CHADEMA ILIVYOIGARAGAZA CCM USA RIVER ARUSHA.

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimeendelea kudhihirisha umwamba wake katika Mkoa wa Arusha, ambapo kwa mara nyingine tena kimeipiga kikumbo CCM na kutwaa halmashauri mpya ya Mamlaka ya Mji Mdogo wa Usa River.
Ushindi huo unakuja zikiwa ni siku chache tangu chama hicho kiitwae Kata ya Daraja Mbili jijini Arusha ambayo ilikuwa ikiongozwa na diwani wa Chama Cha Mapinduzi, aliyefariki dunia.
Uchaguzi huo ulifanyika kutokana na Halmasuri ya Arumeru Mashariki kugawanywa, na hivyo kuunda halmashauri mpya ya mamlaka ya mji mdogo wa Usa River.
Kabla ya kugawanywa, mitaa yote ilikuwa ikiongozwa na CCM na hivyo, ikalazimika viongozi hao wajiuzulu ili uchaguzi ufanyike upya wa kuwapata wenyeviti wapya wa mitaa tisa.
Hadi tunakwenda mitamboni jana jioni, tayari CHADEMA kilikuwa kimejizolea ushindi mkubwa katika mitaa sita, huku CCM kiking’ara kwenye mitaa mitatu.
Mitaa hiyo na kura zake kwenye mabano ilikuwa Manyata Kati (CHADEMA 118, CCM 78), Nganana (CHADEMA 127, CCM 117), Kisambare (CHADEMA 613, CCM 190), Ngarasero (CHADEMA 785, CCM 355) na Magadini ambako CHADEMA walipata kura 303 dhidi ya 106 za CCM.
Hata hivyo, CCM ilifanikiwa kurejesha mitaa mitatu ya Magadirisho, Mlima Sioni na Usa Madukani.
Kwa ushindi huo, CHADEMA sasa wamefanikiwa kuongoza halmashauri ya pili katika Mkoa wa Arusha, kwani kwa zaidi ya miaka kumi wamekuwa wakiongoza Halmashauri ya Wilaya ya Karatu.
Akizungumza na Tanzania Daima kwa simu jana, Katibu wa CHADEMA Mkoa wa Arusha, Amani Golugwa, alisema kuwa wanataka kuifanya halmashauri mpya ya Usa River iwe ya mfano katika Jiji la Arusha.
“Tumejipanga kuiboresha Usa River kuanzia usafi, mapato na miundombinu yake, kwani CCM wamekuwa wakisuasua, lakini sasa wameachia,” alisema.
CHADEMA kimekuwa kikitoa ushindani mkubwa kwa CCM katika Mkoa wa Arusha kwani hata kwenye uchaguzi mdogo wa ubunge katika Jimbo la Arumeru Mashariki, chama hicho kilitwaa kiti hicho kilichokuwa kikikaliwa na wapinzani wao baada ya aliyekuwa mbunge kufariki.// Tanzania Daima.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

HATUTOPAKI BASI DHIDI YA YANGA-MOKWENA

“PEMBA SALUTI KWENU” DK. NCHIMBI*