CHADEMA yamlima barua JK

• Wamtaka awatimue Nchimbi, Mwema, Kamuhanda

na Mwandishi wetu
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimemwandikia rasmi barua Rais Jakaya Kikwete, kikimtaka achukue hatua, kwa mujibu wa mamlaka yake kikatiba kuhusu mauaji ya kisiasa.

Katika barua hiyo ya Septemba 10, mwaka huu, iliyoandikwa na Mwenyekiti wa Taifa, Freeman Mbowe, pamoja na hatua nyingine CHADEMA imetaka Rais Kikwete achukue hatua ya kuwafukuza kazi baadhi ya viongozi.

Wanaotakiwa kufukuzwa ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi, IGP Said Mwema, Kamishna wa Operesheni wa Jeshi la Polisi, Paul Chagonja, RPC wa Mkoa wa Morogoro, Faustine Shigolile na RPC wa Iringa, Michael Kamuhanda, kwa kutowajibika kufuatia mauaji yaliyotokea katika mikoa ya Morogoro na Iringa.

Aidha, CHADEMA kimetaka Rais Kikwete aunde tume ya kijaji/kimahakama ya uchunguzi wa vifo vilivyotokea katika mikusanyiko, mikutano, maandamano au mazingira ya kisiasa yaliyohusisha chama hicho.

Vifo hivi ni vile vilivyotokea Arusha Januari 5, mwaka jana, Igunga Novemba mwaka huo huo, Arumeru Mashariki Aprili mwaka huu, Iramba Julai 14, Morogoro Agosti 27 na Iringa Septemba 2, mwaka huu.

Kwamba wakati wakisubiri hatua za rais pamoja na majibu ya barua hiyo, wanawaagiza viongozi na wanachama wake kutokutoa ushirikiano kwa kamati iliyoundwa na Waziri Nchimbi na timu zilizoundwa na Jeshi la Polisi kuchunguza mauaji yaliyofanywa na askari katika mikoa ya Iringa na Morogoro.

Mbowe alisema itakumbukwa kuwa katika maandamano yaliyoitishwa na CHADEMA Januari 5, mwaka jana jijini Arusha, watu watatu walipoteza maisha baada ya polisi kutumia nguvu na risasi za moto kutawanya waandamanaji.

“Katika uchaguzi mdogo wa Igunga pamoja na matukio mengine yaliyojitokeza na yaliyohusisha vurugu kinyume cha sheria, Mbwana Masoud, mwanachama wa CHADEMA alitekwa, kuteswa na kunyongwa katika mazingira ya kutatanisha. Mpaka sasa hakuna hatua stahiki zilizochukuliwa kufanya uchunguzi kuhusu kifo hicho,” alisema Mbowe.

Alisema kuwa mara baada ya uchaguzi mdogo wa Arumeru Mashariki, kiongozi wa kata wa CHADEMA, Msafiri Mbwambo, alichinjwa na chanzo chake kudaiwa kusababishwa na masuala ya kisiasa.

Aliongeza kuwa hivi karibuni yalitokea mauaji katika Kijiji cha Ndago, Wilaya ya Iramba mkoani Singida ambapo kikundi cha watu kilivamia na kushambulia mkutano wa CHADEMA kwa mawe, huku polisi wakiwepo bila kuchukua hatua.

“Baada ya mkutano kumalizika na viongozi wa CHADEMA kuondoka eneo la mkutano, kijana mmoja anayedaiwa kuwa kiongozi wa kata wa UVCCM alikutwa amepoteza maisha katika kijiji hicho, jirani na eneo ulipofanyika mkutano wa hadhara,” alisema Mbowe.

Kwamba hivi karibuni tena katika maandamano ya mapokezi ya viongozi wa CHADEMA mkoani Morogoro, polisi walimshambulia Ally Zona na kupoteza maisha, na baadaye wakatoa taarifa kuwa aligongwa na kitu kizito.

Katika barua hiyo, Mbowe aliongeza kuwa hivi karibuni mkoani Iringa wakati wa kufungua matawi ya chama chake kwenye Kata ya Nyololo, polisi walimlipua kwa bomu mwandishi wa habari wa kituo cha Televisheni cha Channel Ten, Daudi Mwangosi.

Alisema kuwa pamoja na polisi kuhusika na mauaji hayo, bado Waziri Nchimbi, IGP Mwema, Kamanda Chagonja, makamanda Shigolile na Kamuhanda hawakuchukua hatua yoyote ya kuwajibika kwa kuhusika moja kwa moja na matukio haya au kiutendaji katika jeshi hilo kwa ujumla.

“Ili kupata ukweli wa sababu za vifo hivyo, mauaji yote haya hayajafanyiwa uchunguzi wowote wa kimahakama/kijaji kwa mujibu wa sheria za nchi yetu kinyume na ahadi ya waziri mkuu bungeni wakati akihitimisha hoja yake katika Bunge la Bajeti la mwaka 2011/2012. Hakuna uchunguzi wa kifo ‘inquest’ uliofanyika na hakuna Mahakama ya Korona ‘Coroner’s Court’ iliyoanzishwa ili kuchunguza vifo hivi,” alisema Mbowe.

Kwamba Kamati Kuu ya CHADEMA katika kikao maalumu hivi k
aribuni, mojawapo ya mambo yaliyoazimiwa ni kumwandikia barua rais kwa lengo la kumtaka achukue hatua za utekelezaji kwa mujibu wa mamlaka yake na kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Iwapo serikali haitazingatia, CHADEMA kitawaongoza wananchi kwa njia za kidemokrasia, ikiwemo maandamano ya amani kushinikiza hatua za haraka kuchukuliwa kwa masilahi ya taifa,” alisema Mbowe.

Aliongeza kuwa katika majadiliano ya kina kabla ya kufikia maazimio na maamuzi hayo, kamati kuu ilizingatia kuwa hali ya siasa nchini ni tete, serikali inayoongozwa na CCM imeshindwa kusimamia vizuri rasilimali za nchi ikiwamo kudhibiti mfumuko na ongezeko la bei, hivyo kuchangia ugumu wa maisha kwa wananchi na migogoro ya kijamii na ufisadi nchini.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA

DKT NCHIMBI ASHIRIKI MAZISHI YA ASKOFU.GACHUMA WA KANISA LA NLGCC

π™‚π˜Όπ™ˆπ™Šπ™‰π˜Ώπ™„ π™†π˜Όπ˜Ύπ™ƒπ™€π™•π˜Ό π™†π™„π˜½π™„π™‰π™‚π™’π˜Ό.