MAANDAMANO YA WANAHABARI YATIKISA NCHI

*Waandamana kulaani kuawa Mwangosi
*Wataka polisi walioua wawajibishwe
*Waziri Nchimbi aondolewa mkutanoni

Waandishi wa habari wakiaandamana jijini Dar es Salaam jana kupinga maauaji ya kikatili aliyofanyiwa mwenzao, marehemu Daudi Mwangosi, aliyeuawa mkoani Iringa akiwa kazini Septemba 2, mwaka huu.
Karibu nchini kote, waandishi wa habari jana waliandamana kimya kimya kulaani mauaji ya mwenzao, aliyekuwa mwakilishi wa kituo cha televisheni ya Channel Ten, mkoani Iringa, Daudi Mwangosi, na kumwondoa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi, katika mkutano wao baada ya kufika katika viwanja vya Jangwani, jijini Dar es Salaam, kwa ajili ya kujumuika nao katika kilele cha maandamano hayo bila kualikwa.

Mbali na kumtaka Waziri Nchimbi aondoke eneo la mkutano huo, waandishi walipitisha azimio la pamoja la kutoandika habari zinazohusu Jeshi la Polisi, ambalo askari wake wanatuhumiwa kumuua kwa bomu Mwangosi, ndani ya siku 40 za maombolezo, isipokuwa habari mbaya zitakazolihusu jeshi hilo.

JIJINI DAR


Jijini Dar es Salaam, maandamano hayo yalianzia katika kituo cha televisheni hiyo kilichopo katikati ya jiji, majira ya saa 3.00 asubuhi, baada ya waandishi wengi waliokuwa wamevalia mavazi ya rangi nyeusi kuashiria maombolezo, wakiwa wamefunga plasta na gundi midomoni, kukusanyika katika eneo hilo tayari kwa kuandamana.

Wakiwa wamebeba mabango yenye ujumbe, ambao pamoja na mambo mengine, kulaani mauaji ya mwandishi huyo, maandamano hayo yalipita katika Barabara za Bibi Titi Mohamed na Morogoro na kuhitimishwa katika viwanja hivyo, majira ya saa 3.15 asubuhi, ambako viongozi wa klabu mbalimbali za wanahabari zikiongozwa na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), walihutubia.

Baadhi ya mabango yalikuwa na ujumbe usemao: “IGP Said Mwema hatuna imani na wewe kama vipi achia ngazi”, “Mwema unangoja nini”, “Tunasikitishwa na tunalaani vikali mauaji ya kikatili ya mwandishi wetu wa habari mkoani Iringa Daudi Mwangosi”, “Why killing the messenger”, “Damu ya Mwangosi isafishe Jeshi la Polisi.”

Mabango mengine yalikuwa na ujumbe usemao: “Mtatuua lakini tutaandika ukweli”, Hatunyamazi kwa mtutu wa bunduki”, “Mwangosi Shujaa kafa kishujaa atabaki shujaa”, “Kalamu na kamera zetu ni zaidi ya risasi na mabomu yenu”, Polisi bila bunduki hawana chao”, na “This is not the way stop killing, the way open soon”.

Maandamano ya wanahabari hao yalilindwa na polisi waliokuwa kwenye magari yenye namba T 220 AMV, T 337 AKV na PT 2093, huku baadhi ya askari wakiwa na mabomu na silaha za moto.

Waandamanaji walifika katika viwanja hivyo na kukuta Waziri Nchimbi akiwa tayari amekwishafika akisubiri kuwapokea waandamanaji katika eneo lililotengwa kwa ajili ya kuhitimishia maandamano hayo.

Kwa kuwa hakukuwa na taarifa tangu mapema za kualikwa kwake, wanahabari waliokuwa kwenye maandamano hayo walipigwa na mshangao baada ya kumuona waziri huyo akiwa katika eneo hilo akisubiri kuwapokea na kujumuika nao katika tukio hilo.

Hali hiyo ilizua hasira kutoka kwa wanahabari, ambao walishindwa kujizuia na kuanza kupaza sauti za kumtaka waziri huyo aliyewasili katika viwanja hivyo kwa kutumia gari T 830 AWN aondoke katika eneo hilo.

NCHIMBI AKATALIWA MKUTANONI


Hata hivyo, Waziri Nchimbi, aliendelea kubakia katika eneo hilo na kujongea kwenye kifusi kilichokuwa kinatumika kama jukwaa.

