CHADEMA YABWAGWA NA CCM UDIWANI MWANZA

KITENDAWILI cha nani atakuwa Meya wa Jiji la Mwanza kimeteguliwa jana baada ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kushinda kiti hicho dhidi ya wapinzani wake wakubwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Uchaguzi huo umefanyika baada ya Halmashauri ya Jiji la Mwanza kugawanywa Julai mwaka huu katika sehemu mbili. Halmashauri ya Jiji la Mwanza inakuwa katika Wilaya ya Nyamagana na sehemu ya pili inakuwa Manispaa ya Ilemela.

Wakati CCM kikiibuka na ushindi huo, uchaguzi wa Halmashauri ya Ilemela uliahirishwa baada ya Diwani wa Chadema aliyefukuzwa hivi karibuni, Henry Matata kuweka pingamizi.

Akitangaza matokeo ya uchaguzi wa Meya wa Jiji la Mwanza, Msimamizi wa Uchaguzi huo ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya jiji hilo, Wilson Kabwe alisema kura zilizopigwa na madiwani wa CCM, Chadema na Chama cha Wananchi (CUF) ni 19.

Alisema mgombea wa CCM, Stanslaus Mabula aliibuka mshindi kwa kupata kura 11 wakati mgombea wa Chadema, Charles Chinchibela alipata kura nane.

CCM pia kimeibuka na ushindi katika nafasi ya naibu meya baada ya mgombea wake, John Minja kupata kura 10 dhidi ya Daudi Mkama wa CUF aliyepata kura nane.

Chadema na CUF viliungana katika uchaguzi huo. Wakati Chadema kikisimamisha mgombea umeya, CUF kilifanya hivyo katika nafasi ya naibu meya.
Hata hivyo, kuliibuka mvutano mkali kati ya CCM na Chadema kuhusu wabunge wawili wa chama tawala ambao ilielezwa kwamba walikuwa katika Halmashauri ya Ilemela lakini wakahamishiwa Nyamagana.
Akizungumzia suala hilo, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema demokrasia imezingatiwa katika uchaguzi huo na kwamba suala la kuhamisha madiwani kwenda jimbo jingine lipo katika dhamana ya chama husika.
Alisema kuwa jiografia ya mkoa huo haina pingamizi kwa mbunge wa viti maalumu kuamua wapi anahitaji kufanyia kazi na akisema Chadema kilipiga hesabu zake vibaya.
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willbrod Slaa alisema chama chake kwa sasa hakiwezi kuzungumzia matokeo ya uchaguzi huo akisema ni chama makini ambacho kinahitaji muda wa kuyatafakari kabla ya kutoa uamuzi.

Ilemela
Uchaguzi wa Ilemela umeahirishwa baada ya Diwani wa Chadema aliyevuliwa uanachama na chama hicho, Henry Matata kuweka pingamizi.
Pingamizi hilo liliwasilishwa kwa msimamizi wa uchaguzi huo muda mfupi kabla ya uchaguzi kuanza. Alichukua hatua hiyo baada ya kubaini kwamba jina lake lilikuwa limekatwa miongoni mwa wagombea umeya.
Akisoma pingamizi hilo, Msimamizi wa Uchaguzi huo, Kabwe alisema diwani huyo alidai kwamba alikuwa na haki ya kugombea nafasi hiyo hadi shauri lake lililopo mahakamani litakapoamuliwa.
Hivi karibuni, Ofisi ya Katibu Mkuu wa Chadema ilifuta uteuzi wa awali wa wagombea wa nafasi za umeya na unaibu umeya kwa madai kuwa haukufanyika kwa kuzingatia sheria wa katiba ya chama hicho.
Dk Slaa alisema ofisi yake ndiyo yenye mamlaka ya kuteua wagombea katika nafasi hizo mbili.
Uchaguzi huo ulivuta hisia za wakazi wengi wa jiji la Mwanza kwani ilipotimu saa 3:45 asubuhi kulikuwa na mikusanyiko mingi katika maeneo yake mbalimbali na kusababisha askari wa kikosi cha kutuliza ghasia kufunga baadhi ya barabara.
Barabara ambazo zilifungwa ni Sekou Toure kuingia katika lango kuu la jiji hivyo kusababisha adha kwa wagonjwa waliokuwa wakifika katika Hospitali ya Mkoa.
Watu waliokuwa wakiruhusiwa kuingia katika ofisi ya jiji ni wale waliokuwa wakihusika na uchaguzi huo ambao ni wafanyakazi wa jiji, madiwani pamoja na waandishi wa habari.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KOCHA BENCHIKHA AMESEPA

MASHUSHUSHU WA MAMELODI WALIKUJA KUTUPELELEZA: HERSI

KOCHA WA AL.AHLY ASEMA YANGA NI TIMU BORA NA NGUMU