KAMATI YA UTENDAJI TFF KUJADILI TAMKO LA SERIKALI
Sekretarieti
ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imepokea barua ya
Serikali ikielezea uamuzi wa Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na
Michezo, Dk. Fenella Mukangara kutengua uamuzi wa Msajili wa Klabu na
Vyama vya Michezo nchini kuidhinisha marekebisho ya Katiba ya TFF toleo
la 2012.
Baada
ya kupokea barua hiyo jana alasiri (Februari 25 mwaka huu),
Sekretarieti iliwasiliana na Rais wa TFF, Leodegar Tenga ambaye ameagiza
kuitishwa kikao cha dharura cha Kamati ya Utendaji kujadili tamko hilo.
Kikao hicho cha Kamati ya Utendaji ya TFF kitafanyika Jumamosi (Machi 2 mwaka huu) jijini Dar es Salaam.
KOCHA AZAM AFUNGIWA KWA KUCHOJOA BUKTA
Kocha Mkuu wa
Azam, Stewart John Hall amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh.
500,000 kwa kushusha bukta yake na kumlalamikia mwamuzi msaidizi wakati
wa mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kati ya timu yake na Kagera Sugar
iliyochezwa Januari 26 mwaka huu Uwanja wa Azam Complex ulioko Chamazi,
Dar es Salaam.
Adhabu hiyo
imetolewa na Kamati ya Ligi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF) iliyokutana mwishoni mwa wiki kupitia ripoti za michuano ya VPL na
Ligi Daraja la Kwanza (FDL) msimu wa 2012/2013 inayoendelea hivi sasa
na kufanya uamuzi mbalimbali.
Naye Kocha
Msaidizi wa timu ya Mgambo Shooting, Denis Mwingira ametozwa faini ya
sh. 500,000 kwa kumtolea lugha chafu mwamuzi kwenye mechi dhidi ya
Mtibwa Sugar iliyochezwa Oktoba mwaka jana katika Uwanja wa Manungu.
Ally Jangalu
ambaye ni Kocha Msaidizi wa Polisi Morogoro naye ameangukiwa na rungu la
Kamati ya Ligi kwa kupigwa faini ya sh. 500,000 baada ya kutolewa
kwenye benchi kwa kupinga uamuzi wa refa kwa sauti ya juu. Alitenda kosa
hilo kwenye mechi kati yao na Kagera Sugar iliyochezwa Novemba 10 mwaka
jana Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.
Matukio ya
aina hiyo kwa kocha Jangalu yamekuwa ya kujirudiarudia ambapo Oktoba 13
mwaka jana katika mechi dhidi ya Azam iliyochezwa mjini Morogoro
aliondolewa na mwamuzi kwenye benchi kwa kuchochea wachezaji wa timu
yake wacheze rafu.
Naye Kocha wa
timu ya Moro United inayoshiriki FDL, Yusuf Macho amepigwa faini ya sh.
200,000 kwa kumtolea lugha chafu refa baada ya mechi dhidi ya Transit
Camp iliyofanyika Novemba 4 mwaka jana Uwanja wa Mabatini mjini
Mlandizi.
Pia Kocha wa
Burkina Faso, Hasheem Mkingie amepigwa faini ya sh. 200,000 baada ya
kutolewa kwenye benchi kwa kutoa lugha chafu katika mechi ya FDL dhidi
ya Mkamba Rangers.
Kiongozi wa
Majimaji, Joseph Nswila ambaye aliingia uwanjani baada ya mechi dhidi ya
Mlale JKT kumalizika na kuvamia waamuzi amefungiwa miezi sita.
Vilevile timu
ya Azam imepigwa faini ya sh. 300,000 kwa kuchelewa kufika uwanjani
kwenye mechi kati yao na JKT Oljoro iliyochezwa Novemba 7 mwaka jana
katika Uwanja wao wa Azam Complex ulioko Chamazi, Dar es Salaam.
Pia Coastal
Union imetozwa faini ya sh. 500,000 kutokana na washabiki wake kumrushia
chupa za maji mwamuzi msaidizi namba mbili wakati wa mechi yao dhidi ya
Simba iliyochezwa Oktoba mwaka jana Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.
