Nilichokiona Na Kukisikia Kijijini Nyololo, Siku 4 Baada Ya Mauaji Ya Mwandishi Daud Mwangosi...


Ndugu zangu,

IJUMAA alfajiri ya Septemba 7 niliondoka nyumbani Iringa kuelekea Njombe kikazi. Jana yake, alhamisi usiku, Mwandishi Gershom Malegesi wa Redio Ebony FM alinipigia simu kuniomba nishiriki kwa simu kwenye kipindi chake maarufu cha ' Morning Talk'.

Nikamjibu, kuwa kwa vile nina safari ya Njombe, basi, nikifika kijijini Nyololo, Mufindi, nitasimama na kuongea na wakazi wawili watatu waniambie wanachofikiri juu ya kilichotokea. Kisha Maregesi aniunganishe kwa simu nikiwa hapo Nyololo tuongee redioni. Tukakubaliana.

Baada ya kutoka Mafinga na kuumaliza msitu wa Sao Hill, nilianza kuiona Nyololo kutoka mlimani. Nilipaki gari yangu takribani nusu kilomita kabla ya kuingia kijijini Nyololo. Nikaanza kutembea kwa miguu kuelekea kijijini bila kushika kamera wala mkoba.

Sweta nililovaa siku hiyo la rangi ya zambarau huenda lilinifanya nionekane kama ' wapasua mbao' wengine! Ilinisaidia, maana, kwenye meza ya kwanza ya biashara pale kijijini, niliwakuta akina mama watatu wakisikiliza kwa makini ' Morning Talk' ya Ebony FM. Kulikuwa na watu waliokuwa Nyololo siku ya tukio wakitoa ushuhuda wao studioni.

Nilimwandikia meseji mtangazaji Malegesi kuwa angeweza kuniunganisha hewani kwa wakati huo. " Kaka, nimeshafika Nyololo!" Nilimwandikia. Naye akanijibu; " Kuna jamaa wanatoa ushuhuda wao studioni, nitakuunganisha baada ya dakika 15".

Taratibu nami nikajivuta karibu zaidi kwenye meza ile ya biashara ya mboga mboga iliyozungukwa na akina mama waliokuwa wakifuatilia kinachosemwa kuhusu kilichotokea mahali ambapo wao ndipo walipo kwa wakati huo.

" Kamwene!"- Niliwasalimia kwa Kihehe. Kisha nikajiunga kwenye kusikiliza ' Morning Talk'.

Niliwasikiliza akina mama wale wakijadiliana pia katika baadhi ya waliyokuwa wakiyasikia. Niliwaona wakitingisha vichwa kukubali baadhi ya yaliyokuwa yakisemwa na mashuhuda. Niliwaona pia wakitingisha vichwa kuyakataa baadhi ya yaliyokuwa yakisemwa na mashuhuda.

Nikavuta pumzi, kisha nikawauliza; " Mwenzenu napita njia tu, hivi siku ile ya Jumapili ilikuwaje na mlijisikiaje?"

Nikawaona walivyo na hamu ya kumsimulia ambaye hakuwepo. Nikawasikiliza. Mmoja anasema; hakuwahi hata siku moja kusikia mlio wa bomu. Ilkuwa ni mara yake ya kwanza. Mwingine akaniambia; " Yaani , mimi , niloposikia mabomu tu, nikajifungia ndani na kulala!". Naam, huyu aliugeuza mchana kuwa usiku.

Akina mama wale wanasema, kuwa usiku ule wa Jumapili walikosa hata hamu ya kula chakula. Hawakula chakula. Walilala kwa mashaka pia.

Kando ya meza ile nikawaona watoto wakisogelea na kusikiliza mazungumzo. Nilizioona sura za watoto wenye hofu. Msichana wa miaka 13 akasimulia jinsi alivyokimbilia porini kuhofia maisha yake.

Ndio, kuna watoto wengi wa Nyololo leo ambao wangehitaji msaada wa kisaikolojia kuelewa kilichotokea na kuwapunguzia hofu yao.

Nikiwa nimesimama pale kwenye meza ya biashara nikaisikia simu yangu ikiita. Ni Mtangazaji Gershom Malegesi wa Ebony FM aliyekuwa tayari kuniunganisha na studio. Lakini, kwa nilichokuwa nikikiona na kukisikia pale kutoka kwa wakazi wenyewe wa Nyololo, nikashindwa kuijibu simu ya Malegesi. Sikutaka tena kuunganishwa hewani. Nilihitaji muda wa kutafakari.

Hakika, niliyoyaona kutoka kwa wakazi wa Kijijini Nyololo ni pamoja na hofu, mashaka, hasira na zaidi maswali ya ' Kwa nini?". Kuna wanaojisikia vibaya sana kuona tukio lile baya limetokea kijijini kwao. Kuna wanaojisikia kukatishwa tamaa na mambo ya siasa. Kuwa ambao hawaipendi siasa kwa sasa. Kuna wanaojisikia aibu kuwa Kijiji chao kimejulikana sasa kwa sifa mbaya ya mauaji. Kuna wanajisikia kuwa watu wa kutoka nje wamekuja na kufanya mambo mabaya kijijini kwao.

Nilizunguka kwa miguu kwenye mitaa ya kijiji cha Nyololo. Niliziona teksi mbili tatu kuu kuu ambazo hufanya safari za kutoka barabara kuu hadi vijiji vya ndani. Kuna ambao siku ya tukio gari zao zilikodishwa kuwakimbiza majeruhi au waliotaka kuikimbia Nyololo kwa haraka.

Ndio, niliwaona vijana wale wa Nyololo, wa kike na wa kiume, ambao kwa kawaida ukipita Nyololo huonekana kuchangamka sana, lakini, Ijumaa ile niliyopita Nyololo niliwaona wakiwa kama ' Kuku waliomwagiwa' maji. Wengi hawakuchangamka.

Hata kwenye sura za baadhi yao unaweza kuona, kuwa kuna jambo kubwa limewatokea na wako kwenye kutafakari na labda hofu pia. Maana, redio, runinga na magazeti bado yanazungumzia kilichowatokea.

Na kikubwa nilichokiona ni kuwa; wakazi wa kijijini Nyololo wana ukweli ambao huenda wengine hawaufahamu. Ni wajibu wa wote wenye jukumu la kuusaka ukweli mzima wa kilichotokea kuwasikiliza wakazi wa Nyololo pia.

Na bila shaka, kama Taifa, Nyololo inaweza kutusaidia kufungua ukurasa mpya wa namna iliyo bora na salama ya kwenda mbele kama ndugu wa Taifa moja. Kwamba kilichotokea Nyololo kisitokee tena.

Maggid,
Iringa.
0788 111 765
http://mjengwablog.com

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

KOCHA BENCHIKHA AMESEPA

MASHUSHUSHU WA MAMELODI WALIKUJA KUTUPELELEZA: HERSI