IMEIKUTA MAHALI HII... KIDOGO NILIE, ISOME NA
WEWE;;;;;;
Ni siku
nyingi kidogo, mwaka 1979, lakini ni tukio ambalo liliniuma sana. Ilikuwa
vigumu sana kulisahau na lilinifanya nijiulize, inakuwaje Mungu
anakuwa mkatili kiasi kile. Lakini bila shaka ilikuwa ni wakati ule wa ufahamu
mdogo. Hivi sasa ninafahamu mengi
na hasa baada ya kujifunza maarifa haya ya utambuzi. Ilikuwa ni mwaka 1979 nikiwa nasafiri
kutokea Dar es salaam kwenda Arusha. Sijui ilikuwaje, lakini ilitokea. Tuliondoka
Dar es salaam saa 12.30 jioni. Wakati ule mabasi yalikuwa yakisafiri jioni na
usiku, sio kama siku hizi. Nilikuwa ninakwenda Arusha kwenye usaili kwa
ajili ya ajira, nikiwa ndio kwanza nimemaliza kidato
cha nne. Niliajiriwa moja kwa moja
serikalini, kwani siku zile ajira zilikuwa ni
za kumwaga. Hata hivyo sikuridhishwa na kazi niliyokuwa nafanya,
hivyo niliomba kazi kwenye kampuni moja kule Arusha na niliitwa kwa usaili.
Tulifika mji unaoitwa Korogwe ambao wakati ule ulikuwa ndio mji maarufu
kwa hoteli zake katika barabara yote ya Segera hadi Moshi na Arusha.
Tulipofika Korogwe
basi letu lilisimama kwa ajili ya abiria
kupata chakula. Niliingia kwenye hoteli moja ambayo
nakumbuka hadi leo kwamba ilikuwa ikiitwa Bamboo. Niliagiza chakula na
kula haraka kutokana na muda mfupi wa kula uliotolewa na wenye basi
la TTBS ambalo ndilo nililosafiri nalo. Wakati wa kulipa ndipo
niliposhangaa na kuogopa. Niliingiza mkono mifukoni na kukuta kwamba
sikuwa na hela. Nilianza kubabaika na mwenye hoteli alisema hawezi
kukubali ujinga huo, "Abiria wengine wahuni bwana, anakula na
kujifanya
kaibiwa, ukikubaliana nao kila siku hasara
tu" Mwenye hoteli alisema kwa kudhamiria
hasa. Kulizuka zogo kubwa, huku mwenye hoteli akisema ni lazima
anipeleke polisi. Ni kweli alimtuma mmoja wa watumishi wake kwenda
kituo cha polisi ili nishughulikiwe… … Hapo Hotelini kulikuwa na bwana mmoja
aliyekuwa amekaa pembeni na mkewe na watoto wao wakila. Yule bwana alipoona vile alimtuma
mhudumu mmoja aniite. Niliondoka pale kaunta nilipokuwa nabembeleza
na kuja kwa yule bwana. Alikuwa ni kijana mtu mzima kidogo, mwenye
miaka kama 50 hivi. Nilimsalimia na aliitikia, nilimsalimia mkewe pia.
Yule bwana aliniuliza kisa cha vurugu ile na nilimsimulia.
Aliniuliza sasa huko Arusha ningeishi vipi wakati wa usaili wakati nimeibiwa fedha zote na
ningerudi vipi Dar. Nilimwambia nilikuwa napanga namna ya kurudi Dar, kama
huko polisi ningeaminika. Kama mzaha vile yule bwana aliniambia kuwa
angenipa fedha za kutumia huko Arusha na nikirudi Dar
nimrudishie fedha zake. Nakumbuka alinipa shilingi 90 kwa ahadi kwamba nikirudi Dar nimpelekee
fedha zake ofisini kwake. Alinielekeza ofisini kwake, mtaa wa Nkuruma na
kuniambia kuwa ameamua kunisaidia kwa sababu kila binadamu anahitaji
msaada wa mwingine na maisha haya ni mzunguko.
Nilimshukuru na kuondoka kukimbilia basini. Basi lilikuwa linanisubiri mimi tu. Nilipanda ndani
ya basi na abiria wengine walinipa pole. Tuliondoka Korogwe, lakini
haikuchukua muda basi letu lilipata tatizo la pancha ya gurudumu moja
la mbele. Ilibidi tuegeshe pembeni ili litengenezwe. Baada ya matengenezo,
tuliondoka kuendelea na safari yetu. Karibu na mji wa Same kwenye saa saba
usiku, basi letu lilisimama ghafla. Abiria walisimama ndani ya basi na kulizuka aina ya kusukumana.
Huko nje kulikuwa na ajali. Abiria tulishuka haraka na wengine huko chini
walishaanza kupiga mayowe, hasa wanawake. Niliposhuka niliona gari ndogo nyeusi
ikiwa imebondeka sana na hapo kando kulikuwa na maiti wawili. Nilijua ni
maiti kwa sababu walikuwa wamefunikwa gubigubi.
Halafu kulikuwa na katoto kalikokuwa kanalia sana kakiwa kamefungwa kanga kichwani.