Wanahabari waliendelea kung'ang'ania aondoke kwa kuwa hakuna kiongozi yeyote wa serikali aliyekuwa amealikwa, hivyo shughuli hiyo haikuwa inamhusu.

Kutokana na msimamo wa wanahabari hao huku wakipaza sauti: “Hatutaki, aondoke!”, “Aangalie kwenye Tv!”, “Ataangalia kwenye taarifa ya habari!”, “Atatuletea polisi!”, Waziri Nchimbi aliamua kuondoka eneo hilo, lakini wakati akiondoka wanahabari walianza kumzomea na kutoa sauti zinazofanana na mlipuko wa bomu: “Buubu!” “Buuu!”, “Mheshimiwa buuu!”

Aidha, wakati anaondoka, baadhi ya wanahabari walimfuata kwa lengo la kutaka aeleze namna alivyopokea hatua ya wanahabari kumtimua eneo hilo.

Kitendo cha wanahabari hao kiliwaudhi wenzao, ambao walianza kuwakemea kwa kuwauliza: “Mmeshamkataa, sasa mnamhoji kwanini?” “Aondoke!”, “aondoke!”, “Aondoke!”.

Kabla ya kuondoka katika viwanja hivyo, Waziri Nchimbi alisema uamuzi wa waandishi kufanya maandamano ni jambo jema kwa kuwa maandamano hayo yamefuata taratibu za kisheria kwa kuomba kibali, ambacho baada ya kupewa walipewa ulinzi wa polisi uliowawezesha kutekeleza haki yao ya kidemokrasia.

Alisema serikali inachopambana nacho ni tabia ya watu kufanya maandamano kinyume cha sheria.

Vilevile, alisema maandamano ya wanahabari anayaunga mkono kwa kuwa yana lengo jema linalotaka kila Mtanzania maisha yake lazima yaheshimike na yalindwe na kusema ujumbe huo ni mzuri sana kwa taifa.

“Na ndiyo maana wakati wote na tunapoona mkutano kama wa leo, ujumbe ambao waandishi wanautoa kwa taifa kwamba, maisha ya Watanzania yana thamani kubwa na kufanikiwa juu ya kuyalinda, lazima serikali iuchukue kwa uzito unaostahili,” alisema Dk. Nchimbi na kuongeza:

“…Sisi kama serikali tunaupokea kwa moyo safi na tunawapenda na tunawapa ushirikiano. Na kupitia kwenu nitoe kwa viongozi wote wa polisi wa mikoa wakutane na waandishi wa habari kuzungumza nao kuhusu utaratibu wa kufanya kazi pamoja na ushirikiano.”

Hata hivyo, Waziri Nchimbi ambaye alionekana kuwa ana mengi ya kuzungumza, lakini hakuweza kuendelea baada ya zogo kubwa kuzuka kutoka kwa wanahabari wakati akizungumza hayo na hivyo kulazimika kukatisha na kuondoka eneo hilo.
Baada ya Waziri Nchimbi kuondoka, viongozi wa klabu za waandishi na TEF walianza kuzungumza.

KALAMU NI ZAIDI YA BUNDUKI

Katibu Mkuu wa TEF, Nevil Meena, alisema lengo la kufanya maandamano ni kutumia njia wanazotumia Watanzania wengine kueleza kero zao.

Alisema kuuawa kwa Mwangosi kumeibua hisia kali miongoni mwa waandishi wa habari pamoja na wanaharakati, huku wengi wao wakihoji usalama wa waandishi wanapokuwa kazini hasa katika mazingira magumu.

Aliwataka polisi kutambua kuwa kama waandishi wa habari wataamua kutumia kalamu zao polisi watakuwa katika wakati mgumu lakini hawataki hali hiyo ifike hapo.

“Waandishi wa habari tuna mamlaka makubwa katika nchi hii, kwa taaluma yetu tukisema jambo lolote kwenye vyombo vya habari linaaminika. Haiwezekani waandishi wakawa wanauawa,” alisema Meena.

CHANNEL TEN: ASANTENI

Mhariri Mkuu wa Habari wa Channel Ten, Dina Chahali, aliwashukru wanahabari kwa mshikamano waliouonyesha kwa kufanya maandamano hayo.

