Misaada zaidi inahitajika kupambana na madawa ya kulevya sambamba na kupunguza maambukizi ya virusi vya Ukimwi Zanzibar.

Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Dr. Omar Dadi Shajak akisalimiana na wataalamu kutoka taasisi ya Pangaea ya Marekani waliofika ofisini kwake Migombani. Kutoka kushoto ni Bw. Douglas Bruce na Barrot Lambdin.
  Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Dr. Omar Dadi Shajak akizungumza na wataalamu kutoka taasisi ya Pangaea ya Marekani waliofika ofisini kwake Migombani
  Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Dr. Omar Dadi Shajak akizungumza na wataalamu kutoka taasisi ya Pangaea ya Marekani waliofika ofisini kwake Migombani. Kutoka kushoto ni Bw. Douglas Bruce na Barrot Lambdin.
Mkurugenzi wa Tume ya kuratibu na udhibiti wa dawa za kulevya Zanzibar Bwana Ahmed Salim Awadh akifafanua jambo katika kikao kilichowajumuisha wataalamu kutoka taasisi ya Pangaea ya Marekani kilichofanyika ofisini kwa Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Migombani. Picha na Salmin Said Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais
--
 Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Dr. Omar Dadi Shajak amesema mikakati na misaada zaidi inahitajika katika kupambana na uingizaji wa dawa za kulevya, sambamba na kupunguza maambukizi ya virusi vya Ukimwi Zanzibar. 

 Amesema Zanzibar ambayo ni nchi ya visiwa, itaweza kudhibiti uingizaji na utumiaji wa dawa kulevya iwapo kutakuwa na mikakati imara na uungwaji mkono kutoka taasisi za ndani na nje ya nchi 

 Dr. Shajak ametoa kauli hiyo Ofisini kwake Migombani alipokuwa na mazungumzo na wataalamu wa taasisi ya Pangaea ya nchini Marekani inayojishughulisha na utoaji wa huduma mbali mbali za kiafya zikiwemo za ushauri na tiba kwa watumiaji wa dawa za kulevya na kupunguza maambukizi ya virusi vya Ukimwi. 

Amesema taasisi hiyo ambayo inafanya kazi kwa karibu na kituo cha kudhibiti maradhi mbali mbali nchini Tanzania (CDC), ni vyema ikafikiria namna ya kuleta huduma zao hapa Zanzibar, ili kusaidia kupunguza maambukizi ya Ukimwi hasa kwa makundi hatarishi yakiwemo ya watumiaji wa dawa za kulevya.

Amesema Zanzibar imekuwa ikichukua juhudi mbali mbali za kudhibiti uingizaji na utumiaji wa dawa za kulevya, ikiwa ni pamoja na kuimarisha ulinzi, sambamba na kuanzishwa kwa Sober houses ambazo zimekuwa zikiwasaida vijana walioamua kuachana na matumizi ya dawa hizo. 

 Kwa upande wake wao wataalamu hao kutoka taasisi ya Pangaea ya Marekani wamesema mapambano dhidi ya dawa za kulevya ni muhimu katika kukabiliana na maradhi mbali mbali yakiwemo Ukimwi. Wamesema taasisi hiyo imeanza kupata mafanikio makubwa kwa upande wa Tanzania Bara ambapo wamekuwa wakisaidia kutoa ushauri na dawa za Methadone ambazo huwasaidia watumiaji wa dawa za kulevya kwa kujidunga sindano kuweza kupunguza athari za dawa hizo. 

 Wamesema kufika kwao Zanzibar ni hatua ya matayarisho ya awali ya kuweza kufikisha huduma hizo hapa nchini, na kwamba hatua nyingine zaidi zitafuata katika kuhakikisha kuwa Zanzibar inanufaika na huduma hizo zikiwemo utoaji wa tiba ya Methadone kwa watumiaji wa dawa za kulevya. 

 Mapema akitoa ufafanuzi kuhusiana na mradi huo, Mkurugenzi wa Tume ya kuratibu ya udhibiti wa dawa za kulevya Zanzibar Bwana Ahmed Salim Awadh amesema tayari zipo program mbali mbali zinazolenga kuwafikia moja kwa moja watumiaji wa dawa za kulevya, ili kupunguza athari kwa watumiaji hao. 

 Amesema tume yake kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, inakusudia kushirikiana na taasisti hiyo ya Pangaea ya Marekani ili kuhakikisha kuwa watumiaji wa dawa za kulevya na waathirika wa Ukimwi wanapatiwa tiba mbadala na kuweza kupunguza athari zitokanazo na majanga hayo. 

 Mkurugenzi huyo amesema kwa sasa wanajiandaa kuupokea mradi huo, na kwamba hatua za awali zitakuwa ni kuwaandaa watoaji wa huduma ili kuwapa taaluma na kuweza kuwafikia walengwa kwa urahisi.
 Na
 Hassan Hamad 
Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA

DKT NCHIMBI ASHIRIKI MAZISHI YA ASKOFU.GACHUMA WA KANISA LA NLGCC

π™‚π˜Όπ™ˆπ™Šπ™‰π˜Ώπ™„ π™†π˜Όπ˜Ύπ™ƒπ™€π™•π˜Ό π™†π™„π˜½π™„π™‰π™‚π™’π˜Ό.