NDEVU ZA UAMSHO ZAZUA BALAA WENYEWE WAZIDAI MAHAKAMANI

Sheukh Farid Kabla ya kunyolewa ndevu.
VIONGOZI wa Jumuiya ya Uamsho, Sheikhe Faridi Hadi Ahmed na Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Sheikh Mselem Ali Mselem, wamewasilisha maombi Mahakama Kuu ya Vuga Zanzibar, kutaka kufungua kesi kupinga kunyolewa ndevu wakiwa mahabusu.
Kutokana na ombi hilo, Mahakama Kuu ya Vuga mjini hapa, imekubali ombi hilo na kutoa uamuzi wa kuwaruhusu viongozi hao, wafungue kesi ya madai, kupinga kunyolewa ndevu zao na kutotendewa haki wakiwa mahabusu.

Sheikh Farid na wenzake, wanashtakiwa kwa makosa ya kuhatarisha usalama wa taifa.

Uamuzi wa kuwaruhusu viongozi hao wafungue kesi ya madai, umetolewa jana na Mrajisi wa Mahakama Kuu ya Zanzibar, George Kazi, baada ya kupitia kwa makini maombi ya watuhumiwa hao.

Washtakiwa hao waliwasilisha mambo hayo Novemba 8, mwaka huu, kupitia kwa mawakili wao, wakipinga kitendo cha polisi kuwanyoa ndevu na kutowatendea haki wakiwa mahabusu.

Maombi hayo yaliwasilishwa na washtakiwa wanane, akiwemo Sheikh Farid na Mwenyekiti wa Uamsho, Sheikh Mselem.

Wengine katika kesi hiyo ni Mussa Juma Issa, Suleiman Juma Suleiman, Azan Khalid Hamdan, Khamis Ali Suleiman, Hassan Bakar Suleiman na Ghalib Ahmada Omar.

Akitoa uwamuzi wa kufungua kesi ya kupinga kunyolewa ndevu, Jaji Kazi alisema watuhumiwa wana haki ya kufungua kesi mahakama kuu juu ya kile wanachokilalamikia na kwamba mahakama kuu itakuwa na uamuzi wa kuyasikiliza madai yao tofauti na kesi ya msingi ya uchochezi na kuhatarisha amani.

Kupitia kwa mawakili wao, watuhumiwa hao walidai kuwa wananyimwa uhuru na haki zao za msingi ikiwa ni pamoja na kupigwa marufuku kufuga ndevu wakiwa rumande ya Chuo cha Mafunzo (Magereza).

Katika kesi yao ya msingi, watuhumiwa hao wanakabiliwa na mashtaka manne yakiwemo ya kutoa lugha za uchochezi, kufanya vurugu na kusababisha uharibifu wa miundombinu ya barabara mjini Zanzibar.

Wakizungumzia kesi ya msingi kwa watuhumiwa hao, waendesha mashtaka wa serikali walidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamili na kwamba wanaomba siku nyingine ya kutajwa.

Sheikh Farid baada ya kunyolewa ndevu.
Mrajis huyo wa Mahakama Kuu ya Zanzibar, ameahirisha kesi hiyo hadi Novemba 29, itakapotajwa tena.
Kama kawaida, Jeshi la Polisi lilifunga barabara zote za kuingia na kutoka mahakamani na kuimarisha ulinzi ndani na nje ya mahakama hiyo ambapo kila pembe walionekana makachero wa polisi na Askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), wenye silaha za moto.

Baadhi ya wananchi waliofika mahakamani hapo, waliwataka waandishi wa habari kuandika ukweli kuhusiana na kesi hiyo ili kuinusuru nchi na machafuko.


Watuhumiwa hao wanatetewa na mawakili wa kujitegemea, Salum Toufik na Abdallah Juma Kaka, huku upande wa serikali ukiwakilishwa na Ramadhan Nassibu na wenzake wawil.Tanzania Daima.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

KOCHA BENCHIKHA AMESEPA

MASHUSHUSHU WA MAMELODI WALIKUJA KUTUPELELEZA: HERSI