Mhariri wa gazeti la Jamhuri, Manyerere Jackton, alisema kuuawa kwa Mwangosi kusiwaogopeshe waandishi waliobaki kutekeleza majukumu yao, badala yake wasonge mbele.

Mhariri Mtendaji wa gazeti la NIPASHE, Jesse Kwayu, alisema waandishi wameandamana kwa sababu Mwangosi ametwaliwa kwa njia ya kikatili na si ya kawaida.

Hata hivyo, alisema damu ya Mwangosi itakuwa ndiyo mwanzo wa kubadilisha Jeshi la Polisi ili watambue kazi zinazofanywa na waandishi na kuzithamini.

“Polisi watambue kuwa watu wanalipa kodi ili wapate magwanda, wapate bunduki ili kulinda raia na si kuua raia,” alisema Kwayu.

Mwenyeki wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Dar es Salaam, Jane Mihanji, aliitaka Tanzania, Afrika na dunia kutambua kuwa waandishi ni sawa na wafanyakazi wengine, hivyo lazima wathaminiwe.

Alisema ifike wakati wanahabari wanapewa mafunzo ya jinsi ya kufanya kazi na polisi.

Abubakar Karsan alisema watahakikisha polisi waliomuua Mwangosi wanaihudumia familia ya Mwangosi hadi watakapofariki.

Rais wa Klabu za Waandishi wa Habari, Keneth Simbaya, aliwataka waandishi kujipanga katika kutafuta haki zao, kwani mauaji dhidi yao yanafanywa ili kuidhoofisha demokrasia nchini.

MAANDAMANO YAFANYIKA MWANZA


Mkoani Mwanza, Mkuu wa Polisi Wilaya (OCD) ya Nyamagana (OCD), Ally Kitumbu, alizuia maandamano hayo mpaka hapo Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, takapomaliza ziara yake ya wiki moja iliyoanza juzi mkoani humo.

Hata hivyo, maandamano hayo yalifanyika bila ulinzi wa polisi.

POLISI ARUSHA WAZUIA WAANDISHI

Maandamano ya wanahabari hayakufanyika mkoani Arusha kutokana na polisi kuyauzia kwa madai kwamba, yangeathiri mkutano wa kimataifa wa masuala ya mazingira.

Awali, waandishi wa habari walijikusanya katika eneo la Makumbusho ya Azimio la Arusha kwa nia ya kuanza maandamano, lakini ghafla walipata taarifa za kuzuiwa kwa maandamano yao kwa madai kuwa polisi ni wachache wa kuyalinda.

KAGERA, NA SINGIDA WAANDAMANA

Wanahabari katika mikoa ya Singida na Kagera jana waliungana na wenzao nchini kwa kufanya maandamano kulaani mauaji hayo.

Mkoani Singida, maandamano yalisindikizwa na askari polisi. Yalianzia eneo la Benki ya NBC na kupita katika Barabara ya Kawawa hadi kituo cha mafuta cha Esso, Barabara ya Soko Kuu, Msikitini, Mghandi, Ipembe, Karume, Kinyeto na kumalizikia kwenye ofisi ya klabu ya wanahabari (SINGPRESS).

KILIMANJARO WAANDAMANA
Mkoani Kilimanjaro, maandamano hayo yalianzia katika eneo la Posta na kupita katika Barabara ya Market, JK Nyerere hadi Ofisi za Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Kilimanjaro (Meck).

TANGA, KIGOMA WALAANI MAUAJI


Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari mkoani Tanga (TPC), Hassan Hashim, alisema wanalaani kwa nguvu zote mauaji ya Mwangosi, kwa kuwa ni kinyume cha wajibu wa Jeshi la Polisi.

Pia Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi mkoani Kigoma, Deogratius Nsokolo, alilaani mauaji hayo.

MBEYA KUANDAMANA LEO

Jeshi la la Polisi Wilaya ya Mbeya liligoma kutoa kibali kuruhusu maandamano ya waandishi wa habari kwa madai kuwa barua ya maombi ilichelewa kuwafikia kwa mujibu wa sheria.

Katibu wa Chama cha Waandishi wa Habari mkoani Mbeya (MBPC), Kenneth Mwazembe, alisema Mkuu wa Polisi Wilaya ya Mbeya alikataa kutoa kibali hicho kwa madai kuwa sheria inataka taarifa ifikishwe polisi ndani ya saa 48 kabla ya maandamano kufanyika.

