KARUME ATENGWA ZANZIBAR MABANGO YAKE YACHOMWA MOTO.



WATU wasiojulikana wamechana mabango yenye picha za Rais mstaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume, katika mitaa mbalimbali ya Manispaa ya Zanzibar, huku umati mkubwa ukijitokeza kumpokea Makamu Mwenyekiti mpya wa CCM Zanzibar, Rais Dk. Ali Mohammed Shein.
Mabango hayo yakiwa na ujumbe wa harakati za maendeleo wakati wa uongozi wake yamechanwa na kuchomwa moto siku chache tangu kutokea mabadiliko makubwa ya uongozi ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar.
Picha za rais huyo mstaafu na aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar zilionekana kuchanwa katika makunato ya barabara ya Kiembesamaki, Michenzani na kuibua shangwe kutoka kwa wanachama wa CCM Zanzibar jana.
Dk. Shein alipokewa juzi kwa kishindo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Zanzibar na wanachama na viongozi wa serikali baada ya kuchaguliwa kushika wadhifa huo.
Mabango hayo yenye nguzo za chuma yalipambwa na serikali katika kuunga mkono juhudi za maendeleo zilizokuwa zikifanywa na Karume na kuweka ujumbe wa maneno na picha kubwa “Rais Amani Karume kinara wa maendeleo Zanzibar,” yalisomeka kabla ya kuchanwa.
Uchunguzi wa Tanzania Daima Jumapili mjini Zanzibar umebaini kuwa kumekuwapo na maelewano mabaya kati ya kiongozi huyo mstaafu na wanachama wa CCM Zanzibar kutokana na kutofahamika msimamo wake kuhusu Muungano tangu Jumuiya ya Uamsho ilipoanza kufanya kampeni za kutaka Zanzibar kujitenga na kusababisha vurugu na uvunjifu wa amani visiwani Zanzibar.
Wakizungumza kwa wakati tofauti baadhi ya Wana CCM jana walisema kwamba kitendo cha Karume kuwafananisha na akili za samaki wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM katika hotuba yake ya shukrani pia kumechangia wanachama kupoteza imani dhidi yake na kuamua kuchana mapambo ya picha zake mitaani.
Haji Ali Kombo, mkazi wa Amani, Zanzibar (45), alisema mafanikio ya Karume ya kisiasa na yake binafsi yasingefanikiwa bila ya wanachama kumpa ridhaa ya kuwaongoza, licha ya kuanguka katika kura za maoni mwaka 2000.
Mussa Hashim Mussa (65), mkazi wa Dimani, alisema pamoja na Karume kuanguka katika kura za maoni mwaka 2000, bado viongozi Tanzania Bara walimbeba, lakini sasa anashindwa kutetea hata misingi ya Muungano wa Tanzania.
Alisema wanachama na viongozi walimpa ridhaa ya kuaongoza kwa heshima ya baba yake, licha ya kuangushwa vibaya katika kura za maoni na wanasiasa wakongwe Zanzibar, akiwamo Dk. Mohamed Gharib Bilal.
Karume aliamua kuwafananisha na akili za samaki wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM walipoanza kukatisha hotuba yake na kumzomea baada ya kuonekana mzito kuzungumzia kwa uwazi vurugu za Uamsho Zanzibar.
Makada hao wa CCM walianza kukatisha hotuba yake na kumtupia lawama kuwa alishindwa kutetea misingi ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar pamoja na kuwa mzito kukemea vurugu zilizokuwa zikifanywa na Uamsho na kuchafua hali ya kisiasa na kusababisha makanisa, baa na mali za serikali kuchomwa moto Zanzibar.
Hata hivyo, tayari viongozi wanane wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (JUMIKI) wamefikishwa mahakamani na kusomewa mashitaka ya uharibifu wa mali na kuhatarisha usalama wa taifa, ambapo dhamana zao zimefungwa na Mkurugenzi wa Mashitaka Zanzibar, Ibrahim Mzee Ibrahim.
Hata hivyo, kauli ya Karume kuwafananisha wajumbe wa mkutano huo na akili za samaki imepokewa kwa shangwe na wafuasi wa Chama cha Wananchi (CUF), ambao wamekuwa wakishangilia, wakimaanisha kuunga mkono kauli hiyo.
Alipoulizwa kuhusu kuchanwa kwa picha za Karume katika Manispaa ya mji wa Zanzibar, Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Zanzibar, Vuai Ali Vuai, alisema hadi jana alikuwa hajapokea taarifa zozote kutoka kwa wasaidizi wake.
Hata hivyo alisema chama kitafuatilia tukio hilo ili kupata ukweli na kuchunguza chimbuko la picha za Karume kuchanwa.Tanzania Daima.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

KOCHA BENCHIKHA AMESEPA

MASHUSHUSHU WA MAMELODI WALIKUJA KUTUPELELEZA: HERSI