Tumwahishe huyu mtoto hapo Same hospitali ameumia, ingawa sio sana. Nilikatazama
kale katoto ka kiume kenye umri wa miaka kama mitatu. Kalikuwa kameumie
kwenye paji la uso, lakini kalikuwa hai. Bila shaka wale walikuwa ni
wazazi wake, kalikuwa yatima tayari. Machozi yalinitoka.
Baada ya kupata msaada na askari wa usalama barabarani kuchukua maiti wale tulipanda basini
kuendelea na safari yetu. Kale katoto kalichukuliwa na jamaa fulani
waliokuwa na Land Rover ya serikali kukimbizwa hospitalini. Ndani ya
Basi mazungumzo yalikuwa ni kuhusu ajali ile tu, hadi tunafika
Arusha. Tulichelewa sana kufika Arusha kwani tulifika kwenye saa tano asubuhi, badala ya saa
mbili . Nililala kwenye hoteli rahisi na kufanya usaili kesho yake. Ni
hiyo kesho, baada ya usaili niliponunua gazeti ambapo
nilipata mshtuko mkubwa ajabu. Kumbe wale watu wawili waliokufa kwenye ajali ile ya Same
walikuwa ni yule bwana aliyenisaidia hela na mkewe. Yule mtoto wao ndiye aliyeokoka.
Niligundua hilo baada ya kusoma jina lake na jina la kampuni aliponiambia nimpelekee
fedha zake nikirudi Dar, pamoja na picha yake, mke na mtoto. Nililia sana, kama
mtoto. Nillishindwa kujua ni kwa nini
afe. Nilijiuliza ni nani sasa angemlea mtoto yule? Yalikuwa ni maswali yasiyo na majibu na
pengine maswali ya kijinga pia. Nilijua kwamba nilikuwa na deni, deni la
shilingi tisini. Kwa wakati ule shilingi tisini zilikuwa ni sawa na
shilingi laki moja za sasa. Kwa mara ya kwanza sasa nilijiuliza ni kwa
nini marehemu yule aliniamini nakuamua kunipa fedha zile. Sikupata
jibu. Nilikata kipande
kile cha gazeti la kingereza kilichokuwa na habari ile. Nilichukuwa kipande hicho na kukiweka
kwenye Diary yangu. Deni, Ningelipa vipi deni la watu? Nilijikuta
nikipiga magoti na kuomba mungu anipe uwezo wa kuja kulilipa deni la mtu yule
mwema kwa njia yoyote. 'Mungu naomba uje uniwezeshe kulilipa deni la marehemu kwa sura na
namna ujuavyo wewe. Nataka kulilipa deni hili ili nami niwe nimemfanyia
jambo marehemu,' niliomba. Nilirejea Dar siku hiyo hiyo.Kwa sababu ya
mambo mengi na hasa baada ya matokeo ya usaili ule kuwa mbaya
kwangu, nilijikuta nikiwa na mambo mengi na kusahau haraka sana kuhusu mtu yule aliyenisaidia
mbaye ni marehemu. Nilifanikiwa hata hivyo kupata nafasi ya
kusoma Chuo cha Saruji na baadae chuo cha ufundi na hatimaye nilibahatika kwenda nchini
Uingereza. Mwaka 1991 nilianza shughuli zangu. Ilikuwa ni mwaka 1995
nikiwa ofisini kwangu pale lilipokuwa jengo Nasaco ambalo liliungua
mwaka 1996, ambapo lilijengwa upya na kubadilishwa jina na kuitwa
Water Front. Nikiwa nafanya kazi zangu niliambiwa na sekratari wangu kwamba
kulikuwa na kijana aliyekuwa anataka kuniona. Nilimuuliza ni kijana gani, akasema
hamjui. Nilimwambia amruhusu aingie. Kijana huyo aliingia ofisini. Alikuwa ni
kijana mdogo wa umri miaka kama 17 au 18 hivi, mweupe mrefu kidogo.
Alikuwa amevaa bora liende , yaani hovyohovyo huku afya
yake ikiwa hairidhishi sana. Nilimkaribisha ilimradi basi tu, kwani niliona atanipotezea bure
muda wangu. Ni lazima niwe mkweli kwamba sikuwa mtu mwenye huruma sana na nilikuwa
naamini sana katika watu wenye
pesa au majina. Nilimuuliza, “nikusaidie nini kijana na ukifanya haraka nitashukuru maana nina
kikao baada ya muda mfupi”. Nilisema na sikuwa na kikao chochote , lakini
nilitaka tu aondoke haraka. “Samahani mzee, nilikuwa
na shida…..nimefuk uzwa shule na sina tena mtu wakunisaidia kwa sababu …..nime….niko ….kidato
cha pili na hivyo tu natafuta tu kama atatokea mtu…….. Nilimkatisha. “Sikiliza
kijana. Kama huna jambo lingine la
kusema, ni bora ukaniacha nifanye kazi. Hivi unafikiri kama nikiamua kumsaidia kila mtu aliyefukuzwa
shule si nitarudi kwetu kwa miguu! Nenda Wizara ya Elimu waambie…… Kwanza
wazazi wako wanafanya kitu gani,
kwa nini washindwe …..Kwa nini walikupeleka shule ya kulipia kama hawana
uwezo, wanataka sifa?” “Hapana wazazi wangu walikufa na ninasoma shule ya serikali. Nimekosa
mahitaji ya msingi na nauli ya kwendea shule. Nasoma shule ya Kwiro, Morogoro.