Mwazembe alisema kuwa baada ya Polisi kugoma kutoa kibali, MBPC juzi lipeleka barua nyingine iliyokidhi matakwa ya sheria hiyo ikiomba maandamano hayo yafanyike leo mkoani hapa, ambapo yameruhusiwa.

Maandamano hayo yataanzia katika kituo cha daladala cha Mafiati kilichopo eneo la Mwanjelwa, ambapo waandamanaji watatembea kwa miguu kwenda katikati ya Jiji la Mbeya hadi kituo cha daladala cha BP ya zamani, ambako yatapokelewa na Mwenyekiti wa MBPC, Christopher Nyenyembe.

MAANDAMANO RUVUMA HAYAJAFANYIKA

Mkoani Ruvuma, maandamano hayajafanyika kutokana na viongozi wa Chama cha Waandishi wa Habari mkoani humo kutoyaitisha.

Hali hiyo imesababisha waandishi wa habari kugawanyika na baadhi yao kutishia kujiuzulu nafasi zao za uongozi na uanachama.

IRINGA WAANDAMANA

Mkoani Iringa, ambako marehemu Mwangosi kilikuwa kituo chake cha kazi, maandamano hayo yalifanyika, ambapo pamoja na mambo mengine, waandishi walilitaka Jeshi la Polisi kuhakikisha wanamsaidia mjane na watoto wa marehemu ili aweze kumudu kuendelea na maisha.

Pia walilitaka jeshi hilo kurejesha vitendea kazi alivyokuwa navyo marehemu mauti yalipomkuta akiwa mikononi mwa polisi. Vitu hivyo, ni pamoja na kamera, kompyuta mpakato (laptop) na simu ya kiganjani.

Aidha, waandishi hao waliendelea na msimamo wao wa kutoendelea kufanya kazi na jeshi hilo huku wakimtaka Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Michael Kamuhanda, ajiuzulu kupisha uchunguzi huru wa mauaji hayo.

POLISI SHINYANGA WAZUIA MAANDAMANO


Kamanda wa Polisi mkoani Shinyanga, Evarist Mangala, alizuia maandamano, hatua iliyowafanya waandishi wa habari kutangaza kutoandika habari za polisi hadi hapo polisi watakapofuta amri yao hiyo.

MARA WAZUIWA PIA

Jeshi la polisi mkoani Mara jana lilimepiga marufu kufanyika kwa maandamano ya waandishi wa habari kwa maelezo kuwa walichelewa kutoa taarifa ndani ya saa 48.

Taarifa ya maandishi ambayo ilisaniwa ASP Hamad Panga kwenda Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Mara (MRPC) jana ilimema kamwe jeshi haliwezi kuruhusu kufanyika maandamano hayo kutokana na kukiuka sheria.

Kamanda wa polisi mkoani Mara, Abslom Mwakyoma, akizungumza baada ya barua hiyo kupokelewa na Mwenyekiti wa MRPC, Emanuel Bwimbo, alisema:

“Nimesema siwezi kuruhusu kufanyika kwa maandamano hayo kwa vile hamjatimiza sheria hivyo mimi kama msimamizi wa sheria sitakubali niwe wa kwanza kuzifunja na mkibisha mjaribu muone cha mtema kuni."

“Maandamano yanaazia watu wawili, tukiwakuta waandishi leo mnatembea kuanzia watu wawili msije kutulaumu kwa hatua tutakayochukua, nawashauri kwa vile nyie mnajua sheria tekelezeni agizo hilo, ” alisema Mwakyoma.

Imeandaliwa na Muhibu Said na Thobias Mwanakatwe, Dar; Elisante John, Singida; Salome Kitomari, Moshi; Dege Masoli, Tanga; George Ramadhan, Mwanza; Cynthia Mwilolezi na John Ngunge, Arusha; Emmanuel Lengwa, Mbeya; Gideon Mwakanosya na Nathan Mtega, Songea.

CHANZO: NIPASHE

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA

DKT NCHIMBI ASHIRIKI MAZISHI YA ASKOFU.GACHUMA WA KANISA LA NLGCC

π™‚π˜Όπ™ˆπ™Šπ™‰π˜Ώπ™„ π™†π˜Όπ˜Ύπ™ƒπ™€π™•π˜Ό π™†π™„π˜½π™„π™‰π™‚π™’π˜Ό.