MAKALA MAALUM KUHUSU MKAKATI WA GEWE II KATIKA KUTOKOMEZA UKATILI WA KIJINSIA HAPA NCHINI



Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), Valeria Msoka (katikati), akiwa na viongozi wa Mashirika ya Kutetea haki za Binadamu. Kutoka kushoto ni Salome Assey kutoka TAWLA, Elizabeth Muhangwa wa Kituo cha Usuluhishi (CRC) , Fesliter Mwanyingili kutoka TGNP na Mratibu wa TAMWA Zanzibar, Mzuri Issa. (Makala hii imeandaliwa na www.mwaibale.blogspot.com)

Na Dotto Mwaibale

UKATILI wa kijinsia ni moja ya tatizo kubwa hapa nchini, hali inayowafanya baadhi ya waathirika kukimbia katika maeneo wanayoishi ili kukwepa vitendo hivyo.

Hali hii ya ukatili inatokana na baadhi ya mila na tamaduni zilizozoeleka katika baadhi ya maeneo husika ambapo hapo awali waliona ni jambo la kawaida licha ya kwamba ulikuwa na madhara kwa mtu aliyefanyiwa jambo hilo.

Ukatili huu umegawanyika katika makundi tofauti kwani upo unaotokana na vitendo vya ukeketaji, kunyimwa haki ya kupata elimu kutokana na jinsia ya mtu hasa wanawake.

Mwingine ni kuwanyima haki ya kupata elimu watoto waliozaliwa na ulemavu ikiwa ni pamoja na kuwatenga na kuwafungia ndani hata kuwafanyia ubakaji.

Eneo lingine la ukatili wa kijinsia ni kumuozesha mtoto akiwa chini ya umri wa miaka 18  bila ya ridhaa yake ili mradi wazazi au walezi wake wameamua kufanya hivyo.

Kutokana na kuwaoza mabinti katika utaratibu huo wengi wao wamejikuta wakishindwa kupata elimu na wale wanaopinga vitendo hivyo wamekuwa wakikimbia familia hizo na kwenda kuomba msaada wa kisheria, elimu na hifadhi.

Vitendo hivyo vimekuwa vikifanyika katika baadhi ya mikoa yetu hasa ile inayojishughulisha na ufugaji ambapo wamekuwa wakithamini zaidi mali zitokanazo na kuolewa kwa msichana husika bila ya kujali haki zake za msingi ikiwa ni pamoja ya kupata elimu.

Baadhi ya wasichana hao waliokimbia na kufanikiwa kupata elimu wamekuwa wanaharakati wazuri wa kupinga ukati wa jinsia hivyo kuwa msaada mkubwa kwa wengine kwa kutoa elimu.

Serikali kwa upande wake imekuwa ikiwakamata watu wanaojihusisha na vitendo hivo vikiwemo ukeketaji, kuwaozesha watoto kwa lengo la kupata mali na wale wanaofanyiwa vitendo vya ndivyo sivyo katika jamii.

Kutokana na kubaini kukithiri kwa vitendo hivyo, mashirika matano ya kutetea haki za binadamu yaliamua kuungana na kufanya utafiti wa awali kupitia Mradi wa Gewe II kuhusu ukatili wa kijinsia nchini kwa ufadhili wa Denmark.

Utafiti wa awali uliofanywa na mashirika hayo ulibaini waathirika wa matukio hayo hawana sehemu maalumu ya kupeleka malalamiko yao.

Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa  Habari Wanawake Tanzania (Tamwa), Valeria Msoka anasema utafiti huo umefanywa na mashirika hayo matano ambayo ni Chama cha Wanasheria Wanawake (Tawla), Chama cha Wanasheria Wanawake Zanzibar (Zafela), Kituo cha Usuluhishi (CRC), Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) na Tamwa yenyewe.

Msoka anasema utafiti huo umeonesha asilimia 17 ya wananchi hawana uelewa wa sheria za ukatili hali inayochangia kutokufuatilia haki zao wakati wa uvunjaji na wakati mwingine kutoripoti kesi hizo.

Anazitaja wilaya zilizofanyiwa utafiti huo kuwa ni Wete (Pemba Kaskazini), Magharibi Unguja, Kusini Unguja (Kusini Unguja), Kisarawe (Pwani), Newala (Mtwara), Lindi Vijijini (Lindi), Mvomero (Morogoro) na wilaya mbili za Kinondoni na Ilala (Dar es Salaam).

Msoka anazungumzia ofisa mmoja wa Polisi mkoani Lindi ambaye anabainisha kuwa kesi  nyingi huripotiwa katika hatua ya familia na hufikishwa mahakamani baada ya kushindwa kupata suluhu hivyo kuwa katika hatari ya kupata haki.

Anasema utafiti huo kwa ujumla uliona asilimia 47 za kesi huripotiwa katika Serikali za Vijiji, asilimia 25 huripotiwa polisi nyingine huripotiwa Kamisheni ya Haki za Binadamu, mashirika ya haki za binadamu na kwa wanasheria wanaongoza (Para Legals).

"Hali hiyo ya kutokuwa na mfumo maalumu wa kuripoti inaweka mazingira ya kutopatikana kwa haki na pia kukosekana kwa takwimu sahihi za kesi za ukatili," anasema Msoka.

Anasema taarifa hiyo inaonesha kuwa wananchi hawana majukwaa ya kukaa pamoja na kujadili changamoto zao ambapo ni asilimia 13.5 ndiyo wanachama wa Vyama vya Kijamii (Civil Society Associations)

Mpango huo umewafikia watu asilimia 56 kupitia vipindi mbalimbali vya redio, televisheni na magazeti ambapo kwa upande wa Unguja Magharibi umewafikia watu kwa kiwango kikubwa cha asilimia 72.2 ukilinganisha na Kinondoni ambayo ina asilimia 47.2.


Katika vyombo vikuu vya habari vitatu, redio imekuwa ni maarufu zaidi kwa kuwagusa watu kutokana na vipindi vyao kwa asilimia 56.8 ikifuatiwa na televisheni kwa asilimia 36.6 na magazeti asilimia 6.6.

"Katika Wilaya ya Mvomero ni watu asilimia 18.8 waliopokea mpango huo tofauti na Newala kwa asilimia 8.9, jambo linalohitaji jitihada zaidi ili kila mwananchi kuufahamu mpango huo ikiwezekana nchi nzima," anasema Msoka.

Ofisa Programu wa TGNP, Felister Mwanyingili anasema katika utafiti huo umeonesha watu kuwa na uwoga wa kutoa taarifa baada ya kufanyiwa vitendo hivyo hasa pale baba wa familia anapokuwa amebainika kutenda kosa la ubakaji.

Anasema kazi kubwa inayofanywa na TGNP ni kutoa elimu kwa wananchi, viongozi maofisa watendaji, mahakama mahospitalini na kwa wanasheria ili kuhakikisha kunakuwa na upatikanaji mzuri wa vielelezo.

"Tunashirikisha makundi hayo kwa kuwa yanawajibika moja moja pale inapotokea tukio kama la ubakaji ambapo muathirika atapelekwa ofisi ya kata, hospitali, polisi, mahakamani na kwa wanasheria," anasema Mwanyingili.

Anaweka wazi kuwa mara nyingi kesi hizo zinachukua muda mrefu kwa kukosa ushirikiano wa makundi hayo hivyo kumnyima haki mlalamikaji.

Anasema ukatili wa kijinsia si tu kwa mtu kubakwa hata anapokosa haki ya kupata elimu bora kutokana na shule husika kutokuwa na walimu na vifaa vya kufundishia, huo ni ukatili wa kijinsia.

Ukatili mwingine wa kijinsia ni kukosa kwa huduma mbalimbali kama vile za afya na nyingine nyingi ambazo mtu anastahili kuzipata lakini hazipati.

Mashirika hayo matano ya kutetea haki za binadamu yanatekeleza Mpango wa Usawa wa Jinsia na Uwezeshaji wa Wanawake (GEWE) ambao unafanywa kwa mashirikiano na Serikali ya Denmark.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

HATUTOPAKI BASI DHIDI YA YANGA-MOKWENA

“PEMBA SALUTI KWENU” DK. NCHIMBI*