JAJI MKUU AJITOA KESI YA LEMA!
JAJI
Mkuu wa Tanzania, Mohamed Othman Chande amejitoa
kusikiliza rufaa ya kesi ya aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema,
badala yake nafasi yake imechukuliwa na Jaji Bernard Luanda.
Kujitoa kwa jaji mkuu kumekuja ikiwa
zimebaki siku tano kusikilizwa upya kwa rufaa hiyo Desemba 4, mwaka huu, baada
ya awali Mahakama ya Rufani, kuona rufaa hiyo ilikuwa na dosari.
Mahakama hiyo ilikubali hoja ya
wajiburufaa kuwa rufaa hiyo ilikuwa na dosari kutokana na tofauti ya vifungu
vya sheria vilivyotumika katika hukumu iliyomvua ubunge Lema na vilivyotumika
katika hati ya kukaza hukumu, iliyowasilishwa mahakamani sambamba na rufaa
hiyo.
Hata hivyo, kilichomwokoa Lema ni
kifungu cha 111 cha Kanuni za Mahakama, ambapo mahakama hiyo ilisema kuwa chini
ya kanuni hiyo, dosari hizo zinaweza kurekebishwa.
Jaji Chande ndiye aliyekuwa kiongozi wa
jopo la majaji watatu katika kesi hiyo akiwamo Salum Massati na Natalia Kimaro. Jaji Mkuu aliingia kwenye kesi hiyo
akichukua nafasi ya Jaji Mbarouk Salim Mbarouk aliyekuwa amepangwa awali,
ambaye sababu za kuondolewa hazikuwekwa wazi.
Wakili wa Lema, Method Kimomogoro alithibitisha kuwa
amepata taarifa kuwa jaji mkuu hatasikiliza rufaa hiyo na badala yake Jaji
Luanda ndiye atachukua nafasi yake.
“Ni kweli jaji mkuu hatakuwapo
kusikiliza rufaa ya Lema nimewasiliana na Msajili Dar es Salaam ameniambia
hatokuwepo kwenye hilo jopo,” alisema Kimomogoro na kuongeza:
Hata hivyo, Wakili Kimomogoro alisema
“Huu ni utaratibu wa kawaida wa mahakama kwa kuwa huenda jaji mkuu akawa
amesafiri au ana shughuli nyingine.”
Wakili wa wajiburufaa, Alute Mughwai
alisema hajapata taarifa kama Jaji Mkuu ameondolewa kwenye jopo hilo kwa kuwa
huo si utaratibu wa mahakama kutoa taarifa hizo.
“Mahakama huwa haitoi taarifa, zinawekwa
(taarifa) kwenye ubao wa mahakama siku ambayo rufaa inasikilizwa,” alisema.
Aliendelea, “Jaji yeyote atakayepangwa
sisi hatuna tatizo kwa kuwa wote ni majaji, wewe uko huko Dar na mimi niko huku
bara (Arusha), hivyo unaweza ukazipata taarifa zaidi huko kwa kuwa ndiyo uko
jikoni Dar.” kwa mujibu wa gazeti la Mwananchi.
Comments