Nayo klabu ya
African Lyon imepigwa faini ya sh. 500,000 kwa timu yake kugoma kuingia
kwenye chumba cha kubadilishia nguo wakati wa mapumziko katika mechi
dhidi ya Coastal Union iliyochezwa Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga,
Oktoba 24 mwaka jana.
Timu ya
Burkina Faso ya Morogoro imepigwa faini ya sh. 200,000 kutokana na
kuonesha vitendo vya ushirikina kabla ya mechi yao dhidi ya Mbeya City
iliyochezwa Oktoba 24 mwaka jana Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.
Faini ya
ushirikina ya sh. 200,000 pia imepigwa timu ya Pamba baada ya kuonesha
vitendo hivyo kwenye mechi yao dhidi ya Mwadui iliyochezwa Novemba 4
mwaka jana Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.
Nayo Mkamba
Rangers imepigwa faini ya sh. 200,000 baada ya washabiki wake kumtolea
lugha chafu Katibu wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Morogoro (MRFA),
Hamis Semka na kumrushia chupa za maji mwamuzi wa mezani katika mechi
dhidi ya Mbeya City iliyochezwa mjini Morogoro.
Polisi Dodoma
imepigwa faini ya sh. 200,000 kutokana na washabiki wake kuvamia
uwanjani na kutaka kuwapiga waamuzi katika mechi yao dhidi ya JKT
Kanembwa na kusababisha mipira miwili ya Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa
wa Dodoma (DOREFA) kupotea.
Pia klabu
kadhaa zimeandikiwa barua za onyo kwa timu zao kuchelewa kufika uwanjani
au kutofika kwenye mkutano wa maandalizi ya mechi (Pre-match meeting).
Klabu hizo ni Coastal Union, JKT Ruvu, Toto Africans, Simba, Green
Warriors, Majimaji, Mkamba Rangers, Polisi Dodoma, JKT Kanembwa, Moro
United.
Mchezaji
Stanley Nkomola wa JKT Ruvu baada ya mechi dhidi ya Coastal Union
alikwenda jukwaani na kuanza kupigana na washabiki. Pia kipa wa timu ya
Transit Camp, Baltazar Makene baada ya mechi dhidi ya Tessema aliruka
uzio na kwenda kupigana na washabiki.
Kwa vile
masuala ya wachezaji hao ni ya kinidhamu yamepelekwa kwenye Kamati ya
Nidhamu inayoongozwa na Kamishna wa Polisi (CP) mstaafu Alfred Tibaigana
kwa ajili ya kuchukuliwa hatua.
MWAMUZI FIFA, MAHAGI WAONDOLEWA VPL
Mwamuzi
Msaidizi wa FIFA, Ferdinand Chacha ameondolewa kuchezesha mechi za VPL
baada ya kupata alama za chini kwenye mechi kati ya African Lyon na
Simba iliyochezwa mwezi uliopita Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Waamuzi
wanaopata alama 6.5 au chini ya hapo kati ya 10 zinazohitajika pia
wanaondolewa kwenye mechi za VPL na FDL.
Waamuzi
wengine walioondolewa kwa kutomudu mechi walizochezesha za VPL ni Mathew
Akrama (Yanga vs Simba), Ephrony Ndissa (Yanga vs Simba), Ronald Swai
(Yanga vs Mtibwa Sugar).
Walioondolewa
kwa kupata alama za chini ni Alex Mahagi (Simba vs JKT Ruvu), Methusela
Musebula (Toto Africans vs Coastal Union), Lingstone Lwiza (Toto
Africans vs Coastal Union), Idd Mikongoti (Toto Africans vs Mtibwa
Sugar) na Samson Kobe (Toto Africans vs Mtibwa Sugar).
Masoud Mkelemi
aliyekuwa mwamuzi wa mezani katika mechi ya FDL kati ya Moro United na
Villa Squad ameondolewa kwa kutofika kwenye mkutano wa maandalizi ya
mechi (Pre-match meeting) na alichelewa kwa dakika tano kufika uwanjani.
