WAKUU WA MAJESHI YA POLISI WA NCHI ZA SADC KUKUTANA ZANZIBAR

IGP Said Mwema mwenyeji wa mkutano huo.
Na Mohammed Mhina, wa Jeshi la Polisi Zanzibar

Wakuu wa Majeshi ya Polisi kutoka nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika SADC-SARPCCO, watakutana mjini Zanzibar Tanzania, kujadili na kuweka mikakati ya pamoja itakayosaidia kukabiliana na uhalifu wa kiamataifa ukiwemo ule unaovuka mipaka.
 
Mratibu wa maandalizi ya mkutano huo ambaye pia ni Mkuu wa Kitengo cha Shirikisho la Polisi wa Kimataifa Duniani  (INTERPOL) nchini Tanzania, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Gustavus Babile, amesema kuwa mkutano huo wa siku tatu ambao utafanyika mwanzoni mwa mwezi ujao, utatanguliwa na mikutano mingine midogo midogo ya kamati tendaji (Technical Organs)  kutoka nchi wanachama.

Kamanda Babile amesema maandalizi ya mkutano huo utakaoanza Septemba 3 hadi 5, mwaka huu, yapo katika hatua za mwisho na kwamba tayari Wakuu wa Majeshi ya Polisi kutoka nchi 11 kati ya 14 wanachama wa Shirikisho hilo la Wakuu wa Majeshi ya Polisi kwa nchi za Kusini mwa Afrika yaani Southern African Region Police Chiefs Co-Opereratio Organization (SARPCCO) wamethibitisha kushiriki.

Amesema Wakuu wa Majeshi ya Polisi waliothibisha kushiriki katika mkutano huo ni kutoka Afrika ya Kusini, Botswana, Namibia, Swaziland, Lesotho, Malawi, Msumbiji, Congo DRC, Zambia, Zimbabwe na wenyeji Tanzania.

Amesema Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Angola Kamishna Jenerali Ferire Do Santos Ambrosio De Lemos, atatuma mwakilishi kwenye mkutano huo kutokana na nchi hiyo kukabiliwa na uchaguzi mkuu wa vyama vingi ambao utafanyika katika siku za hivi karibuni.

Kamanda Babile amesema ofisi yake bado inaendelea kuwasiliana na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Mauritius, Kamishna Jenerali Rampersad Dhun ili kuthibitisha ushiriki wake yeye pamoja na wajumbe wengine wanaopaswa kuwepo kwenye mkutano huo.

Mbali ya Wakuu hao wa Majeshi ya Polisi kutoka nchi za SADC, pia Kamanda Babile amewataja Wajumbe wengine wanaopaswa kuwepo kwenye mkutano huo kuwa ni pamoja na Wakurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai kutoka nchi wanachama ambao nao watawaongoza Wataalamu Viongozi katika Vitengo mbalimbali vya Majeshi hayo ya Polisi kutoka katika nchi shiriki.

Wataalamu hao ni pamoja na Wakuu wa Vitengo vya Sheria, Wakuu wa Mafunzo, Wakuu wa Mitandao ya Wanawake, Wakuu wa Maabara ya Uchunguzi wa Vielelezo, Wakuu wa Udhibiti wa Silaha  ndogondogo na za rashasha, Wakuu wa Vikosi vya Afya na Utabibu, Wakuu wa Mifumo ya Kompyuta pamoja na Wakuu wa Vitengo vya Interpol kutoka kila nchi wanachama.

Amesema, pamoja na mambo mengine, wajumbe wa mkutano huo pia watajadili, kubadilishana uzoefu wa kiutendaji na hatimaye mbinu na mikakati ya pamoja itakayosaidia kukabiliana na makosa yenye athali kwa maisha ya binadamu na yale yanayodhoofisha nguvu za kiuchumi kwa nchi za Kiafrika na duniani kwa ujumla.

Ameyataja makosa hayo kuwa ni pamoja na Ugaidi, Uharamia, Usafirishaji haramu wa binadamu, Biashara haramu ya Madawa ya kulevya, makosa ambayo amesema yana athali za moja kwa moja kwa binadamu.
 
Ameyataja baadhi ya Makosa yanayothoofisha nguvu za kiuchumi Duniani ambayo pia yatajadiliwa kwenye mkutano huo kuwa ni ya hujuma na wizi wa fedha kutoka kwenye mabenki na taasisi nyingine za kifedha unaofanywa kwa kutumia mifumo huru ya kompyuta.

Makosa mengine ni ya wizi na usafirishaji wa magari na mifugo kutoka nchi moja kwenda nyingine kwa magendo pamoja  na uwekezaji wa miradi mikubwa ya kiuchumi itokanayo na fedha za biashara haramu.
 
Hata hivyo, Kamnda Babile ameyataja mambo mengine yatakayofanyika wakati wa mkutano huo kuwa ni pamoja na uchaguzi wa Mwenyekiti mpya wa Shirikisho hilo la SARPCCO ambapo Mkuu wa Jeshi la Polisi hapa nchini Inspekta Jenerali Saidi Ali Mwema, anapewa nafasi kubwa ya kushika wadhifa huo baada ya Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Afrika ya Kusini Kamishna Jenerali Bi. Mangwashi Phiyega, kumaliza muda wake katika nafasi hiyo.

Kamanda babile amesema. Endapo IGP Mwema, atachaguliwa kuwa Mwenyekiti mpya wa Shirikisho hilo la SARPCCO, itakuwa ni mara ya pili kwa Jeshi la Polisi nchini Tanzania kushikilia tena nafasi hiyo kubwa ya Mashirikisho ya Kimataifa Duniani.

Kwa mara ya kwanza Tanzania ilipata nafasi hiyo mwaka 2004 na  2005 kupitia kwa aliyekuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi hapa nchini Inspekta Jenerali Mstaafu Omari Iddi Mahita.

IGP Mstaafu Mahita, aliweka historia ya kuwa Mkuu wa kwanza wa Jeshi la Polisi hapa nchini kuwaongoza Wakuu wa Majeshi ya Polisi kwa nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika kupitia Shirikisho hilo kubwa la (SARPCCO) tangu lilipoanzishwa mnamo mwaka 1995, katika mji wa  Swakompumg nchini Namibia.

 “Ingawa mkutano huo utazungumzia zaidi masuala ya kiusalama, lakini pia ni fursa pekee kwa Visiwa vya Zanzibar na Tanzania kwa ujumla kutangaza na kukuza vivutio vyake vya kitalii kutokana na ujio wa wageni wengi kutoka mataifa mbalimbali duniani”. Alisema Kamanda Babile.

Amesema huo ni wakati wa wafanya biashara kufanya biashara zaidi na hata kupata nafasi ya masoko nje ya nchi kutokana na bidhaa zinazozaliswa ama kutengenezwa hapa nchini.

 Amesema, hata baada ya kumalizika kwa mkutano huo, kuna uhakika kuwa baadhi ya washiriki hasa wale wa Mashirika ya Kimataifa, watapenda kuendelea kubaki Zanzibar kutembelea fukwe za Bahari na kuona maeneo ya mbalimbali ambayo ni vivutio kwa wageni yakiwemo yale ya mji Mkongwe  yenye historia ya muda mrefu Ulimwenguni.

Zaidi ya wajumbe 250 kutoka nchi za SADC pamoja na wa Mashirika mbalimbali ya Kimataifa  duniani, wanatarajiwa kushiriki katika mkutano huo.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

HATUTOPAKI BASI DHIDI YA YANGA-MOKWENA

“PEMBA SALUTI KWENU” DK. NCHIMBI*

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA