YANGA KUJENGA UWANJA UTAKAOBEBA MASHABIKI 40,000
KLABU
ya Yanga imesaini makubaliano ya awali na Kampuni ya Beijing
Construction Engineering Group kwa ajili ya ujenzi wa Uwanja wa Kaunda.
Makubaliano
hayo ya awali yalifikiwa na Mwenyekiti wa Yanga Yusuf Manji na Meneja
Mkuu wa Kampuni hiyi David Zhang kwenye makao makuu ya klabu hiyo
yaliyopo kwenye makutano ya mitaa ya Jangwani na Twiga jana.
Ujenzi
wa Uwanja huo utakaotumika kwa ajili ya mechi mbalimbali za timu hiyo
utaanza Juni mwakani na utakapokamilika utakuwa na uwezo wa kuingiza
kati ya watazamaji 30000 na 40000.
Akizungumza
na waandishi wa habari wakati wa makunaliano hayo jana Mwenyekiti wa
Yanga Yusuf Manji alisema wanayo furaha kubwa kuanza safari ya ujenzi wa
uwanja wao na ujenzi huo hautakuwa mwisho wa mipango yao ya kuifanya
klabu hiyo kujitegemea kiuchumi.
“Lengo
ni kuifanya Yanga ijitegemee kiuchumi, wote tumeona makato makubwa ya
TFF, lakini tukiwa na vitega uchumi vyetu tutaifanya Yanga ijitegemee na
kuepukana na makato hayo.”alisema Manji.
Alisema
kwenye mipango yao ya kuitegemeza kiuchumi klabu yao lipo pia jingo lao
la mtaa wa Mafia lakini wameona ni bora kuanza kujenga uwanja sehemu
ambayo ina historia kubwa ya klabu ya Yanga na Tanzania kwa ujumla.
“Lipo
pia jengo la mtaa wa Mafia nalo ni sehemu ya mipango yetu lakini
tumeona tuanze na huku nyumbani sehemu ambayo ina historia ndefu na
klabu ya Yanga na Tanzania kwa ujumla.”alisema Manji.
Manji
alisema chini ya uongozi wake wamedhamiria kufanya kitu kitakachoacha
historia hapa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla hasa ukichukulia
ukweli ya kwamba Yanga ndio timu ya kwanza kwenye ukanda huu kumiliki
uwanja wake.
Alisema
ujenzi wa uwanja sio jukumu la uongozi wa klabu hiyo pekee bali ni
jukumu la kila mwanachama na shabiki wa klabu ya Yanga, hivyo wanaomba
ushirikiano wa hali na mali kutoka kwa mashabiki na wanachama wao
kufanikisha ujenzi huo wa uwanja.
Manji
alisema Jumatatu kampuni hiyo ya ujenzi kutoka China ambayo ndiyo
iliyojenga Uwanja wa Taifa itachukua vipimo kwenye Uwanja wa Kaunda na
Uongozi wa Yanga kuliwasilisha suala la ujenzi huo kwenye Mkutano Mkuu
wa Wanachama wa klabu hiyo Desemba 8.
Alisema
baadhi ya fedha kwa ajili ya uwanja huo wa kisasa watakapo benki na
gharama nyingine zitatokana na michango ya wanachama baada ya kuwa
wamepata gharama nzima za ujenzi za uwanja huo.
Meneja
Mkuu wa Kampuni ya Beijing Cobnstruction Engineering Group alisema
wanafurahia kufikia makubaliano ya awali ya ujenzi wa uwanja na klabu ya
Yanga.
Alisema
wao ndio walijenga Uwanja wa Taifa na viwango vya ujenzi vya uwanja huo
vilisifiwa na timu ya taifa ya Brazil iliyokuja kucheza mechi ya
kirafiki na Tanzania mwaka 2010 ikiwa njiani kuelekea Afrika Kusini
ambako fainali za kombe la Dunia zilifanyika.
Comments