MAKAMISHNA VPL/FDL WASIMAMISHWA, WAONYWA
Baadhi ya
makamishna wa VPL na FDL wameondolewa na wengine kusimamishwa kusimamia
mechi za ligi hizo kutokana na upungufu kwenye ripoti zao au
kutowasilisha kabisa ripoti hizo TFF baada ya mechi.
Kamishna
Mohamed Jumbe aliyesimamia mechi kati ya Mgambo Shooting na Simba
ameondolewa kwenye orodha ya makamishna kutokana na ripoti yake kuwa na
upungufu.
Makamishna wa
mechi kati ya JKT Oljoro vs Yanga (Hakim Byemba), JKT Oljoro vs Kagera
Sugar (Salum Kikwamba), Toto Africans vs African Lyon (Charles Komba),
Coastal Union vs JKT Oljoro (Mohamed Nyange) wamesimamishwa hadi
watakapowasilisha ripoti zao TFF.
Kwa upande wa
FDL makamishna waliosimamishwa hadi watakapowasilisha ripoti zao TFF ni
wa mechi kati ya Kurugenzi vs Polisi Iringa, Morani vs Mwadui, Polisi
Mara vs Pamba, Polisi Mara vs Mwadui, Morani vs JKT Kanembwa na Pamba vs
Polisi Dodoma.
Wengine ni
Mwadui vs JKT Kanembwa, Polisi Tabora vs Morani, Polisi Dodoma vs Polisi
Mara, Polisi Tabora vs Mwadui, Polisi Mara vs Morani, JKT Kanembwa vs
Polisi Mara, Morani vs Rhino Rangers na Small Kids vs Mkamba Rangers.
Kamati ya Ligi
imewakumbusha makamishna wote kuwa ni jukumu lao kuhakikisha ripoti zao
zimefika TFF na kurekebisha upungufu wa jinsi ya kuripoti matukio
yanayotokea uwanjani. Licha ya kutuma nakala kwa njia ya email,
wanatakiwa pia kuwasilisha ripoti halisi (original) TFF.
MECHI YA SIMBA, MTIBWA YAINGIZA MIL 62/-
Mechi namba
121 ya Ligi Kuu ya Vodacom iliyochezwa juzi (Februari 24 mwaka huu)
kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kumalizika kwa Mtibwa Sugar
kuibuka ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Simba imeingiza sh. 239,686,000.
Watazamaji
10,669 walikata tiketi kushuhudia mechi hiyo ambayo viingilio vilikuwa
sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000 huku kila klabu ikipata
mgawo wa sh. 14,577,252.45 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT)
iliyolipwa ni sh. 9,467,694.92.
Kiingilio cha
sh. 5,000 ndicho kilichovutia watazamaji wengi ambapo waliokata tiketi
hizo walikuwa 9,491 na kuingiza sh. 47,455,000 wakati idadi ndogo ya
washabiki ilikuwa ya kiingilio cha sh. 20,000 kilichovutia washabiki 105
na kuingiza sh. 2,100,000.
Mgawo mwingine
wa mapato hayo ni asilimia 15 ya uwanja sh. 7,412,162.26, tiketi sh.
3,183,890, gharama za mechi sh. 4,447,297.36, Kamati ya Ligi sh.
4,447,297.36, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh.
2,223,648.68 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA)
sh. 1,729,504.53.
VUMBI LA VPL KUENDELEA JUMATANO
Michuano ya
Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania Bara inaendelea
kesho (Februari 27 mwaka huu) kwa mechi tano zitakazochezwa katika
viwanja tofauti.
Vinara wa ligi
hiyo Yanga wataikaribisha Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam kwa viingilio vya sh. 5,000 (viti vya bluu na kijani), sh. 8,000
(viti vya rangi ya chungwa), sh. 15,000 (VIP C na B) na sh. 20,000 (VIP
A).
Mechi nyingine
za ligi hiyo ni Coastal Union vs Ruvu Shooting (Mkwakwani, Tanga),
Polisi Morogoro vs Mgambo Shooting (Jamhuri, Morogoro), JKT Ruvu vs Toto
Africans (Azam Complex, Dar es Salaam) na Mtibwa Sugar vs Tanzania
Prisons (Manungu, Morogoro).
Boniface Wambura Mgoyo
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
Comments