aliitwa na kuambiwa asimtumie tena Ngassa kwa kitendo cha mchezaji huyo kwenda kuibusu na kuivaa jezi ya Yanga, baada ya kufunga bao la ushindi. Ngassa ameuzwa Simba SC, baada ya sakata hilo.
Lakini Stewart katika kikao hicho, kwanza alimtetea Ngassa kutokana na kufunga bao la ushindi na kumuelezea kama mchezaji muhimu kwake, lakini msimamo wa bodi ulikuwa ni asipangwe tena.
Katika fainali, Stewart alimvalisha jezi Ngassa akamuanzishia benchi, lakini kama ilivyokuwa kwenye Nusu Fainali alimuingiza kipindi cha pili timu ikiwa nyuma kwa 1-0 na mwisho wa mchezo ikashinda 2-1 yeye akifunga la pili, dhidi ya Yanga pia alimuingiza timu ikiwa nyuma kwa 1-0.
Lakini Ngassa alishindwa kurudia kile alichofanya kwenye mechi na AS Vita na Yanga ikashinda 2-0.
Mserbia huyo anakuwa kocha wa tano Azam, ndani ya miaka minne tangu ianze kucheza Ligi Kuu, 2008 baada ya Stewart, Mbrazil Neider dos Santos, Sylvester Marsh na Itamar Amorin, Mbrazil mwingine.
Lakini ni Stewart angalau anaacha kumbukumbu ya taji na Medali Azam, baada ya kuiwezesha kutwaa Kombe la Mapinduzi Januari, kushika nafasi ya pili katika Ligi Kuu Aprili, kabla ya kushika nafasi ya pili Kombe la Urafiki na Kagame mwezi uliopita.
Stewart ana sifa ya kutokuwa mbinafsi na mwenye kuwaamini watu wa chini yake, kwa mfano namna ambavyo amekuwa akimpromoti Kali Ongala. Alimkuta Kali kama mchezaji, lakini kwa sababu ya umri kumtupa mkono, akashauriana naye awe Kocha Msaidizi na mshambuliaji huyo wa zamani wa Yanga, akakubali.
Chini ya Stewart, Kali alikuwa akiachiwa timu aiongoze ili kumjengea kujiamini zaidi na mwezi uliopita aliachiwa timu kwenye Kombe la Urafiki, akaifikisha fainali, ambako ilifungwa na Simba kwa penalti kufuatia sare ya 2-2 ndani ya dakika 90.
Wachezaji wa Azam na makocha wapya wa klabu hiyo, pamoja na baadhi ya maofisa wa klabu hiyo, waliangua vilio, wakati wakimuaga Stewart.
Wachezaji walioongoza kwa kilio Uwanja wa Chamazi Ijumaa iliyopita, ni Luckson Kakolaki, Ibrahim Mwaipopo, Ramadhan Chombo ‘Redondo’, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Hajji Nuhu na Erasto Nyoni, wakati kwa maofisa, aliyeongoza ni Vivek Nagul.
Stewart mwenyewe pia alibubujikwa machozi wakati anaagana na familia yake, aliyoishi nayo kwa zaidi ya mwaka kwa furaha, amani, upendo na mafanikio.

WASIFU WA BORIS BUNJAK:
JINA KAMILI: Boris Bunjak
KUZALIWA: Novemba 17, 1954 (Miaka 57)
KLABU ALIZOCHEZEA:
1967- 1975: FK Sloga (Kraljevo)
1975- 1978 FK Vozdovac (Beograd)
1978- 1979 FK Radnicki (Kragujevac)
1979- 1980 FK Olimpia (Ljubljana)
1980- 1981 FK Sumadija (Arandjelovac)
1981- 1985 FK Sloga (Kraljevo)
1985- 1986 FK Borac (Cacak)
1986- 1990 FK Sloga (Kraljevo)

KLABU ALIZOFUNDISHA:
1990-1993: FK Sloga (Kraljevo)
1995-1996: FK Javor (Ivanjica)
1996-1997: Crvena Zvezda (Gnjilane)
1999: FK Radnicki (Nis)
2000: FC Uralan Elista (Urusi)
2000-2002: FK Mladi (Radnik)
2002-2004: FK Crvena Zvezda (Beograd)
2004: Al-Shaab (UAE)
2005: FK Hajduk (Kula)
2006-2007: Al-Nasr (Oman)
2009: Al Oruba Sur (Oman)
2011: FC Damac (Saudi Arabia)
2011: AL NASER (Oman)

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

KOCHA BENCHIKHA AMESEPA

MASHUSHUSHU WA MAMELODI WALIKUJA KUTUPELELEZA: HERSI