Chadema wamwakia Spika Makinda.DK SLAA AMTAKA ATOE MAJIBU YA RUFAA ZAO, KAMATI YA MAADILI KUCHUNGUZA VURUGU ZILIZOTOKEA

WAKATI Spika wa Bunge, Anne Makinda akitangaza kufutwa kwa hoja zote binafsi za wabunge kutokana na vurugu zilizotokea bungeni juzi na jana, Chadema kimewataka wabunge wao wasiende kwenye Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge hadi pale rufaa zao 10 zitakapotolewa uamuzi.

Rufaa hizo ni pamoja na ile ya Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu kulitaka Bunge lisitishe uamuzi wa kupewa ujaji wa Mahakama Kuu, jaji mmoja kwa madai kuwa hana vigezo vya kuwa na nafasi hiyo.

Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa alitoa msimamo huo jana baada ya Spika Makinda kueleza bungeni kuwa Lissu ndiye kinara wa vurugu, huku ikielezwa kuwa Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge itamchukulia hatua za kinidhamu.

Kabla ya Spika Makinda kuahirisha Bunge, kulitokea mvutano kati yake na Mbunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki, Joshua Nassari baada ya Makinda kumweleza kuwa hajui kanuni hivyo atulie.

Hata hivyo, alimruhusu kuzungumza na ndipo Nassari alipopinga Kamati ya Uongozi ya Bunge kufuta hoja binafsi za wabunge akieleza ni kinyume cha kanuni za Bunge kufanyika kitu hicho.

Kabla ya Spika Makinda kujibu, Lissu alisimama na kuomba mwongozo wa Spika akisema; “Mheshimiwa Spika tunataka utueleze tutaendelea kukata rufaa hadi lini, wakati una rufaa zetu 10 kuanzia mwaka juzi na hujazitolea uamuzi, naomba mwongozo wako Mheshimiwa Spika,” alisema Lissu na kujibiwa na Spika Makinda kuwa, “Rufaa hizo zinafanyiwa kazi na zitatolewa uamuzi.”

Makinda aliliahirisha Bunge kwa kile alichosema kukithiri kwa vitendo vya utovu wa nidhamu ndani ya Bunge hilo na kufuta hoja binafsi ambazo hutolewa na kuchangiwa baada ya kipindi cha maswali na majibu.

Makinda alisema: “Waheshimiwa wabunge, tangu Januari 30, hadi jana (juzi) Februari 4, 2013 tuliamua kuwasilisha bungeni hoja binafsi za wabunge ambazo ziliahirishwa katika mkutano wa tisa wa Bunge kwa nia njema ya kujadiliana masuala makubwa ya kitaifa na kuishauri Serikali nini kifanyike ili kukabiliana na matatizo mbalimbali yanayowahusu wananchi.

“Hata hivyo, imelazimu kuahirisha mijadala yote ya hoja binafsi kutokana na tabia iliyojitokeza ya utovu wa nidhamu kwa baadhi ya wabunge na hivyo kuamua kwa makusudi kuanzisha vurugu na kulifanya Bunge kupoteza heshima yake,” alisema Spika Makinda.

Alisema kutokana na hali hiyo, Kamati ya Uongozi imekubaliana kuwa suala hilo lipelekwe kwenye Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge ili ilichunguze na kuwasilisha mapendekezo yake kabla ya mkutano unaoendelea kumalizika na kwamba hoja zote binafsi zisiwasilishwe kutokana na utovu wa nidhamu ambao ungeweza kujitokeza katika hoja zilizobakia.

Hata hivyo, Lissu alisema kuwa kelele za kutetea taratibu na kanuni ndizo zinamfanya aonekane kuwa ana utovu wa nidhamu.

“Spika anaonyesha upendeleo wa waziwazi, anakiuka kanuni kwa makusudi. Mimi nitasema, sitaogopa kamati, hata nikiitwa nitasema... Sasa tunachokifanya, tumekutana leo (jana) na tumeandaa taarifa ya kutaka Spika aondolewe yeye na naibu wake, hii tutaiwasilisha kama taarifa kati ya kesho (leo) na keshokutwa (kesho),” alisema Lissu.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

KOCHA BENCHIKHA AMESEPA

MASHUSHUSHU WA MAMELODI WALIKUJA KUTUPELELEZA: HERSI