YANGA KUIBUKIA KWA MAAFANDE WA JKT RUVU LEO?


Kikosi cha Mabingwa wa Kombe la Kagame Yanga, ambacho kesho kinashuka Uwanja wa Taifa kuivaa JKT Ruvu katika mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.

DAR ES SALAAM, Tanzania

BAADA ya kuyumba katika mechi mbili za kwanza za Ligi Kuu ya Bara, Yanga, leo Jumamosi wanashuka dimbani kwa mara ya tatu kuwakabili JKT Ruvu ya Pwani kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

Yanga iliyokuwa ikipewa nafasi kubwa ya kufanya vema kutokana na usajili mzuri, iliianza ligi kwa sare ya 0-0 dhidi ya Prisons kabla ya kufungwa 3-0 na Mtibwa Sugar.

Matokeo hayo yanaifanya Yanga leo kukutana na JKT Ruvu ikiwa nafasi ya pili kutoka mkiani, ikiwa na ponti moja, haijafunga bao huku nyavu zake zikitikiswa mara tatu.

Wapenzi na mashabiki wa timu hiyo wameshikwa na butwaa wakihoji yako wapi mashuti ya akina Saidi Bahanunzi, Didier Kavumbagu, Hamisi Kiiza na vipi ukuta imara wa timu hiyo, uruhusu mabao matatu.

Licha ya ukuta wake kusukwa na Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kelvin Yondani, Mbuyu Twite na viungo Athumani Idd ‘Chuji’, Haruna Niyonzima, waliruhusu nyota wa Mtibwa kufunga mara tatu.

Akizungumzia mechi ya leo, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Tom Saintfiet, amewataka nyota wake kusahau kipigo hicho, wapambane kuhakikisha wanashinda kuanza safari upya.

Alisema ni matumaini yake kushinda mechi ya leo licha ya ubora wa wapinzani wao, ambao nao watakuwa wakitaka ushindi kusawazisha makosa ya kufungwa mabao 2-0 na Simba. 

Hata hivyo, Saintfiet alisema kwa kuitambua vizuri taaluma yake, hata ikitokea akapoteza mechi ya leo, hatajuta akitambua kuwa ni sehemu ya mchezo.

Pia, amewasihi wapenzi na mashabiki wa timu hiyo kujitokeza kwa wingi kuipa sapoti timu yao kwa kuishangilia, akitambua kuwa hamasa ina nafasi yake katika kupigania ushindi.

Kuhusu kikosi chake, Tom amesema Bahanunzi, Salum Telela na Juma Seif ‘Kijiko’ ndio majeruhi, wengine wote wako fiti kuipigania timu yao.

Vita nyingine ya ligi hiyo iliyoanza Septemba 15, itakuwa kwenye Uwanja wa Chamazi kwa wenyeji Azam kuwakaribisha wababe wa Yanga, Mtibwa Sugar.

Mechi nyingine itakuwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha kwa JKT Oljoro kuwakabili Polisi Moro huku Coastal Union ikiwaalika Toto African ya Mwanza Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

KOCHA BENCHIKHA AMESEPA

MASHUSHUSHU WA MAMELODI WALIKUJA KUTUPELELEZA: HERSI