FERGUSON APANIA MABAO 100 LIGI KUU ENGLAND
MANCHESTER, England
KOCHA Sir Alex Ferguson, ameshawikika kuamini kuwa, kikosi
chake cha Manchester United kitafanya makubwa msimu huu wa Ligi Kuu, ikiwamo
kutikisa nyavu mara 100 katika mechi tofauti za ligi hiyo.
Rekodi ya karibu kwa Fergie kufikisha idadi hiyo ilikuwa ni
msimu wa 1999/2000, wakati Mashetani Wekundu walipofunga jumla ya mabao 97 na
kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu kwa tofauti ya pointi 18 dhidi ya Arsenal.
Tambo za Fergie msimu huu zimekuja wakati klabu hiyo ikiwa
imefunga mabao kadhaa kupitia wachezaji 13 tofauti, huku Robin van Persie akiongoza
kwa mabao yake 11 katika mechi 14 za mashindano tofauti.
Mabao manane ya Mholanzi huyo katika mechi nane
alizoanzishwa katika Ligi Kuu, yameifanya Man United kufunga jumla ya mabao 26
- kabla ya pambano lao la jana Jumamosi dhidi ya Aston Villa kwenye Uwanja wa
Villa Park.
Fergie anasisitiza kuwa, kikosi chake kina uwezo wa
kuimarika kila uchao na kuwezesha kufunga mara tatu zaidi ya hayo.
Akasema kuwa: “Jambo la kufarahisha kwangu ni kuzidi
kutikisa nyavu zaidi na zaidi kwa kila timu itakayokatiza mbele yetu. Kuwa na
wafungaji tofauti 13 hadi sasa, ni jambo linalotupa nguvu ya ziada katika mechi
zetu.
Comments