MICHELSEN AHOFIA WAKONGO KULETA VIJEBA

Michelsen wa tatu kutoka kulia waliosimama akizungumza na wachezaji wa Serengeti. Kulia kwake ni wasaidizi wake, Jamhuri KIhwelo na Manyika Peter, wakati kushoto kwake ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Serengeti, Kassim Dewji, Katibu wa Kamati, Henry Tandau, Suleiman na Nyambui na Katibu wa TFF, Angetile Osiah.KWA HISANI YA BIN ZUBEIRY BLOG

Na Mahmoud Zubeiry
KOCHA Mkuu wa timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys, Mdenmark Jacob Michelsen amesema kwamba kuelekea mechi ya keshokutwa ana wasiwasi wapinzani wake, Kongo Brazzaville wana wachezaji waliozidi umri.
Akizungumza na BIN ZUBEIRY jana Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam baada ya mazoezi ya jioni, Michelsen alisema kwamba ameichunguza vizuri Kongo na sasa anaifahahamu vema.
Serengeti itamenyana na Kongo keshokutwa Uwanja wa Taifa, katika mchezo wa kwanza wa Raundi ya Tatu na ya mwisho ya kuwania kucheza Fainali za Vijana Afrika zitakazofanyika nchini Morocco mwakani.
Michelsen alisema kwamba alikwenda kushuhudia mchezo wa kwanza wa raundi iliyopita, baina ya Kongo na Zimbabwe waliotolewa na wapinzani wao hao na kujionea makali ya wapinzani wao.
Pamoja na kukiri kwamba Kongo ni timu bora na ilicheza Fainali zilizopita za Kombe la Dunia nchini Mexico mwaka jana na kutolewa raundi ya pili, Michelsen alisema bado ana wasiwasi timu hiyo ina ‘vijeba’.
“Nilipokwenda kuwaangalia wakicheza na Zimbabwe, nilikuta kikosini mwao kuna wachezaji sita wa kikosi kilichokwenda Mexico kwenye Kombe la Dunia, inanitia shaka kwa sababu hakuna mchezaji anayeweza kucheza michuano mikubwa kama ile akiwa ana umri wa miaka 15.
Mimi ni kocha wa vijana na ninajua, haiwezekani. Ucheze fainali za Kombe la Dunia za U17 una miaka 15, hakuna,”alisema Michelsen, ambaye aliwataja baadhi ya wachezaji anaowatilia shaka wamezidi umri ni Hady Binguila na Charvely Mabiat.
Pamoja na hayo, Michelsen amesema ana matumaini ya kuwatoa Kongo kutokana na maandalizi yao ya muda mrefu na pia sapoti anayoipata kutoka kwa viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Kamati maalum iliyoundwa kuhakikisha timu hiyo inafanya vizuri.
Amesema wamecheza mechi za kujipima nguvu 15 zikiwemo dhidi ya timu za Ligi Kuu na hawajafungwa hata moja, kitu ambacho anaamini ni kipimo cha ubora wa timu yake.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Saidia Serengeti Ishinde, Kassim Dewji alisema kwamba wanapambana kwa uwezo wao wote kuhakikisha timu hiyo inakwenda kwenye fainali za Morocco, mwakani.
Dewji aliwataka wachezaji wa timu hiyo kucheza kwa nidhamu, kujituma na kufuata maelekezo ya makocha wao, ili wapate ushindi katika mchezo wa Jumapili.
Serengeti imefanikiwa kufuzu hadi Raundi ya Tatu bila jasho, baada ya wapinzani wake wa awali katika Raundi ya Kwanza na ya Pili, Kenya na Misri kujitoa. Iwapo timu hii itafuzu, hii itakuwa mara ya pili kwa Serengeti kukata tiketi ya kucheza fainali hizo, baada ya mwaka 2005.
Hata hivyo, pamoja na kuzitoa Rwanda, Zambia na Zimbabwe, Serengeti haikwenda Gambia mwaka huo kutokana na kuondolewa kwenye michuano hiyo na Shirikisho la Soka Afrika (CAF), baada ya kubainika walitumia kijana aliyezidi umri, Nurdin Bakari

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

HATUTOPAKI BASI DHIDI YA YANGA-MOKWENA

“PEMBA SALUTI KWENU” DK. NCHIMBI*