BREAKING NEWS ...KANISA ZANZIBAR LACHOMWA MOTO
Na Mohammed Mhina, wa Jeshi la Polisi
WAKATI Watanzania wakiendelea kutafakari tukio la kuuawa kwa kupigwa
risasi kwa Padre Evaristus Mushi, wa Kanisa Katoriki Zanzibar, watu
wasiojulikana wamelishambulia kwa mawe na baadaye kulichoma moto Kanisa
la Walokole la Shaloom lililoko eneo la Kiyanga kwa Sheha mkoa wa Kusini
Unguja, Zanzibar.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Kusini Unguja Zanzibar, ACP Augostine Olomi,
alisema leo kuwa tukio hilo limetokea majira ya saa 9.30 usiku.
Amesema moto huo ulizuka mara baada ya kikundi cha watu watatu kuonekana
wakipita njia karibu na kanisa hilo na baada ya muda mlinzi wa kanisa
hilo alisikia kanisa likishambuliwa kwa mawe juu ya mapaa.
Amesema baada ya mlinzi huyo kubaini kuwepo kwa hatari, alilazimika
kukimbia kwenda kujificha lakini huku akiangalia kwa mbali
kinachoendelea.
Kamanda Olomi amesema kuwa wakati mlinzi huyo akiwa amejibanza mafichoni
huku akiangalia kinachotokea, mara aliona moto ukiwaka ndani ya kanisa
na ndipo alipopiga simu kwa kiongozi wa kanisa hilo naye kuwajulisha
Polisi.
Amesema Polisi walipofika hapo walisaidiana na wananchi kuuzima moto huo
lakini wakati huo tayari ulishateketeza thamani za kanisa hilo na vitu
vingine vilivyokuwa kanisani hapo.
Kamanda Olomi amesema moto huo ungeweza kusababisha athali kubwa kama
usingedhibitiwa mapema.
Hata hivyo amesema uimara wa dali lililotengenezwa kwa Gibsam kumesaidia
kuunusuru moto huo kuunguza mapaa na kuliteketeza kabisa kanisa hilo.
Amesema wakati uongozi wa kanisa hilo ukifanya tathimini ya harasa
iliyopatikana kutokana na moto huo, Jeshi la Polisi limeanza kuwasaka
washukiwa kwa kutafuta taarifa kwa raia wema na bado hakuna mtu ama watu
waliokamatwa kuhusika na tukio hilo.
Hata hivyo Kamanda Olomi amesema Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na
vikundi vya Ulinzi Shirikishi na Polisi Jamii, wataanza utaratibu wa
kuyalinda makanisa yote ili kuzuia matishio mengine kama hayo.
Comments