MAIGE AHOJIWA NA TAKUKURU

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), imemvaa aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige na kumhoji kuhusu tuhuma kadhaa zinazomkabili, ikiwamo kumiliki ghorofa la mamilioni ya fedha, jijini Dar es Salaam.

Katika siku za hivi karibuni, Maige amekumbwa na kashfa kadhaa kubwa ikiwamo ya kumiliki nyumba yenye thamani ya Dola 410,000 za Marekani (sawa na Sh700 milioni), nyumba ambayo ilizua mjadala mkubwa huku baadhi ya watu wakihoji namna alivyopata fedha hizo wakati akiwa mtumishi wa umma.

Kashfa nyingine dhidi ya Maige ni ile ya kujimilikisha vitalu na kufanya biashara ya wanyama hai, akiwa waziri mwenye dhamana ya Maliasili na Utalii.

Habari zilizopatikana jana zilisema mbali na kuhojiwa kuhusu nyumba hiyo, pia alihojiwa kuhusu tuhuma mbalimbali ikiwamo ile iliyomfanya Rais Jakaya Kikwete amwondoe katika Baraza la mawaziri.

Hata hivyo, alipoulizwa kuhusu suala hilo, Maige alisema asingependa kulizungumzia na kwamba hajahojiwa na Takukuru.

"Sipendi kuzungumzia hilo, hata hivyo mimi sijahojiwa na Takukuru, niko Mwanza katika shughuli zangu binafsi," alisema.
Tuhuma nyingine zinazomkabili zinatokana na Ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) iliyotolewa wakati Maige akiwa waziri, ikieleza kuwa ofisi yake ilipoteza Sh874,853,564 baada ya kufanya uamuzi wa upendeleo wa kutoa kiwango cha chini cha mrabaha katika mauzo ya misitu.

Katika kipindi cha ukaguzi wa hesabu za Shirika la Hifadhi ya Taifa Tanzania (Tanapa), ilibainika kuwa shirika liliingia mkataba na Kampuni ya CATS Tanzania LTD , kuhusu matengenezo ya kawaida, ufungaji wa vifaa vya mawasiliano na vifaa vingine katika mkataba wa jumla ya Dola milioni moja za Marekani.

Maige pia anakabiliwa na tuhuma za kutengeneza mazingira ya rushwa katika ugawaji wa vitalu vya uwindaji, ugawaji ambao inadaiwa ulitawaliwa na dosari nyingi ikiwamo kutangaza majina ya waliopata vitalu bila kuonyesha vitalu walivyopewa.

Pia, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi na Maliasili ilieleza kuwa kampuni 16 zilizopewa vitalu hivyo, hazikuomba na kwamba vitalu hivyo vilikuwa vya daraja la kwanza na la pili.

Habari zaidi zilisema kuwa Takukuru pia imepanga kufuatilia mali zake katika Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma, ili kubaini kama alichokiorodhesha ni sahihi.

“Takukuru wamesema hiyo ni moja ya kazi zao za kila siku, kuchunguza tuhuma mbalimbali na ukipatikana ukweli, hukabidhi jalada kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP)” zilieleza habari hizo.

Habari hizo zilisema Takukuru imeanza uchunguzi dhidi ya tuhuma hizo na hadi jana, Maige alikuwa amehojiwa mara tatu.

"Usiku wa kuamkia leo (jana), alihojiwa Makao Makuu ya Takukuru tangu saa 2 usiku hadi usiku wa manane. Alienda Takukuru akiwa na mwanasheria wake," ilisema moja ya chanzo cha habari.

Chanzo hicho kimeendelea kueleza kuwa mbali na kumhoji, Takukuru imewasiliana na Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma kuchunguza tamko la Maige kuhusu mali zake.

Mkurugenzi wa Takukuru, Dk Edward Hoseah alipotakiwa kuzungumzia suala hilo hakutaka kuthibitisha wala kukanusha.

Alisema “Siwezi kulizungumzia jambo hilo kwa kuwa sheria zinanibana.”

Mwanzoni wa wiki hii wakati anajibu maswali ya washiriki wa kongamano la kujadili utekelezaji wa awamu ya pili ya mpango wa kupambana na rushwa nchini na mapendekezo yanayopaswa kuzingatiwa katika utekelezaji wa mpango wa awamu ya tatu wa 2012-2016, Dk Hoseah alisema uchunguzi wowote ukikamilika jalada hupelekwa kwa DPP.


Nyumba ambayo Maige anadaiwa kuimiliki ipo katika eneo la Mbezi Beach jijini Dares Salaam ambayo hivi karibuni alidaiwa kutafuta wanunuzi kwa Dola za Marekani 800,000 (takriban Sh700 milioni).

Watu wa karibu na Maige walilidokeza gazeti hili kuwa waziri huyo wa zamani, amefikia uamuzi wa kuuza nyumba hiyo, kwa kile alichoeleza kuwa ni kama mkosi kwake kwa kuwa ni moja ya sababu za mambo yake kuwa mabaya kisiasa.

Habari za awali zilizolifikia gazeti hili zilieleza kuwa Waziri Maige alinunua nyumba hiyo kutoka kwa Kampuni ya Savana Real Estate.

Mmoja wa madalali wanaouza nyumba za kampuni hiyo aliyejitambulisha kwa jina moja la Athuman (Ustadhi) alilithibitishia gazeti hili kwamba Maige alinunua nyumba moja kati ya nne zilizokuwa sokoni kwa wakati huo.

Hata hivyo, hakutaka kueleza alinunua nyumba hiyo lini na kwa gharama gani baada ya kueleza kuwa yeye siyo msemaji wa kampuni hiyo.

Baada ya kuibuka kwa taarifa hizo mwanzoni mwa mwaka huu, Maige aliliambia gazeti hili kwamba hakununua nyumba hiyo kwa Dola 700,000 kama ilivyodaiwa, bali aliinunua kwa Dola za Marekani 410,000.

Maige alifafanua namna alivyoinunua nyumba hiyo na kuonyesha nyaraka mbalimbali, huku akieleza kuwa sehemu ya fedha alizonunulia, zilikuwa za mkopo kutoka Benki ya CRDB.

Alisema 2005 alipoanza kuwa mbunge alipata mkopo ambapo yeye na wenzake watatu, waliunda kampuni ya kusafirisha mzigo ya Splendid Logistic na kuanza kununua magari matatu na baadaye magari hayo yaliongezeka na kufikia saba.

Alisema kuwa Septemba, 2010 mwenzao mmoja alijitoa katika kampuni hiyo, hivyo waliamua kugawana mali kwa kuzingatia mtaji wa kampuni ambapo alipata magari mawili na mwenzake manne akiongeza kuwa gari moja kati ya hayo saba lilipata ajali.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA

DKT NCHIMBI ASHIRIKI MAZISHI YA ASKOFU.GACHUMA WA KANISA LA NLGCC

π™‚π˜Όπ™ˆπ™Šπ™‰π˜Ώπ™„ π™†π˜Όπ˜Ύπ™ƒπ™€π™•π˜Ό π™†π™„π˜½π™„π™‰π™‚π™’π˜Ό.