Shangazi ndiye anayenisomesha, naye ana kansa na hivi sasa hata kazi hafanyi….,”
Alianza kulia. Huruma fulani ilinijia na nilijiambia, kama ni nauli tu na matumizi,
kwa nini nisiwe mwema, angalau
kwa mara moja tu. “Baba na mama walifariki lini?” Niliuliza nikijua kwamba, watakuwa wamekufa
kwa ukimwi, maana kipindi kile ndipo fasheni ya ukimwi ilipoanza, ambapo kula
anayekufa huhesabiwa kwamba kafa kwa ukimwi. “Walikufa kwa ajali
nilipokuwa mdogo sana, nilipokuwa na miaka mitatu.
Ndio shangazi yangu akanichukua na kunilea hadi sasa anakufa kwa kansa.” Yule kijana alilia
zaidi. Naomba nikwambie wewe msomaji unayesoma hapa kwamba, kuna nguvu
fulani na sasa naamini kwamba ziko nyingi ambazo huwa zinaongoza maisha
yetu bila sisi kujua. Kitu fulani kilinipiga akilini paaa! Nilijikuta
namuuliza yuel kijana. “Kwa nini umeamua kuja kwangu, ni nani
alikuelekeza hapa na wazazi wako walikufa mwaka gani na wapi?” Yule kijana alisema, “Nimeona
nijaribu tu kwa mtu yeyote ambaye anaweza kunisaidia, na ndionimejikuta
nikiingia hapa, sijui……..sikutu mwa na mtu. Wazazi wangu walikufa mwaka1979
huko Same na mimi wanasema nilikuwa kwenye ajali, nikaokoka.
Niliumia tu hapa.” Alishika kwenye kovu juu ya paji lake la uso.
Nilihisi kitu fulani kikipanda tumboni na kuja kifuani halafi niliona kama vile
nimebanwa na kushindwa kupumua. “Baba yako alikuwa anaitwa nani?” “Alikuwa anaitwa Siame….Cosmas
Siame….” Niliinuka ghafla hadi yule kijana alishtuka . Nilikwenda kwenye
kabati langu mle ofisini na kuchafua kwenye droo moja na kutoka na diary.
Mikono ikinitetemeka, nilitoa kipande cha gazeti ndani ya diary hiyo,
nilichokuwa nimekihifadhi. “Ndio alikuwa anaitwa Cosmas
Siame. Huyu ni mtoto wake, ni yule mtoto aliyenusurika.” Nilinong’ona. Nilijikuta nikipiga
magoti na kusali. “Mungu, wewe ni mweza na hakuna kinachokushinda . Nimeamini
baba kwamba kila jema tunalofanya ni akiba yetu ya kesho na kesho hiyo
huanzia hapa duniani.” Halafu nillinyamaza na kulia sana. Nililia kwa
furaha na ugunduzi wa nguvu zinazomgusa binadamu kwa kila analofanya.
Nilisimama nikiwa nimesawajika kabisa. Nilihisi kuwa mtu mwingine
kabisa. Nilimfuata yule kijana na kumkumbatia huku nikiwa bado ninalia. “Mimi
ni baba yako mdogo, ndiye nitakyekulea sasa. Ni zamu yangu sasa kukulea
hadi mwisho” Naye alilia bila kujua sababu na alikuwa amechanganyikiw a kabisa.
Nilirudi kwenye kiti na kumsimulia kilichotokea miaka 17 iliyopita.
Tuliondoka hapo na kwenda kumwona shangazi yake
Ubungo, eneo la maziwa ambako alikuwa amepanga chumba. Kutokana na hali yake nilimhamishia
kwangu, baada ya kumsimulia kilichotokea. Huyo dada yake Cosmas alifurahi
sana hadi akashindwa kuzungumza kwa saa nzima. Alifariki hata hivyo mwaka mmoja
baadae, lakini akiwa ameridhika sana. Kijana Siame alisoma na kumaliza
Chuo Kikuu na hivi sasa yuko nchini Australia anakofanya kazi. Ukweli
ni kwamba ni mwanangu kabisa sasa. Naamini huko waliko Mbinguni
wazazi wake wanafurahia kile walichokipanda miaka mingisana nyuma. Lakini
nami najiuliza bado. Ilikuwaje Cosmas akanipa msaada ule? Halafu najiuliza
ni kitu gani kilimvuta mwanae Siame hadi ofisini kwangu akizipita
ofisi nyingine zote? Nataka nikuambie, usiwe mbishi sana bila sababu, kuna
nguvu za ziada zinazoongoza matokeo maishani mwetu…………
*************MW ISHO*******
Comments