Afya ya Ndesamburo yazua utata

Mbunge wa Jimbo la Moshi Mjini, Phillemon Ndesamburo

UTATA umegubika afya ya Mbunge wa Jimbo la Moshi Mjini (Chadema), Philemon Ndesamburo huku taarifa zikidai kuwa anaumwa na anapatiwa matibabu nchini Uingereza.

Wakati hali ikiwa hivyo kwa Ndesamburo, Waziri wa zamani wa Elimu, Jackson Makwetta inaelezwa kuwa hali yake ni mbaya.

Ndugu wa karibu wa mbunge huyo wa zamani wa Njombe Kaskazini aliyekataa kutaja jina lake gazetini, alisema Makweta alianza kusumbuliwa na ugonjwa wa moyo kwa muda mrefu jambo lililosababisha kulazwa katika Hospitali ya Consolata Ikonda iliyopo Wilaya ya Makete Mkoa wa Iringa.

"Hali yake ilianza kubadilika juzi akiwa hospitalini na kulazimika kumhamishia jijini Dar es Salaam ambapo alikodiwa ndege maalumu kwa ajili ya kwenda kupata matibabu zaidi," alisema.

Makwetta aliyetumikia Jimbo la Njombe Kaskazini tangu 1975 hadi 2010 kabla ya kustaafu, alishika nyadhifa mbalimbali ikiwamo Waziri wa Elimu.


Ndesamburo adaiwa kufanyiwa upasuaji

Taarifa zilizozagaa mjini Moshi zinadai Ndesamburo alifanyiwa upasuaji nchini Uingereza na anaendelea vizuri, lakini taarifa nyingine zikidai hajafanyiwa upasuaji bali anasumbuliwa na ugonjwa wa kisukari.

Ndesamburo hajaonekana katika medani za kisiasa kwa takriban mwezi mmoja sasa na hata kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani Kilema Kusini Wilaya ya Moshi Vijijini na Nanjara Reha wilayani Rombo hakushiriki.

Mbali na kutoshiriki katika kampeni hizo, mbunge huyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Kilimanjaro, hakuhudhuria vikao vya Bunge vilivyomalizika Ijumaa kutokana na kuwapo kwake nje ya nchi.

Habari zisizo rasmi zilizopatikana jana zilidai hata mtoto wa Mbunge huyo, Lucy Owenya aliondoka nchini hivi karibuni kwenda nchini Uingereza kwa ajili ya kumuuguza baba yake na bado yuko nchini humo.


Habari zilizomkariri mmoja wa ndugu wa karibu wa familia ya Ndesamburo zilidai mbunge huyo ni mgonjwa, lakini kwa sasa anaendelea vizuri baada ya kutibiwa Uingereza.

“Ni kweli mzee anaumwa, lakini sasa hivi anaendelea vizuri, huo uvumi kuwa hali yake ni mbaya sijui unaanzia wapi,”alisema mwanafamilia huyo aliyekataa jina lake lisitajwe.

Hata hivyo, Owenya ambaye ni mbunge wa Viti Maalumu kupitia Chadema alipoulizwa kwa simu na gazeti hili juzi kutoka nchini Uingereza alikanusha baba yake kuugua.

“Nini? Eti unasema?” aliuliza Owenya kwenye simu na baada ya kuelezwa kuna taarifa zimezagaa baba yake ni mgonjwa alijibu kwa kifupi, "Hakuna kitu kama hicho.”

Habari zaidi zilidai kuwa mbunge huyo anatarajiwa kurejea nchini leo na yuko salama tofauti na taarifa zilizozagaa jimboni kwake kuwa ni mgonjwa.

Katibu wa wabunge wa Chadema, David Silinde alisema kuwa ni kweli Ndesamburo anaumwa na yuko nchini Uingereza kwa matibabu.

"Ni kweli yuko Uingereza anaumwa na anaendelea na matibabu ila anaendelea vizuri."

Silinde ambaye pia ni mbunge wa Mbozi Magharibi alisema, Ndesamburo alikuwa nchini Uingereza kwa mapumziko na kuumwa kwake kulitokea huko huko na si kwamba alikwenda kwa matibabu.

"Alikuwa Uingereza kwenye mapumziko na huko huko hali ya ugonjwa ikamtokea," alisema Silinde na kuongeza: "Nitafuatilia nijue anarudi lini kwa kuwa sasa hivi sina taarifa kamili za kurudi kwake."

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

HATUTOPAKI BASI DHIDI YA YANGA-MOKWENA

“PEMBA SALUTI KWENU” DK. NCHIMBI*

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA