Kampuni ya Century Insurance yakabidhi madawati Shule ya Msingi Majani ya Chai, Kipawa
Meneja
wa Kitengo cha Madai wa Kampuni ya Bima ya Century Michael Emanuel
(kulia), akimkabidhi madawati 100 yenye thamani ya sh.milioni 7.5 Kaimu
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi ya Majani ya Chai, iliyopo Kata ya
Kipawa Manispaa ya Ilala jijini Dar es Salaam leo, Mary Itimay
(kushoto), madawati hayo yametokana na harambee iliyofanywa mwezi juni
mwaka huu na Diwani wa Kata hiyo Bonah Kaluwa kwa kuwashirikisha wadau
mbalimbali ambapo sh.milioni 421 zilipatikana. Wa pili kulia ni Mkuu wa
Utawala wa Kampuni hiyo Colman Macha na Diwani wa Kata ya Kipawa Bonah
Kaluwa.
Meneja
wa Kitengo cha Madai wa Kampuni ya Bima ya Century Michael Emanuel
(kushoto), akiwaelekeza wanafunzi hao jinsi ya kubandika stika za
kampuni hiyo kwenye madawati hayo.
Wanafunzi wakibandika stika katika madawati hayo.
Wanafunzi wakiwa wamekaa kwenye madawati hayo baada ya kukabidhiwa.
Mkuu
wa Utawala wa Kampuni hiyo, Colman Macha na Diwani wa Kata ya Kipawa
Bonah Kaluwa wakiwa wamekaa na wanafunzi hao baada ya kuwakabidhi
madawati hayo.
Wanafunzi hao wakifurahi baada ya kupokea msaada huo. (Picha zote na Dotto Mwaibale)
Shule za Kipawa zapata madawati
Na Dotto Mwaibale
SHULE
tano za msingi katika Kata ya Kipawa Manispaa Ilala Dar es Salaam
zimenufaika kwa msaada wa madawati yalitokana na harambee iliyofanywa na
Diwani wa kata hiyo, Bonah Kaluwa.
Madawati
hayo yalipatikana kupitia wadau mbalimbali kujitokeza kusaidia sekta ya
elimu katika kata hiyo ikiwemo Kampuni ya Bima ya Century ambayo jana,
ilikabidhi madawati 100 yenye thamani ya sh. milioni 7.5 kwa Shule ya
Msingi Majani ya Chai.
Meneja
wa Kitengo cha Madai wa kampuni hiyo, Michael Emanuel akizungumza baada
ya kukabidhi madawati hayo, alisema msaada huo ni sehemu ya mpango wao
katika kusaidia sekta ya elimu nchini.
"Sisi
pia ni wazazi hivyo tuna kila sababu ya kuwasaidia watoto wetu ili wawe
katika mazingira mazuri ya kupata elimu, ndiyo maana tumechukua jukumu
hili," alisema Emanuel.
Emanuel
alisema kuwa tatizo la ukosefu wa madawati ni kubwa, hivyo kila mtu
anapaswa kusaidia ili wanafunzi wapate elimu sahihi na yenye ubora.
Diwani
wa Kata ya Kipawa, Bonah Kaluwa akizungumza katika hafla hiyo, alisema
shule takriban tano za kata hiyo zimenufaika kutokana na harambee
iliyofanyika Juni mwaka huu, ambapo zilipatikana sh. milioni 421.
Alisema
lengo lilikuwa ni kupata madawati 1000, hata hivyo, aliwashukuru wadau
waliojitokeza kwa kuchangia kwani shule hizo zimeweza kupata na visima
saba vya maji ambavyo vimegharimu sh. milioni 75.
Alizitaja shule hizo kuwa ni Mogo, Karakata, Minazi Mirefu, Airwing na Majani ya Chai.
Naye
Kaimu Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Majani ya Chai, Mary Itimay
alisema licha ya kupata madawati hayo, tatizo kubwa walilonalo ni
ukosefu wa vyumba vya madarasa.
"Madawati
yapo tatizo ni vyumba vya madarasa, kwani mahitaji halisi ni vyumba 33,
lakini hivi sasa tuna vyumba 14 tu," alisema Itimay.
Pia alisema shule hiyo yenye wanafunzi 2,239 ina madawati 479 ambayo yamehifadhiwa kwa ajili ya kukosa vyumba vya madarasa.
Comments